5 Mose 12

5 Mose 12

Agizo la kuyakomesha matambiko yote ya kimizimu.

1Haya ndiyo maongozi na maamuzi, mtakayoyaangalia, myafanye katika hiyo nchi, Bwana Mungu wa baba zako atakayokupa, uichukue, iwe yako siku zote, mtakazoishi huku nchini.

2Sharti mpaangamize kabisa mahali pote, wamizimu mtakaowafukuza walipoitumikia miungu yao juu ya milima mirefu nako vilima, tena chini ya miti yenye majani mengi.[#5 Mose 7:5,25.]

3Sharti mpabomoe pao pa kutambikia, nazo nguzo zao za mawe za kutambikia mzivunje, nayo miti yao ya Ashera mwiteketeze, navyo vinyago vya miungu yao vya kuchongwa mvikatekate, myatoweshe majina yao mahali pale palipokuwa pao.

Matambiko ya Kimungu.

4Bwana Mungu wenu msimfanyizie hivyo,

5ila mahali pale pamoja, Bwana Mungu wenu atakapopachagua katika mashina yote pa kuliwekea Jina lake, likae papo hapo, ndipo papasapo, mpaingie mtakapomtafuta.

6Tena ndipo papasapo, mpapeleke ng'ombe zenu za tambiko za kuteketezwa nzima na ng'ombe zenu nyingine za tambiko na mafungu yenu ya kumi na vipaji vya mikono yenu vya tambiko vya kunyanyuliwa na matoleo ya kuyalipa mliyoyaapa na matoleo yenu, mtakayoyatoa kwa kupenda wenyewe, na wana wenu wa kwanza wa ng'ombe na wa mbuzi na wa kondoo.

7Napo ndipo papasapo, mle mbele ya Bwana Mungu wenu mtakapomtambikia kwa kuyafurahia yote, iliyoyachukua mikono yenu ninyi nayo yao waliomo nyumbani mwenu, kwa kuwa Bwana Mungu wako alikubariki.

8Msiyafanye haya yote, tunayoyafanya sisi leo huku, kila mtu akiyafanya yanyokayo machoni pake yeye.

9Kwani hamjaingia bado kwenye kituo wala katika nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe yako.

10Lakini mtauvuka Yordani, mpate kukaa katika nchi hiyo, Bwana Mungu wenu atakayowapa, iwe fungu lenu; ndiko, atakakowapatia kupumzika kwa kuwashinda adui zenu wote pande zote, mkae na kutulia.[#1 Fal. 4:25.]

11Kisha mahali pale, Bwana Mungu wenu atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, sharti mpeleke hapo yote, mimi ninayowaagiza leo: ng'ombe zenu za tambiko za uteketezwa nzima na ng'ombe zenu nyingine za tambiko na mafungu yenu ya kumi na vipaji vya mikono yenu vya tambiko vya kunyanyuliwa, nayo yote ya kuyalipa, mliyoyaapa kumtolea Bwana kwa kupenda wenyewe.

12Tena ndipo, mtakapomfurahia Bwana Mungu wenu, ninyi na wana wenu wa kiume na wa kike na watumishi wenu wa kiume na wa kike, nao Walawi watakaokaa milangoni kwenu, kwani wao hawatapata fungu la nchi litakalokuwa lao.[#4 Mose 18:20,24.]

13Jiangalie, usitoe ng'ombe zako za tambiko za kuteketezwa nzima mahali po pote, utakapopaona!

14Ila mahali pale pamoja tu, Bwana atakapopachagua katika moja lao mashina yako, ndipo papasapo, utolee hapo ng'ombe zako za tambiko za kuteketezwa nzima, tena ndipo papasapo, uyafanye yote, mimi ninayokuagiza.

15Lakini roho yako ikiwa na uchu wa nyama tu, utazichinja na kuzila malangoni pako po pote kwa mbaraka ya Bwana Mungu wako aliyekupa hizo nyama; mwenye uchafu na mwenye kutakata atazila, kama ni za paa au kama ni za kulungu.[#5 Mose 12:22; 14:5.]

16Damu tu msiile, ila mwimwage mchangani kama maji.[#3 Mose 3:17.]

17Lakini ni mwiko kula malangoni pako fungu la kumi la ngano zako, nalo la mvinyo zako mbichi, nalo la mafuta yako, nao wana wa kwanza wa ng'ombe wako nao wana wa kwanza wa mbuzi wako na wa kondoo wako, nayo yo yote ya kuyalipa uliyoyaapa, nayo matoleo yako, utakayoyatoa kwa kupenda mwenyewe, navyo vipaji vya mikono yako vya tambiko vya kunyanyuliwa.

18Haya yote utayala mbele ya Bwana Mungu wako mahali pale tu, Bwana Mungu wako atakapopachagua; hapo na uyale wewe na wana wako wa kiume na wa kike na watumishi wako wa kiume na wa kike, naye Mlawi aliopo malangoni pako, upate kuyafurahia mbele ya Bwana yote, mikono yako iliyoyachukua.[#5 Mose 14:23.]

19Jiangalie tu, usimwache Mlawi siku zote, utakazokuwapo katika nchi yako![#5 Mose 12:12; 14:27.]

20Bwana Mungu wako atakapoipanua mipaka yako, kama alivyokuambia, nawe utakaposema: Nataka kula nyama, kwani roho yangu ina uchu wa nyama, basi, na ule nyama kwa huo uchu wote wa roho yako.

21Kama mahali pale, Bwana Mungu atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, patakuwa mbali kutoka kwako, basi, na utoe wa kuchinja katika ng'ombe wako au katika mbuzi na kondoo wako, Bwana aliokupa, ule nyama, kama nilivyokuagiza, malangoni pako, uukomeshe uchu wote wa roho yako.

22Kama nyama za paa na za kulungu zinavyoliwa, hivyo ndivyo, utakavyozila hizo nyama nazo, mwenye uchafu na mwenye kutakata watazila pamoja.[#5 Mose 12:15.]

23Lakini ushike mwiko huu tu, usile damu! Kwani damu ndiyo yenye roho, haifai ukiila roho pamoja na nyama.[#5 Mose 12:16.]

24Kwa hiyo usiile, ila uimwage mchangani kama maji.

25Usiile, upate kuona mema wewe na wanao watakaokuwapo nyuma yako, ukiyafanya yanyokayo machoni pake Bwana.

26Ni vipaji vyako vitakatifu tu na malipo yao, uliyoyaapa, ndiyo uyachukue kwenda mahali pake, Bwana atakapopachagua.

27Hapo pa kumtambikia Bwana Mungu wako ndipo papasapo, uzitoe ng'ombe zako za tambiko za kuteketezwa nzima, nyama pamoja na damu. Nazo damu za ng'ombe zako nyingine za tambiko sharti zimwagwe hapo pa kumtambikia Bwana Mungu wako, lakini nyama utazila.[#5 Mose 12:6.]

28Angalia, uyasikie vema haya maneno, mimi ninayokuagiza, upate kuona mema kale na kale, wewe na wanao watakaokuwako nyuma yako, utakapoyafanya yaliyo mema nayo yanyokayo machoni pa Bwana Mungu wako.

29Bwana Mungu wako atakapowang'oa mbele yako wamizimu hao, ambao utaingia kwao kuichukua nchi yao, iwe yako, ukiwafukuza, upate kukaa katika nchi yao,

30jiangalie, usinaswe, kwamba uwafuate wao, wakiisha kuangamizwa mbele yako, wala usiulizeulize habari za miungu yao kwamba: Hao wamizimu walivyoitumikia miungu yao, ndivyo, nitakavyofanya nami.[#5 Mose 7:16.]

31Usimfanyizie Bwana Mungu wako hivyo! Kwani yote yaliyo matapisho kwake Bwana kwa kuyachukia waliifanyizia miungu yao, kwani nao wana wao wa kiume na wa kike waliitolea miungu yao na kuwateketeza motoni.

32Maneno haya yote, mimi ninayowaagiza ninyi, sharti myaangalie, myafanye. Msiyaongeze, wala msiyapunguze![#5 Mose 4:2.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania