Matendo ya Mitume 28

Matendo ya Mitume 28

Paulo aliyoyaona Melite.

1Tulipokwisha kuokoka, ndipo, tulipoambiwa, ya kuwa kisiwa kinaitwa Melite.

2Wenyeji wa huko wakatutunza kwa upendo usiopatikana kila siku: wakawasha moto, wakatupokea mwao sisi sote kwa ajili ya mvua iliyotunyea na kwa ajili ya baridi.[#2 Kor. 11:27.]

3Paulo alipodondoa mzigo wa vijiti kuvitia motoni, mkatoka humo nyoka kwa ajili ya moto, akamzingazinga mkono.

4Wenyeji walipomwona yule mdudu, alivyomng'ang'ania mkononi pake, wakasemezana wao kwa wao: Mtu huyu hakosi kuwa mwuaji, kwani ingawa ameokoka baharini, tena lipizi halimwachi, awepo.

5Alipomkung'uta yule mdudu motoni, hakuna kiovu tena kilichompata.[#Mar. 16:18.]

6Lakini wale walimtunduia na kungoja, avimbe au aanguke chini akifa papo hapo. Lakini walipongoja sana na kuona, ya kuwa hapati kibaya cho chote, wakageuka na kusema: Yeye ni mungu![#Tume. 14:11.]

7Lakini hapo karibu palikuwa na kiunga cha mkuu wa kisiwa, jina lake Pubulio. Huyu akatupokea mwake siku tatu, akatutunza na kutupendeza.

8Baba yake Pubulio alipoingiwa na homa na kuhara damu, Paulo akaingia mwake, akamwombea, akambandikia mikono, akamponya.

9Hayo yalipokwisha kufanyika, nao wengine wa kisiwa kile waliokuwa wenye magonjwa wakamjia, wakaponywa,

10wakatutukuza kwa matukuzo mengi. Nasi tulipoingia chomboni tena, wakatupakilia navyo vyote vya kutumia njiani.

Kufika Roma.

11Miezi mitatu ilipopita, tukaondoka tukijipakia chomboni kilichotoka Alekisandria; kilikuwa kimezimaliza siku za kipupwe pale kisiwani; kilikuwa chenye chapa cha mapacha.

12Tulipofika Sirakuse, tukakaa huko siku tatu.

13Kutoka huko tukazunguka, tukafika Regio. Tulipongoja siku moja, kukavuma upepo wa kusini, tukafika Puteoli kwa mwendo wa siku mbili.

14Huko tukakuta ndugu, tukabembelezwa nao, tukae kwao siku saba. Ndivyo, tulivyokwenda kufika Roma.

15Ndugu wa huko walipovisikia wakaja kukutana na sisi, wakatujia mpaka Apioforo, wengine mpaka Tiretaberne. Paulo alipowaona akamshukuru Mungu, akachangamka.

16Tulipoingia Roma, bwana askari akampa mwenzake mkubwa wafungwa, lakini Paulo akapewa ruhusa ya kukaa, alipotaka, pamoja na askari aliyemlinda.[#Tume. 27:3.]

Paulo na Wayuda wa Roma.

17Siku tatu zilipopita, akawakusanya wakubwa wa Wayuda. Walipokusanyika, akawaambia: Waume ndugu, mimi sikuwakosea wao wa ukoo wetu wala mazoea ya baba zetu. Nimefungwa huko Yerusalemu, nikatiwa mikononi mwa Waroma.[#Tume. 23:1.]

18Nao waliponiulizauliza wakataka kunifungua, kwa sababu kwangu hakuna neno linalopasa, niuawe.

19Lakini Wayuda walipobisha, nikashurutishwa kutaka kuhukumiwa na Kaisari, lakini hapo siko kwamba: Niwasute walio wa taifa langu.[#Tume. 25:10-11.]

20Kwa sababu hii nimewaita, niwaone ninyi, tusemeane. Kwani kingojeo cha Waisiraeli ndicho, nilichofungiwa mnyororo huu.[#Tume. 26:6-7.]

21Nao wakamwambia: Sisi kwa ajili yako hatukupata barua toka Yudea, wala hakuna ndugu aliyetujia na kutusimulia mambo yako, wala kusema kibaya, ulichokifanya.

22Lakini twataka kusikia kwako mwenyewe mawazo yako, kwani chama hiki tumekijua, nako kwetu kinatambulika, ya kuwa kinabishiwa po pote.[#Tume. 24:14; Luk. 2:34.]

23Walipokwisha kuagana naye siku, wengi wakamjia huko, alikofikia, akawaeleza tangu asubuhi mpaka jioni akiushuhudia ufalme wa Mungu; tena akajaribu kuwashinda kwa ajili yake Yesu na kuwafumbulia maonyo ya Mose na maneno ya wafumbuaji wengine wakayaitikia maneno yake, wengine wakakataa kuyategemea.

24Wengine wakayaitikia maneno yake, wengine wakakataa kuyategemea.

25Hivyo wakashindwa kupatana wao kwa wao, wakajiendea zao. Ndipo, Paulo aliposema neno kwa kinywa cha mfumbuaji Yesaya:

26Nenda kwao wa ukoo huu, useme:

Kusikia mtasikia, lakini hamtajua maana;

Kutazama mtatazama, lakini hamtaona.

27Kwani mioyo yao walio ukoo huu imeshupazwa,

wasisikie kwa masikio yao yaliyo mazito,

nayo macho yao wameyasinziza,

wasije wakaona kwa macho yao,

au wakasikia kwa masikio yao,

au wakajua maana kwa mioyo yao,

wakanigeukia, nikawaponya.

28Basi, ijulikane kwenu ninyi ya kwamba: Wokovu huu wa Mungu umepelekwa kwenye wamizimu; hao ndio watakaousikia.[#Tume. 13:46.]

29Alipovisema hivyo, Wayuda walikwenda wakibishana sana wao kwa wao.

30Paulo akakaa miaka miwili mzima katika nyumba yake, aliyokuwa ameipanga, akawapokea wote walioingia kwake,

31akautangaza ufalme wa Mungu, akayafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo pasipo woga na pasipo kuzuiliwa na mtu.[#Tume. 28:23.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania