5 Mose 1

5 Mose 1

Waisiraeli hawakuyashukuru matendo mema ya Mungu.

1Haya ndiyo maneno, Mose aliyowaambia Waisiraeli wote ng'ambo ya huku ya Yordani nyikani kwenye mbuga zinazoielekea Bahari Nyekundu katikati ya Parani na Tofeli na Labani na Haseroti na Di-Dhahabu.

2Kutoka Horebu ulikuwa mwendo wa siku kumi na moja kwa kushika njia ya kwenda mlimani kwa Seiri mpaka Kadesi-Barnea.

3Ikawa siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na moja katika mwaka wa arobaini, ndipo, Mose alipowaambia wana wa Isiraeli hayo yote, kama Bwana alivyomwagiza kuwaambia.

4Ilikuwa hapo, alipokwisha kumpiga Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekaa Hesiboni, na Ogi, mfalme wa Basani, aliyekaa Astaroti karibu ya Edirei.[#4 Mose 21:21-35.]

5Naye alikuwa ng'ambo ya huku ya Yordani katika nchi ya Moabu; ndiko, Mose alikoanza kuwaelezea mafunzo haya ya Maonyo, akasema:

6Bwana Mungu wetu alituambia kule Horebu kwamba: Siku za kukaa kwenu kwenye mlima huu zimetimia.[#4 Mose 10:11-12.]

7Kwa hiyo ondokeni huku na kujielekeza kwenda milimani kwa Waamori nako kwao wote wanaokaa karibu yao nyikani na milimani na mabondeni na kusini na pwani kwenye bahari, mfike katika nchi ya Kanaani hata Libanoni mpaka ule mto mkubwa, lile jito la Furati.

8Tazameni, nchi hii iliyoko mbele yenu nitawapa, iingieni, mwichukue nchi hii, Bwana aliyowaapia baba zenu Aburahamu na Isaka na Yakobo kuwapa wao nao wa uzao wao watakaokuwapo nyuma yao.

9Hapo ndipo, nilipowaambia ninyi: Mimi peke yangu siwezi kuwatunza ninyi.[#2 Mose 18:18; 4 Mose 11:14.]

10Bwana Mungu wenu amewafanya kuwa wengi sana; nikiwatazam leo, mnafanana na nyota za mbinguni kwa wingi.[#1 Mose 15:5; 5 Mose 10:22.]

11Bwana Mungu wa baba zenu na aendelee kuwafanya kuwa wengi zaidi, wao walioko sasa waongezeke mara elfu, kisha na awabariki, kama alivyowaambia ninyi.

12Mimi nitawezaje peke yangu kuuchukua huo mzigo wenu mzito sana wa magomvi yenu?

13Kwa hiyo toeni kwenu watu werevu wa kweli walio watambuzi wanaojulikana katika mashina yenu, niwaweke kuwa vichwa vyenu.

14Nanyi mkanijibu kwamba: Neno hili, ulilolisema, linafaa kulifanya.

15Kisha nikiwachukua waliokuwa vichwa vya mashina yenu na watu waliojulikana kuwa wenye werevu wa kweli, nikawaweka kuwa vichwa vyenu, wawe wakuu wa maelfu na wakuu wa mamia na wakuu wa hamsini na wakuu wa makumi, tena wawe wenye amri wa mashina yenu.

16Nao waamuzi wenu nikawaagiza siku hizo kwamba: Wasikilizeni ndugu zenu, mwamue kwa kweli, mtu akiwa na shauri la ndugu yake au la mgeni wake![#3 Mose 19:15.]

17Shaurini msiupendelee uso wa mtu, kama shauri lake ni dogo, au kama ni kubwa, wote mwasikilize pasipo kumwogopa ye yote, kwani hukumu ni yake Mungu. Lakini shauri likiwa gumu zaidi la kuwashinda ninyi, na mlilete kwangu, nilisikilize.[#5 Mose 16:19; 2 Mose 21:6.]

18Ndivyo, nilivyowaagiza siku zile mambo yote yaliyowapasa kuyafanya.

19Tulipoondoka Horebu tukasafiri katika ile nyika yote inayotisha kwa ukubwa wake, kama mlivyoona; tukaishika njia ya kwenda milimani kwa Waamori, kama Bwana Mungu wetu alivyotuagiza, tukafika mpaka Kadesi-Barnea.[#4 Mose 20:1.]

20Ndipo, nilipowaambia: Mmefika milimani kwa Waamori, ndiyo nchi, Bwana Mungu wetu anayotaka kutupa sisi.

21Tazameni, Bwana Mungu wetu ameiweka nchi hii machoni penu. Pandeni tu kuichukua, iwe yenu, kama Bwana Mungu wa baba zenu alivyosema! Msiogope, wala msiingiwe na vituko![#5 Mose 9:23.]

22Ndipo, ninyi nyote mlipokuja kwangu, mkaniambia: Na tutume watu kwenda mbele yetu, watupelelezee nchi hii, kisha watuletee habari za njia, tutakazozishika za kupandia huko, na habari za miji, tutakayoiingia.[#4 Mose 13:2.]

23Kwa kuwa neno hili lilikuwa jema machoni pangu, nikachagua kwenu watu kumi na wawili, kwa kila shina mtu mmoja.

24Wao wakajielekeza kupanda milimani, wakafika mpaka kijitoni kwa Eskoli wakiipeleleza nchi.

25Wakachukua kwa mikono yao matunda mengineyo ya nchi hiyo, wakashuka nayo kutuletea sisi, wakatuletea nazo habari za kwamba: Nchi hii, Bwana Mungu wetu anayotaka kutupa, ni nzuri.

26Lakini hamkutaka kupanda, mkalikataa agizo la Bwana Mungu wenu,[#4 Mose 14.]

27mkanung'unika mahemani mwenu kwamba: Kwa kutuchukia Bwana alitutoa katika nchi ya Misri, atutie mikononi mwao Waamori, watuangamize.

28Sisi tupande kwenda wapi? ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu waliposema: Watu ni wengi na warefu kuliko sisi, nayo miji ni mikubwa yenye maboma yanayofika hata mbinguni; hata wana wa Anaki tumewaona huko.[#5 Mose 9:1-2.]

29Ndipo, nilipowaambia ninyi: Msitetemeke, wala msiwaogope!

30Bwana Mungu wenu anayewatangulia, yeye atawapigia vita, matendo yake yawe kama yale yote, aliyowafanyizia kule Misri, mliyoyaona kwa macho yenu.[#2 Mose 14:14,25; Yos. 10:14.]

31Nako nyikani mmeona, Bwana Mungu wenu alivyowachukua, kama mtu anavyomchukua mwanawe, katika hizo safari zote, mlizokwenda, mpaka mkifika mahali hapa.[#2 Mose 19:4; 5 Mose 8:5.]

32Lakini ijapo ameyafanya hayo yote, ninyi hamkuwa mkimtegemea Bwana Mungu wenu.

33Naye alikuwa amewatangulia njiani, awatafutie mahali pa kupigia makambi yenu; aliwatangulia usiku kwa moto, awaangazie hizo njia, mlizokwenda, tena mchana kwa wingu.[#2 Mose 13:21.]

34Hapo, Bwana alipoyasikia yale maneno, mliyoyasema, akachafuka, akaapa kwamba:

35Watu hawa wote wa hiki kizazi kibaya hawataiona kabisa hiyo nchi njema, niliyowaapia baba zao kuwapa,

36Kalebu, mwana wa Yefune, yeye tu ataiingia, nami nitampa nchi hiyo, aliyoikanyaga, iwe yake yeye na ya wanawe, kwa kuwa alimfuata Bwana kwa moyo wote.

37Mimi nami Bwana akanikasirikia kwa ajili yenu, akaniambia: Wewe nawe hutaiingia hiyo nchi.[#4 Mose 20:12.]

38Lakini Yosua, mwana wa Nuni, anayekutumikia, yeye ataingia huko; mshikize moyo, kwani ndiye atakayewagawia Waisiraeli mafungu ya nchi yatakayokuwa yao.[#4 Mose 34:17.]

39Nao watoto wenu, mliowasema, ya kama watakuwa mateka, nao wana wenu wasiojua leo bado kupambanua mema na mabaya, wao ndio watakaoingia huko, nao nitawapa hiyo nchi, waichukue, iwe yao.

40Lakini ninyi geukeni na kuondoka hapa, mrudi nyikani na kushika njia ya kwenda kwenye Bahari Nyekundu.

41Ndipo, mlipojibu na kuniambia: Tumemkosea Bwana. Sisi na tupande, tupige vita na kuyafanya yote, Bwana Mungu wetu aliyotuagiza. Lakini hapo mlipojifunga mata yenu ya kupigia vita kwa kuwaza, ya kama ni kazi nyepesi kupanda huko milimani,

42Bwana akaniambia: Waambie: Msipande, wala msipige vita! Kwani mimi simo katikati yenu, msije kupigwa mbele ya adui zenu.

43Nilipowaambia hayo, hamkusikia, mkalikataa neno, kinywa cha Bwana kililolisema; mkapanda milimani kwa kujivuna.

44Kwa hiyo Waamori waliokaa kule milimani walipotoka kupigana nanyi, wakawafukuza, kama nyuki wanavyofanya, wakawapiga ninyi huko Seiri, mfike mpaka Horma.

45Mkarudi na kumlilia Bwana, lakini Bwana hakuzisikia sauti zenu, wala hakuwategea ninyi sikio.

46Kwa hiyo mkakaa Kadesi hizo siku nyingi, mlizozikaa huko.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania