The chat will start when you send the first message.
1*Basi, kama mmefufuka pamoja naye Kristo, yatafuteni yaliyoko juu! Ndiko, Kristo akaako kuumeni kwa Mungu.[#Kol. 2:12.]
2Yawazeni yaliyoko juu, msiyawaze yaliyopo nchini![#Mat. 6:33.]
3Kwani mmekufa, lakini uzima wenu uko umefichwa pamoja na Kristo kwake Mungu.[#Rom. 6:2.]
4Hapo Kristo aliye uzima wenu atakapofunuliwa, ndipo, nanyi mtakapofunuliwa pamoja naye kuwa wenye utukufu.*[#1 Kor. 15:43.]
5Basi, viueni viungo viyatimizavyo yaliyopo nchini: ugoni na uchafu na tamaa na kijicho kiovu na choyo kilicho sawa na kutambikia vinyago![#Rom. 6:6; 8:13.]
6Kwa ajili ya mambo hayo makali ya Mungu hutokea.[#Ef. 5:6.]
7Nanyi mambo hayo mliandamana nayo hapo kale, mlipokuwa mkiyakalia.
8Lakini sasa nanyi hayo yote sharti myatoke: makali na mifundo ya mioyo na maovu na matusi na mateto mabaya yaliyomo vinywani mwenu.[#Ef. 4:29,31.]
9Msiambiane yaliyo ya uwongo! Mvueni mtu wenu wa kale pamoja na matendo yake![#Ef. 4:22,25.]
10Mvaeni yule mtu mpya apataye upya kwamba: Katika utambuzi afanane naye aliyemwumba![#1 Mose 1:27; Ef. 4:24.]
11Hapo hapana tena Mgriki na Myuda, wala aliyetahiriwa na mwingine asiyetahiriwa, wala mgeni na mshenzi, wala mtumwa na mwungwana. Ila Kristo ndiye yote, naye yumo mwao wote.[#Gal. 3:28.]
12*Ninyi watakatifu na wapendwa, kwa hivyo, mlivyochaguliwa na Mungu, vaeni mioyo yenye huruma za kweli na utu na unyenyekevu na upole na uvumilivu![#1 Petr. 2:9.]
13Mvumiliane ninyi kwa ninyi na kuachiliana, mtu akiwa na neno la kumkamia mwenziwe! Kama naye Bwana alivyowaachilia ninyi, vivyo hivyo vifanyeni nanyi![#Mat. 6:14; Ef. 4:24.]
14Lakini lililo kuu kuliko haya yote: uvaeni upendano! Maana ndio unaoyatimiza yote na kutupatanisha kuwa mmoja.[#Rom. 13:8,10.]
15Nao utengemano wa Kristo utawale mioyoni mwenu! Kwani ndio, mlioitiwa, maana m mwili mmoja. Tena mema, mliyogawiwa, myavumishe![#1 Kor. 12:13,27; Fil. 4:7.]
16Neno la Kristo likae mwenu, kama ni mali, mzikaliazo, mkifundishana pamoja na kuonyana na kujulishana ujuzi wote, mmwimbie Mungu mioyoni mwenu shangwe na nyimbo na tenzi za Kiroho za kwamba: Tumegawiwa mema![#Ef. 5:19.]
17Nayo yote, mtakayoyatenda, ikiwa maneno ya kusema au kazi za kufanya, yafanyeni yote katika Jina la Bwana Yesu mkimvumisha Mungu Baba kwa kufanya hivyo!*[#1 Kor. 10:31.]
18Ninyi wake, watiini waume wenu, kama inavyowapasa walio wa Bwana!
19Ninyi waume, wapendeni wake zenu, msiwaendee kwa ukali![#1 Petr. 3:7.]
20Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote! Kwani hivi vinampendea Bwana.
21Ninyi baba, msiwachokoze watoto wenu, wasishindwe na kutii!
22Ninyi watumwa, katika mambo yote watiini walio mabwana zenu kimtu! Msiwatumikie hapo machoni tu, kama wenye kupendeza watu, ila kama wenye kumwogopa Bwana watumikieni kwa mioyo iliyo na neno moja tu!
23Katika yote, mnayoyatenda, zifanyeni kazi zenu kwa mioyo, kama ni kazi zinazofanyiziwa Bwana, zisizofanyiziwa watu!
24Jueni, ya kuwa mtapokea kwake Bwana malipo hapo, mtakapoupata urithi wenu! Mtumikieni Bwana Kristo!
25Lakini mpotovu atayatwaa mapato yao yale, aliyoyapotoa, lakini hakuna upendeleo.[#Rom. 2:11.]