Amosi 1

Amosi 1

Yatakayowapata majirani zao Waisiraeli.

1Maneno ya Amosi aliyekuwa mchunga ng'ombe na kondoo kwao Tekoa; ni mambo yatakayowapata Waisiraeli, naye aliyaona katika siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na za Yoroboamu, mwana wa Yoasi, mfalme wa Isiraeli; ilikuwa miaka miwili kabla ya ule mtetemeko wa nchi[#Amo. 7:14; 2 Fal. 14:23; 15:1; Zak. 14:5.]

2Alisema:

Bwana atanguruma mle Sioni,

ataivumisha sauti yake mle Yerusalemu;

ndipo, mbuga za wachungaji zitakaposikitika,

nao mlima wa Karmeli utakauka juu yake.

3Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Kwa ajili ya mapotovu ya Damasko matatu au manne

sitayarudisha, yasiwapate,

kwa kuwa waliupura Gileadi kwa magari ya chuma ya

kupuria.

4Nitatupa moto nyumbani mwa Hazaeli, uyale majumba ya Benihadadi,

5nitalivunja komeo la Damasko,

nitawang'oa wakaao katika Bonde la Maovu,

nitamng'oa naye mshika bakora ya kifalme mle Beti-Edeni;

nao watu wa Ushami watatekwa na kuhamishwa kwenda Kiri.

Bwana ameyasema.

6Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Kwa ajili ya mapotovu ya Gaza matatu au manne

sitayarudisha, yasiwapate,

kwa kuwa waliwateka wote pia na kuwahamisha,

wawapeleke utumwani kwa Waedomu.

7Nitatupa moto bomani mwa Gaza, uyale majumba yao,

8nitawang'oa wakaao mle Asdodi,

naye mshika bakora ya kifalme mle Askaloni;

kisha nitaugeuza mkono wangu, uujie Ekroni,

ndipo, Wafilisti waliosalia watakapoangamia.

Bwana Mungu ameyasema.

9Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Kwa ajili ya mapotovu ya Tiro matatu au manne

sitayarudisha, yasiwapate,

kwa kuwa wote pia, waliowateka, waliwahamisha

na kuwapeleka kwa Waedomu,

hawakulikumbuka agano la Kindugu.

10Nitatupa moto bomani mwa Tiro, uyale majumba yao.

11Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Kwa ajili ya mapotovu ya Edomu matatu au manne

sitayarudisha, yasiwapate,

kwa kuwa waliwakimbiza ndugu zao kwa panga,

wakajizuia, wasiwahurumie,

kwa kuwa waliendelea siku zote kuwanyafua kwa ukali,

hawakomi kuwachafukia kale na kale.

12Nitatupa moto mle Temani, uyale majumba ya Bosira.

13Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Kwa ajili ya mapotovu ya wana wa Amoni matatu au manne

sitayarudisha, yasiwapate

kwa kuwa waliwatumbua wenye mimba wa Gileadi,

wapate kuipanua mipaka yao.

14Lakini nitawasha moto bomani mwa Raba, uyale majumba

yao,

wapige makelele, kwa kuwa ni siku ya vita,

pawe uvumi, kwa kuwa ni siku ya chamchela.

15Naye mfalme wao atakwenda kuhamishwa, kwa kuwa atatekwa yeye na wakuu wake.

Bwana ameyasema.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania