Matendo ya Mitume 26

Matendo ya Mitume 26

Paulo mbele ya Agripa.

1Agripa alipomwambia Paulo: Una ruhusa kujisemea mwenyewe, ndipo, Paulo aliponyosha mkono, akajikania hivyo:

2Mfalme Agripa, ninashangilia moyoni, kwa kuwa yote, ninayosutwa na Wayuda, nitajikania leo mbele yako wewe,

3uliyeyatambua sanasana mazoea na mashindano yote ya Kiyuda. Kwa hiyo nakuomba, unisikilize kwa kuvumilia.

4Mwendo wangu ulivyokuwa hapo mwanzo, nilipokuwa kijana pamoja na vijana wenzangu huko Yerusalemu, Wayuda wote wanavijua.

5Kwani wamenitambua kale; wakitaka wangenishuhudia, ya kwamba nimekifuata kile chama kinachokaza kuyashika mambo ya tambiko letu, kwani nalikuwa Fariseo.[#Tume. 23:6; Fil. 3:5-6.]

6Hata sasa ninasimama hapa, nihukumiwe, kwa sababu nangojea, kile kiagio kitimie, Mungu alichokiagana na baba zetu.[#Tume. 28:20.]

7Vile vile mashina yetu kumi na mawili hungojea, wakifikie; kwa hivyo wanajihimiza kumtumikia Mungu usiku na mchana. Hicho kingojeo ndicho, ninachosutiwa na Wayuda, mfalme Agripa.[#Tume. 24:15.]

8Kwa sababu gani huwaza kwenu, ya kuwa neno hilo halitegemeki la kwamba: Mungu anafufua wafu?

(9-20: Tume. 9:1-29; 22:3-21.)

9Kweli nami vyaliniingia moyoni kwamba: Sharti nifanye mdngi ya kulipinga Jina la Yesu wa Nasareti.

10Hayo niliyafanya huko Yerusalemu; nilipopewa ruhusa na watambikaji wakuu nikawatia watakatifu wengi kifungoni, tena walipouawa, nami nikasaidia.

11Hata katika nyumba zote za kuombea niliwaumiza mara kwa mara, nikiwashurutisha kumbeza Yesu, nikawaendea na ukorofi kama mwenye wazimu, nikawakimbiza mpaka kwenye miji iliyoko ugenini.

12Kwa hiyo nikaenda hata Damasko, nilipokwisha kupata maelekezo na maagizo kwa watambikaji wakuu.

13Ilipokuwa saa sita ya mchana, ndipo, mfalme, nilipoona hapo njiani mwanga uliotoka mbinguni wenye kumetuka kulishinda jua, ukatumulikia pande zote mimi na wenzangu waliokwenda pamoja nami.

14Tulipoanguka chini sote, nikasikia sauti iliyoniambia kwa msemo wa Kiebureo: Sauli, Sauli, unanifukuzaje? Utashindwa na kupiga mateke penye machomeo.

15Mimi nilipouliza: Ndiwe nani, Bwana? Bwana akasema: Mimi ni Yesu, ambaye unanifukuza wewe.

16Lakini inuka, usimame kwa miguu yako! Kwani hii ndiyo, niliyokutokea; Nikulinganye, utumike kuyashuhudia, uliyoyaona, nayo utakayoonyeshwa nami.[#Ez. 2:1,3.]

17Nitakuokoa kwao walio wa kwenu nako kwao wamizimu, maana ndiko, nitakakokutuma,

18uwafumbue macho yao na kuwaongoza, watoke gizani, waingie mwangani, tena watoke katika nguvu ya Satani, wamfikie Mungu; hivyo watapata kuondolewa makosa na kupewa fungu lao penye watakatifu, wakiwa wakinitegemea.[#Tume. 20:32.]

19Hapo, mfalme Agripa, sikukataa kuliitikia hilo jambo la mbinguni, nililoliona,[#Gal. 1:16.]

20ila niliwatumikia kwanza wa Damasko, tena wa Yerusalemu, tena wote walioko katika nchi ya Yudea, kisha hata wamizimu nao, nikiwaambia, wajute wakimgeukia Mungu na kutenda matendo yaliyo ya kujuta kweli.

21Kwa sababu hiyo Wayuda walinikamata, nilipokuwa hapo Patakatifu, wakajaribu kuniua.[#Tume. 21:30-31.]

22Lakini kwa hivyo, nilivyopata msaada kwa Mungu, ninasimama mpaka siku hii ya leo nikiwaeleza wakubwa na wadogo; sisemi mengine, yasipokuwa yale, waliyoyasema Wafumbuaji na Mose kwamba:[#Luk. 24:44-47.]

23Yatakayokuwapo ni haya: Kristo sharti ateswe, kisha atakuwa limbuko la ufufuko wa wafu, kisha atawaalika wao wa ukoo huu nao wamizimu, wafike mwangani.[#1 Kor. 15:20.]

24Alipojikania hivyo, Festo akapaza sauti akisema: Paulo, una wazimu! Ujuzi wako mwingi unakupapayusha.

25Paulo akasema: Bwana wangu Festo, sina wazimu, ila natoa maneno yenye kweli na yenye maana.

26Nawe mfalme, haya unayajua vema; kwa hiyo nasema mbele yako waziwazi. Kwani najua sana, ya kuwa hayo yote hakuna hata moja, usilolitambua, kwa sababu hayo hayakufanyika pembeni.[#Yoh. 18:20.]

27Mfalme Agripa, unawategemea Wafumbuaji? Nimekujua, ya kuwa unawategemea.

28Agripa akamwambia Paulo: Pamesalia padogo, ungenishinda, nikawa Mkristo.

29Ndipo, Paulo aliposema: Namwomba Mungu, paliposalia padogo napo paliposalia pakubwa, wote hapa walionisikia leo, si wewe tu, awape kuwa, kama mimi nilivyo, pasipo minyororo hii.

30Kisha mfalme na mtawala nchi na Berenike nao waliokaa pamoja nao wakainuka,

31wakajongea pembeni, wakasemezana wao kwa wao: Mtu huyu hakufanya neno linalopasa, auawe au afungwe.

32Agripa akamwambia Festo: Mtu huyu angeweza kufunguliwa, kama asingalikuwa ametaka kuhukumiwa na Kaisari.[#Tume. 25:11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania