5 Mose 14

5 Mose 14

Waisiraeli wanakatazwa matanga ya kimizimu.

1Ninyi m watoto wake Bwana Mungu wenu; kwa hiyo msijichanje chale, wala msizinyoe nyushi katikati ya macho yenu kwa ajili ya mfu![#3 Mose 19:27-28.]

2Kwani ninyi m watu watakatifu wa Bwana Mungu wako, maana Bwana akikuchagua kuwa kabila lililo lake mwenyewe kuliko makabila yote yakaayo huku nchini.

Nyama wenye kutakata nao wenye uchafu.

3Usile cho chote kinachotapisha!

4Hawa ndio nyama, mtakaowala: ng'ombe, kondoo na mbuzi,

5kulungu na paa na funo na mbarapi na kuro na pofu na swala.

6Nyama wote wenye kwato zilizopasuka na kutengeka kabisa kuwa kwato mbili, kama ni wenye kucheua, ndio, mtakaowala miongoni mwa nyama.

7Lakini nao hao msiwale miongoni mwao wanaocheua namo miongoni mwao walio wenye kwato zilizopasuka na kutengeka: ngamia na sungura na pelele. Kweli wanacheua, lakini hawapasui kwato, kwa hiyo ni mwiko kwenu.

8Naye nguruwe, kweli anayapasua makwato, lakini hacheui; kwa hiyo ni mwiko kwenu. Nyama zao hao msizile, nayo mizoga yao msiiguse.

9Katika nyama wote waliomo majini mtakula hawa: wote wenye mapezi na magamba mtawala;

10lakini wote wasio wenye mapezi na magamba msiwale! ni mwiko kwenu.

11Kila ndege mwenye kutakata mtakula.

12Lakini wao, mtakaoacha kula nyama zao, ni hawa: kozi na pungu na furukombe,

13na tumbuzi na mwewe na ngusu na ndugu zake,

14na makunguru yote na ndugu zao,

15na mbuni na kinega na dudumizi na kipanga na ndugu zake,

16na mumbi na bundi na yangeyange,

17na korwa na tai na shakwe,

18na korongo na kitwitwi na ndugu zake na hudihuda na popo.

19Wadudu wote wenye mabawa wanaotambaa ni mwiko kwenu, hawaliwi.

20Ndege wote wenye kutakata mtakula.

21Msile kibudu cho chote! Mgeni aliomo malangoni mwako utampa, ale, au utakiuza kwa mtu wa kimizimu. Kwani ninyi m watu watakatifu wa Bwana Mungu wenu. Kitoto cha mbuzi usikipike katika maziwa ya mama yake.[#2 Mose 22:31; 23:19.]

Mafungu ya kumi.

22Mwaka kwa mwaka sharti utoe fungu la kumi la mapato yote ya mbegu zako zitakazotoka shambani.[#3 Mose 27:30.]

23Hili fungu la kumi ulile mbele ya Bwana Mungu wako mahali pale, atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, nalo hilo fungu la kumi ulitolee ngano zako na mvinyo zako mbichi na mafuta yako, tena wana wa kwanza wa ng'ombe nao wa mbuzi na kondoo wako, upate kujifunza kumcha Bwana Mungu wako siku zote.[#5 Mose 12:18.]

24Kama safari ya kutoka kwako kwenda huko itakuwa ndefu zaidi, usiweze kuyapeleka hayo matoleo, kwa kuwa ni mbali zaidi kutoka kwako kwenda mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake, basi, hapo Bwana Mungu wako atakapokubariki,

25yale matoleo yageuze kuwa fedha, kisha hizo fedha zifunge mkononi mwako, upate kwenda nazo mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua.

26Ndipo, utakapoweza kujipatia kwa hizo fedha yote, roho yako itakayotunukia, ng'ombe na mbuzi na kondoo na mvinyo na vileo nayo mengine yote, roho yako itakayoyapenda, ujipatie, kisha utakula hapo mbele ya Bwana Mungu wako, mfurahiwe pamoja wewe nao waliomo nyumbani mwako.

27Naye Mlawi atakayekuwapo malangoni pako usimwache, kwani hana fungu la nchi kwako lililo lake mwenyewe.[#5 Mose 12:19.]

28Miaka mitatu itakapopita, mafungu yote ya kumi utakayoyatolea mapato yako ya mwaka huo, uyaweke malangoni pako.[#5 Mose 26:12-15.]

29Kisha Walawi, kwa kuwa kwako hawana fungu lao la nchi lililo lao wenyewe, na waje pamoja na wageni, nao wliofiwa na wazazi, nao wajane waliomo malangoni mwako, na waje, wale, washibe! Hivyo ndivyo, Bwana Mungu wako atakavyokubarikia kazi zote za mikono yako, utakazozifanya.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania