Wakolose 1

Wakolose 1

Anwani.

1Mimi Paulo niliye mtume wa Kristo Yesu kwa hayo, Mungu ayatakayo, na ndugu Timoteo[#Rom. 1:7.]

2tunawaandikia ninyi mlioko Kolose, ndugu watakatifu mnaomtegemea Kristo: Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba yetu!

Kazi ya utume.

3Twamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tunapowaombea ninyi.

4Kwani tumesikia, mnavyomtegemea Kristo Yesu, tena mnavyowapenda watakatifu wote.[#Ef. 1:15.]

5Maana mwakishika kingojeo cha yale, mliyowekewa mbinguni; hayo mmeyasikia kale, mlipotangaziwa Utume mwema wa neno la kweli.[#1 Petr. 1:3-4.]

6Nao Utume ulifika kwenu, kama ulivyofika po pote ulimwenguni: huzaa matunda, tena hukua. Vivyo hivyo uko hata kati yenu tangu siku ile, mlipousikia na kuutambua upole wa Mungu kwamba: Ndio wenye kweli.

7Ndivyo, mlivyofundishwa na Epafura; ni mtumwa mwenzetu mpendwa, tena ni mtumishi mwelekevu wa Kristo anayewafanyizia ninyi kazi.[#Kol. 4:12.]

8Naye ndiye aliyetueleza, mnavyopendana Rohoni.

Kazi ya Kristo.

9*Kwa hiyo hata sisi tangu siku ile, tulipoyasikia mambo hayo, hatuachi kumwangukia Mungu na kuwaombea ninyi, mpate kuyatambua yote, ayatakayo, kisha mpewe werevu wote ulio wa kweli na ujuzi wote wa Kiroho.[#Ef. 1:16-17.]

10Hivyo mtaweza kuendelea na kumpatia Bwana macheo, apendezwe nanyi kabisa; kisha mtazaa matunda mkizifanya kazi njema zote kwa kuendelea kumtambua Mungu.[#Ef. 4:1; Fil. 1:27.]

11Tena tunawaombea, mtiwe nguvu zo zote kwa hivyo, utukufu wake ulivyo wenye nguvu, mpate kuyavumilia na kuyanyenyekea yote.[#1 Kor. 1:5.]

12Mpate hata kumshukuru Baba kwa furaha, maana amewatengeneza ninyi, mgawiwe fungu la urithi wa watakatifu uliomo mwangani.[#Ef. 1:11.]

13Yeye ndiye aliyetuokoa katika nguvu ya giza, akatukalisha kwenye ufalme wa mwana wake mpendwa.[#Kol. 2:15.]

14Mwake yeye ndimo, tupatiamo ukombozi kwa kuondolewa makosa.*[#Ef. 1:7.]

15Yeye anafanana na Mungu asiyeonekana; ndiye aliyevitangulia viumbe vyote kuzaliwa.[#Ebr. 1:3.]

16Tena ndiye, ambaye vyote viliumbwa mwake yeye, vilivyoko mbinguni navyo vilivyopo nchini, vinavyoonekana navyo visivyoonekana, vikiwa viti vya kifalme au maboma au makao ya wakuu au pengine penye nguvu: vyote pia viliumbwa naye, tena humwelekea.[#Yoh. 1:3,10.]

17Naye mwenyewe alikuwapo, vitu vyote vilipokuwa havijakuwapo bado, navyo vyote hushikwa naye.[#Fano. 8:25-27; Rom. 11:36.]

18Naye mwenyewe ni kichwa cha mwili, maana cha wateule. Naye ni wa kwanza, ni limbuko la wafu, kusudi yeye awe wa kwanza katika mambo yote.[#Tume. 26:23; 1 Kor. 15:20; Ef. 1:22; Ufu. 1:5.]

19Kwani ilimpendeza Mungu, yote pia yamkalie yeye,[#Kol. 2:9; Yoh. 1:16.]

20tena yote yapatanishwe naye, yarudi kwake yeye, kwani hapo, damu yake ilipomwagwa msalabani, ameyapatia utengemano yale yote yaliyopo nchini nayo yaliyopo nchini nayo yaliyoko mbinguni.[#Ef. 1:10; 1 Yoh. 2:2.]

Utukufu wa Utume.

21Hata ninyi kale mlikuwa wageni naye, mkawa hata wachukivu wake, maana mioyoni mlifuata matendo mabaya.[#Rom. 5:10; Ef. 2:12-13; 4:18.]

22Lakini sasa amewapatanisha hata ninyi hapo, alipokufa na kuutoa mwili wake wa kimtu, awageuze nanyi kuwa machoni pake watakatifu pasipo kilema wala kosa.[#Ef. 5:27.]

23Mtakuwa hivyo mkifuliza kumtegemea, kwani mmajengwa juu ya msingi wenye nguvu, msiwezekane kuondolewa penye kingojeo cha Utume mwema, mliousikia; ndio unaotangaziwa kila kiumbe kilichoko chini ya mbingu. Nami Paulo ninautumikia.

24Sasa nafurahiwa nayo mateso, niliyoyapata kwa ajili yenu. Nayo maumivu, Kristo aliyoyasaza, nayatimiliza katika mwili wangu, unapoteswa kwa ajili ya mwili wake, maana wateule wake.[#Ef. 3:13; 2 Tim. 2:10.]

25Ndio wao, niwatumikiao nikiufuata utunzaji wa Mungu, niliopewa, niwatimilizie ninyi Neno lake Mungu.

26Ni lile fumbo lililokuwa limefichwa tangu kale, baba wasilijue. Lakini sasa watakatifu wake wamekwisha kufumbuliwa;[#Rom. 16:25-26; Ef. 1:9-10; 3:4-9; 1 Tim. 3:16.]

27kwani ndio, Mungu aliotaka kuwatambulisha, limbuko likuavyo, lile la utukufu wa fumbo hili, awalimbikialo wamizimu, ndilo hili: Kristo yumo mwenu, yeye ndio utukufu unaongojewa.[#1 Tim. 1:1.]

28Naye ndiye, tunayemtangaza sisi, tukimwonya kila mtu na kumfundisha kila mtu werevu wote ulio wa kweli, tupate kumgeuza kila mtu kuwa mtimilifu kwa nguvu ya Kristo.[#Kol. 1:22.]

29Kazi hii ndiyo, niisumbukiayo na kuishindania kwa uwezo wake yeye anayeniwezesha hivyo kwa nguvu yake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania