The chat will start when you send the first message.
1Watambikaji Walawi, ndio shina lote la Lawi, wasipate fungu la nchi kuwa lao wenyewe kwao Waisiraeli. Ng'ombe za tambiko za Bwana za kuteketezwa nayo yampasayo Bwana kupewa yawe yao; ndiyo, watakayokula.[#4 Mose 18:8-20; 5 Mose 10:9; 1 Kor. 9:13.]
2Kweli wasiwe na fungu lililo lao kwao ndugu zao, ila Bwana mwenyewe atakuwa fungu lao, kama alivyowaambia.
3Lakini hii itakuwa haki yao watambikaji kwao watu watakaochinja ng'ombe ya tambiko, kama ni ng'ombe, au kama ni kondoo: sharti wampe mtambikaji mkono na mashavu mawili na matumbo.
4Tena malimbuko ya ngano zako nayo ya mvinyo mbichi nayo ya mafuta, nayo malimbuko ya nywele za kondoo, mkiwanyoa, na mmpe.
5Kwani Bwana Mungu wako amemchagua katika mashina yako yote, asimame na kutumikia katika Jina lake Bwana, yeye na wanawe siku zote.
6Itakapokuwa, Mlawi atoke malangoni pako pawapo pote kwao Waisiraeli, anapokaa ugenini, aende kwa tunu yote ya roho yake mahali pale, Bwana atakapopachagua,
7basi, na atumikie katika Jina la Bwana Mungu wake, kama ndugu zake Walawi wote wanaosimama hapo mbele ya Bwana.
8Watakula sawasawa na kugawiana fungu kwa fungu kuliko yale, atakayoyapata kwa kuuza mali ya baba zake.
9Utakapoingia katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, usijifundishe kuyafanya matapisho ya hao wamizimu.
10Kwako asionekane mtu atakayemtumia mwanawe wa kiume au wa kike kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa, wala asionekane mwenye kuagulia ndege na mawingu, wala mpiga bao, wala mlozi,[#3 Mose 18:21; 19:26,31; 20:27.]
11wala mfinga nyoka kwa uganga, wala mwenye kuuliza mizimu, wala mwenye kujua uchawi wote, wala mfanya mashauri na wafu.[#1 Sam. 28:11.]
12Kwani kila ayafanyaye hayo humchukiza Bwana, naye Bwana Mungu wako anawafukuza wao mbele yako kwa ajili ya hayo machukizo.
13Lakini wewe sharti ukae kwa Bwana Mungu wako pasipo kumkosea.[#1 Mose 6:9; Sh. 15:2.]
14Kwani mataifa hayo, utakayoyafukuza, huwasikia waaguliao mawingu na ndege, lakini wewe Bwana Mungu wako hakukupa ruhusa kuwatumia hao.
15*Miongoni mwa ndugu zako wewe Bwana Mungu wako atakuinulia mfumbuaji atakayelingana na mimi, nanyi sharti mmsikie.[#4 Mose 12:6-8; Yoh. 1:45; 6:14; Tume. 3:22; 7:37; Ebr. 12:24.]
16Ni kwa ajili yao yote, uliyomwomba Bwana Mungu wako kule Horebu siku hiyo ya mkutano kwamba: Nisiendelee kuisikia sauti ya Bwana Mungu wangu na kuuona huu moto mkubwa, nisife.[#2 Mose 20:19; Ebr. 12:19.]
17Ndipo, Bwana aliponiambia: Wamefanya vema waliposema hivyo.[#5 Mose 5:28.]
18Nitawainulia mfumbuaji miongoni mwa ndugu zao atakayelingana na wewe; nitampa maneno yangu kinywani mwake, awaambie yote, nitakayomwagiza.
19Itakuwa, mtu akikataa kuyasikia maneno yangu, atakayoyasema katika Jina langu, mimi nitamlipisha.*
20Lakini mfumbuaji atakayejikuza mwenyewe na kusema neno katika Jina langu, nisilomwagiza kulisema, analolisema katika jina la mungu mwingine, huyo mfumbuaji hana budi kufa.[#5 Mose 13:5; Yer. 14:15.]
21Nawe ukiuliza moyoni mwako: Tutajuaje neno kuwa neno, Bwana asilolisema?
22ni hivi: mfumbuaji akisema neno kwa Jina la Bwana, lakini hilo neno haliji, wala halitimii, basi, hilo ndilo neno, Bwana asilolisema, yule mfumbuaji amelisema kwa kujikuza tu, kwa hiyo usimwogope!