The chat will start when you send the first message.
1Kwa hiyo umpende Bwana Mungu wako na kuyaangalia mambo yake yanayopasa, uyaangalie siku zote, maongozi yake na maamuzi yake na maagizo yake!
2Ndipo, mtakapomtambua na leo; kwani sisemi na wana wenu, maana hawayajui, wala hawakuyaona mapatilizo ya Bwana Mungu wenu na matendo yake makuu na nguvu za kiganja chake na uwezo wa mkono wake, alipoukunjua.
3na vielekezo vyake na matendo yake yote, aliyomfanyizia Farao, mfalme wa Misri, nao wenyeji wa nchi yake kule kwao Misri,
4nayo aliyovifanyia vikosi vya Farao na farasi wake na magari yake, aliowafurikishia maji ya Bahari Nyekundu ya kuwatosa, walipokimbia, wawafikilie ninyi, Bwana akawaangamiza, wasionekane tena hata leo.[#2 Mose 14:25,27.]
5Hawakuyaona nayo, aliyowafanyia ninyi nyikani, mpaka mfike mahali hapa,
6nayo aliyowafanyia Datani na Abiramu, wana wa Eliabu, mwana wa Rubeni, nchi ilipowaasamia na kuwameza wao na nyumba zao na mahema yao pamoja nao wote waliosimama upande wao kwa miguu yao katikati yao Waisiraeli wote.[#4 Mose 16:31-35.]
7Ila ninasema nanyi, kwani macho yenu ndiyo yaliyoyaona hayo matendo makuu yote, Bwana aliyoyafanya.
8Kwa hiyo yaangalieni maagizo yote, mimi ninayowaagiza leo, mpate nguvu za kuiingia hiyo nchi na kuichukua, iwe yenu, maana mnaivukia kuichukua, iwe yenu,
9nanyi siku zenu zipate kuwa nyingi katika nchi hiyo, Bwana aliyowaapia baba zenu kuwapa wao nao wa uzao wao, hiyo nchi ichuruzikayo maziwa na asali.
10Kwani hiyo nchi, utakayoiingia kuichukua, iwe yako, haifanani na nchi ya Misri, mlikokaa: ulipopanda mbegu huko hukuwa na budi kuzinywesha kwa kazi za miguu yako, zipate kuwa shamba la mboga.
11Lakini hiyo nchi, mtakayovukia kuichukua, iwe yenu, ni nchi yenye milima na mabonde, nayo hunyweshwa maji ya mvua za mbinguni.
12Nayo ni nchi, Bwana Mungu wako anayoipatia yaipasayo, nayo macho yake Bwana Mungu wako hayakomi kuitazama tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wa mwaka.[#Sh. 65:10-11.]
13Itakuwa, mtakapoyasikia vema maagizo yangu, mimi ninayowaagiza leo, mmpende Bwana Mungu wenu na kumtumikia kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote:[#3 Mose 26:3-39.]
14nitatoa mvua za nchi yenu, siku zake zitakapotimia, mvua ya vuli na ya masika, upate kuzivuna ngano zako na mvinyo zako na mafuta yako.
15Nao nyama wako wa kufuga nitawapa majani maporini, upate kula na kushiba.
16Jiangalieni tu, mioyo yenu isidanganyike, mmwache Bwana, mkaenda kutumikia miungu mingine na kuitambikia.
17Mtakapofanya hivyo, makali ya Bwana yatawawakia ninyi, azifunge mbingu, mvua isinye, nchi isitoe mazao yake; ndipo, mtakapoangamia upesi, mtoweke katika hiyo nchi njema, Bwana atakayowapa.[#3 Mose 26:19; 5 Mose 28:23.]
18Kwa hiyo haya maneno yangu yawekeni mioyoni na rohoni mwenu! Tena yafungeni mikononi penu kuwa kielekezo, yawe napo mapajini penu katikati ya macho yenu![#5 Mose 6:6-9.]
19Yafundisheni watoto wenu na kuyasema nao ukikaa nyumbani mwako, ukienda safari zako, ukitaka kulala, hata ukiamka!
20Yaandike vizingitini namo milangoni nyumbani mwako!
21Ndipo, siku zenu nazo siku za wana wenu zitakapokuwa nyingi katika hiyo nchi, Bwana Mungu wenu aliyowaapia baba zenu kuwapa, iwe yao siku zote, mbingu zitakazokuwa juu ya nchi.
22Kwani mtakapoyaangalia vema haya maagizo yote, mimi ninayowaagiza ninyi, myafanye na kumpeda Bwana Mungu wenu na kuzishika njia zake na kugandamana naye,
23ndipo, Bwana atakapoyafukuza hayo mataifa yote mbele yenu, mchukue nchi za mataifa walio wengi na wenye nguvu kuliko ninyi.[#5 Mose 7:1-2.]
24Ndipo, mahali po pote, nyayo za miguu yenu zitakapopakanyaga, patakapokuwa penu, mpaka wenu utoke nyikani na Libanoni nako kwenye lile jito kubwa la Furati, ufike kwenye bahari ya machweoni kwa jua.
25Hatakuwako mtu atakayeweza kusimama mbele yenu, kwani Bwana Mungu wenu atawastusha, wawaogope ninyi katika nchi zote, mtakazozikanyaga, kama alivyowaambia ninyi.
26Tazameni, leo hivi mimi ninaweka mbele yenu mbaraka na kiapizo:[#5 Mose 30:1,15.]
27mbaraka mtaipata mtakapoyasikia maagizo ya Bwana Mungu wenu, mimi ninayowaagiza leo.[#5 Mose 28:2,15.]
28Lakini kiapizo kitawapata, msipoyasikia maagizo ya Bwana Mungu wenu, mwondoke katika njia hiyo, mimi ninayowaagiza leo, mkafuata miungu mingine, msiyoijua.
29Hapo, Bwana Mungu wako atakapokuingiza katika nchi hiyo, wewe utakayoiingia kuichukua, iwe yako, ndipo utoe mbaraka juu ya mlima wa Gerizimu, nacho kiapizo juu ya mlima wa Ebali[#5 Mose 27:12-13; Yos. 8:33-34.]
30Milima hii iko ng'ambo ya huko ya Yordani nyuma ya njia inayokwenda machweoni kwa jua katika nchi ya Wakanaani wanaokaa katika nyika inayoelekea Gilgali, ni huko kando ya kimwitu cha More.[#1 Mose 12:6.]
31Kwani ninyi mtauvukia Yordani kuichukua hiyo nchi, iwe yenu, Bwana Mungu wenu atakayowapa, nanyi mtaichukua, iwe yenu kweli, kisha mtaikaa.
32Kwa hiyo angalieni, myafanye haya maongozi na maamuzi yote, mimi ninayoyaweka leo mbele yenu.