Matendo ya Mitume 22

Matendo ya Mitume 22

Paulo anasema na watu.

1Waume mlio ndugu na baba, sikilizeni, ninayojikania sasa mbele yenu![#Tume. 7:2; 13:26.]

2Waliposikia, ya kuwa anasema nao kwa msemo wao wa Kiebureo, wakakaza kunyamaza.[#Tume. 21:40.]

(3-21: Tume. 9:1-29; 26:9-20.)

3Akasema: Mimi ni mtu wa Kiyuda, nimezaliwa Tarso katika nchi ya Kilikia. Nikalelewa humu mjini, nikakaa miguuni pa Gamalieli na kufundishwa Maonyo ya baba zetu kwa uangalifu wote. Nikajipingia kumfanyia Mungu kazi, kama nanyi nyote leo.[#Tume. 5:34.]

4Njia hiyo nikaifuata, mpaka nikiua watu; waume na wake nikawafunga na kuwatia kifungoni.[#Tume. 8:3.]

5Hayo hata mtambikaji mkuu na wazee wote watanishuhudia. Kisha nikapewa barua nao za kwenda kwa ndugu walioko Damasko, nako niwafunge wale waliokuwako, niwalete Yerusalemu, wapatilizwe.

6Lakini nilipokwenda na kufika karibu ya Damasko, ilipokuwa saa sita ya mchana, mara palitoka mwanga mkubwa mbinguni, ukanimulikia pande zote.

7Nikaanguka chini, nikasikia sauti iliyoniambia: Sauli, Sauli, unanifukuzaje?

8Nami nilipojibu: Ndiwe nani, Bwana? akaniambia: Mimi ni Yesu wa Nasareti, ambaye unanifukuza wewe.

9Nao wenzangu, tuliokuwa pamoja, waliuona mwanga, lakini aliyesema nami hawakumsikia sauti yake.

10Nilipouliza: Nifanyeje, Bwana? Bwana akanijibu: Inuka, uende Damasko! Ndimo, utakamoambiwa yote, uliyoagizwa kuyafanya.

11Kwa hivyo, nilivyokuwa sioni kwa kumetuka kwake ule mwanga, nikashikwa mkono na wenzangu, nikaingia Damasko.

12Kulikuwa na mtu, jina lake Anania, ni mwenye kuyashika Maonyo yote, kama wanavyomshuhudia Wayuda wote wanaokaa huko.

13Huyo akanijia, akasimama mbele yangu, akaniambia: Ndugu yangu Sauli, uwe mwenye kuona! Nami saa ileile nikapata kuona.

14Kisha akasema: Mungu wa baba zetu amekuchagua huko kale, upate kuyatambua, ayatakayo, umwone naye Mwongofu wake, uisikie na sauti ya kinywa chake mwenyewe,

15anavyokuambia: Utakuwa shahidi wangu kwa watu wote ukiwaambia, uliyoyaona nayo uliyoyasikia.

16Sasa unakawilia nini? Inuka, ubatizwe na kuoshwa, makosa yako yakuondoke, ukilitambikia Jina lake!

17Niliporudi Yerusalemu nikaja kuombea Patakatifu; hapo nikazimia roho,

18nikamwona, naye akaniambia; Piga mbio, utoke upesi Yerusalemu! Kwani hawatakupokea, ukinishuhudia mimi.

19Nam nikasema: Bwana, wao wenyewe wanajua, mimi nilivyowafunga waliokutegemea na kuwapiga mo mote nyumbani mwa kuombea.[#Tume. 22:4.]

20Napo hapo, damu ya shahidi wako Stefano ilipomwagwa, mimi mwenyewe nilikuwa nimesimama hapohapo kwa kupendezwa, nikayalinda mavazi yao wale waliomvua.[#Tume. 7:58; 8:1.]

21Naye akaniambia: Enenda tu! Kwani mimi nitakutuma, uende mbali kwa wamizimu.[#Tume. 9:15; 13:2.]

22Ndipo, wale waliomsikiliza mpaka neno hili walipopaza sauti wakisema: Mwondoe huyu nchini! Kwani haimpasi kuwapo.[#Tume. 21:36.]

23Walipopiga kelele hivyo na kuzirarua nguo zao na kutupa uvumbi juu angani,

24mkuu wa kikosi akaagiza, aingizwe bomani; akasema, wamwulize kwa mapigo, apate kuijua sababu ya kumpigia makelele kama hayo.

25Walipomfunga kwa mikanda, apigwe, Paulo akamwambia bwana askari aliyesimama hapo: Je? Mko na ruhusa kupiga mtu aliye Mroma, asipohukumiwa kwanza?[#Tume. 16:37-38; 23:27.]

26Bwana askari alipovisikia hivi akamwendea mkuu wa kikosi, akamjulisha akisema: Wataka kufanya nini? Kwani mtu huyu ni Mroma.

27Mkuu wa kikosi akamwendea, akamwambia: Niambie, wewe u Mroma? Naye akasema: Ndio.

28Mkuu wa kikosi alipojibu: Mimi huu Uroma nimeununua kwa fedha nyingi, Paulo akasema: Mimi nimezaliwa nao.

29Papo hapo wale waliotaka kumwuliza kwa mapigo wakamwacha. Naye mkuu wa kikosi akaogopa alipotambua, ya kuwa ni Mroma, kwani yeye alimfunga.

Paulo mbele ya wakuu.

30Kesho yake alitaka kuyatambua mashtaka ya Wayuda, kama ni ya kweli; kwa hiyo akamfungua, akaagiza, watambikaji wakuu na baraza yote ya wakuu wakusanyike pamoja, akampeleka Paulo chini kwao, akamsimamisha mbele yao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania