5 Mose 19

5 Mose 19

Miji ya kuikimbilia

(1-13: 4 Mose 35:6-34; Yos. 20.)

1Bwana Mungu wako atakapokwisha kuyang'oa hayo mataifa walio wenye hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe yako, ukae mijini mwao namo nyumbani mwao,[#5 Mose 4:41-43.]

2ndipo ujitengee miji mitatu katikati ya hiyo nchi yako, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe yako.

3Utakapojitengenezea njia za kwenda huko uanze kuigawanya mipaka ya hiyo nchi yako, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe yako mwenyewe, uitoe mafungu matatu, mwuaji apate pa kukimbilia.

4Nalo shauri lake mwuaji atakayekimbilia kwako, apate kupona, liwe hivyo: Itakuwa, mtu ampige mwenzake pasipo kuvijua, pasipo kuwa mchukivu wake tangu zamani.

5Itakuwa, kama mtu akienda na mwenzake mwituni kukata kuni, napo hapo, mkono wake ulipolipandisha shoka kukata mti, chuma kikachomoka katika kipini, kikampata mwenzake, naye akafa, basi, hapo na akimbilie miji hiyo mmojawapo, apate kupona.

6Naye mwenye kuilipiza hiyo damu asimkimbize huyo mwuaji kwa ajili ya moto huo unaowaka moyoni mwake, amkamate, kwa kuwa njia ni ndefu, ampige, azimie roho, naye yule hakukora manza za kuuawa, kwani hakuwa mchukivu wake tangu zamani.

7Kwa sababu hii mimi ninakuagiza kwamba: Jitengee miji mitatu!

8Tena itakuwa, Bwana Mungu wako aipanue mipaka yako, kama alivyowaapia baba zako, ya kuwa atawapa.

9Hivi vitakuwa, ukiyaangalia na kuyafanya haya maagizo yote, mimi ninayokuagiza leo, umpende Bwana Mungu wako, uzishike njia zake siku zote; basi, hapo, hivyo vitakapotimia, sharti hiyo miji mitatu uiongeze kwa kujitengea mji mitatu mingine,

10ni kwamba: katikati ya hiyo nchi yako, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako, isimwagwe damu ya mtu asiyekora manza za kufa, hiyo damu ikakukalia wewe.

11Lakini mtu akiwa mchukivu wa mwenzake, akamvizia na kumnyatianyatia, mwisho akampata, ampige na kuizimiza roho yake, afe kabisa; napo, atakapokimbilia miji hiyo mmojawapo,

12wazee wa mji wake na watume watu, wamchukue kule na kumtia mikononi mwake mlipiza hiyo damu, afe.

13Jicho lako lisimwonee machungu, upate kuondoa kwao Waisiraeli damu ya mtu asiyekora manza za kufa. Ndipo, utakapoona mema.

Mipaka isisogezwe.

14Usimsogezee mwenzako mipaka, wakale waliyoikata penye fungu lako, utakalolichukua, liwe lako katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe yako.[#5 Mose 27:17.]

Mapatilizo ya mashahidi wa uwongo.

15Mtu mmoja asimwondokee mwingine katika shauri la manza zo zote, wala la ukosaji wo wote uliomkosesha mtu kosa lo lote, watu wanalolikosa, ila shauri litawezekana tu kwa ushahidi wa watu wawili au watatu.[#5 Mose 17:6; Yoh. 8:17; 2 Kor. 13:1.]

16Shahidi mkorofi atakapomwinukia mwenzake kumsingizia upotovu,

17Nao watu wawili wanaobishana na waende kusimama mbele ya Bwana na mbele ya watambikaji na mbele ya waamuzi watakaokuwapo siku hizo,[#5 Mose 17:9.]

18nao waamuzi na watafute vema sana iliyo kweli. Nao watakapoona, ya kama yule shahidi ni shahidi wa uwongo, naye alitaka kumkorofisha ndugu yake kwa uwongo,

19basi, na mmfanyie yaleyale, aliyoyawazia kumfanyizia ndugu yake. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako.

20Wao wengine wasiokuwapo watakapovisikia wataogopa, wasiendelee kufanya mambo mabaya kama hayo katikati yako.

21Jicho lako lisiwaonee machungu, ila uwatoze roho kwa roho, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu.[#2 Mose 21:23-25.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania