The chat will start when you send the first message.
1Kisha tukageuka na kuondoka huko, turudi nyikani na kushika nja ya kwenda kwenye Bahari Nyekundu, kama Bwana alivyoniambia, tukazunguka siku nyingi kwenye mlima wa Seiri.[#4 Mose 21:4; 5 Mose 1:40.]
2Kisha Bwana akaniambia kwamba:
3Siku, mlizouzunguka mlima huu, ni nyingi, sasa geukeni kwenda upande wa kaskazini!
4Waagize watu kwamba: Piteni katika mipaka yao ndugu zenu wana wa Esau wanaokaa Seiri! Wao watawaogopa ninyi, lakini jiangalieni sana,[#4 Mose 20:14.]
5msiwapelekee vita! Kwani sitawapa ninyi hata kipande kidogo cha nchi yao, ijapo pawe pa kukanyagia kwa mguu mmoja tu, kwani mlima wa Seiri nilimpa Esau, auchukue, uwe nchi yake.[#1 Mose 36:8,43.]
6Chakula sharti mjinunulie kwao kwa fedha, mpate kula, nayo maji ya kunywa sharti myanunue kwao kwa fedha.
7Kwani Bwana Mungu wako amekubariki katika mambo yote, uliyoyafanya kwa mkono wako, anazijua safari zako, ulizozifanya katika nyika hii kubwa; hii miaka arobaini Bwana Mungu wako amekuwa pamoja na wewe, usikose cho chote.
8Ndipo, tulipoendelea kusafiri na kuondoka kwao ndugu zetu wana wa Esau waliokaa Seiri, tukaziacha njia za huko nyikani na za Elati na za Esioni-Geberi, tukageuka na kushika njia ya kwenda kwenye nyika ya Moabu.
9Ndipo, Bwana aliponiambia: Usiwasonge Wamoabu, wala msiwapelekee vita mkipigana nao! Kwani sitakupa kipande cha nchi yao, mwichukue, iwe yenu, kwa kuwa naliwapa wana wa Loti nchi ya Ari, waichukue, iwe yao.[#1 Mose 19:37.]
10Kale Waemi walikaa huko, nao walikuwa watu wakubwa na warefu wengi mno kama Waanaki.[#5 Mose 1:28.]
11Nao waliwaziwa kuwa Majitu kama Waanaki, lakini Wamoabu waliwaita Waemi.
12Huko Seiri kale walikaa Wahori; ndio, wana wa Esau waliowafukuza na kuwaangamiza mbele yao, kisha wakakaa mahali pao, kama Waisiraeli walivyofanya katika nchi, waliyoichukua, iwe yao, Bwana aliyowapa.[#1 Mose 14:6; 36:20.]
13Sasa inukeni, mkivuke kijito cha Zeredi! Ndipo, tulipokivuka hicho kijito cha Zeredi.[#4 Mose 21:12.]
14Nazo siku, tulizosafiri toka Kadesi-Barnea mpaka tulipokivuka kijito cha Zeredi, zilikuwa miaka 38; ndipo, kile kizazi chote cha wapiga vita kilipokuwa kimeishilizwa makambini, kama Bwana alivyowaapia.[#5 Mose 1:34.]
15Nao mkono wa Bwana ulikuwa ukiwapingia, upate kuwaangamiza makambini, mpaka waishilizwe kabisa.
16Ikawa, wale wapiga vita walipokwisha kuishilizwa wote na kuondolewa kwa wenzao wa ukoo kwa hivyo, walivyokufa,
17Bwana akaniambia kwamba:
18Leo hivi wewe upite mpaka wa Moabu na kupita Ari.[#4 Mose 21:13.]
19Kisha utafika karibu kwao wana wa Amoni; usiwasonge, wala usiwapelekee vita! Kwani sitakupa kipande cha nchi ya wana wa Amoni, ukichukue, kiwe chako, kwani nchi hiyo naliwapa wana wa Loti, waichukue, iwe yao.[#1 Mose 19:38.]
20Nchi hii nayo iliwaziwa kuwa ya Majitu; kale Majitu walikaa huko kweli, nao Waamoni waliwaita Wazamuzumi.
21Nao walikuwa watu wakubwa na warefu wengi mno kama Waanaki, lakini Bwana aliwaangamiza mbele yao; ndipo, walipoichukua nchi yao, iwe yao, wakakaa mahali pao.
22Ni vivyo hivyo, alivyowafanyizia wana wa Esau wanaokaa Seiri, maana mbele yao waliwaangamiza Wahori, wapate kuichukua nchi yao na kukaa huko mahali pao mpaka siku hii ya leo.
23Nao Waawi waliokaa vijijini mpaka Gaza waliangamizwa na Wakafutori waliotoka Kafutori, kisha wao walikaa mahali pao.[#1 Mose 10:14; Yos. 13:3.]
24Nanyi inukeni na kuondoka huku, mkivuke kijito cha Arnoni! Tazama Mwamori Sihoni, mfalme wa Hesiboni, nimemtia mikononi mwako pamoa na nchi yake. Haya! Anza kuichukua ukimpelekea vita, upigane naye!
25Leo hivi nitaanza kuyatisha makabila yote chini ya mbingu, wakustukie kwa kukuogopa; watakapousikia uvumi wako watakutetemekea na kujipinda kwa machungu.
26Ndipo, nilipotuma wajumbe toka nyikani kwa Kedemoti kwake Sihoni, mfalme wa Hesiboni, kumwambia maneno haya ya mapatano kwamba:[#4 Mose 21:21-26.]
27Ninataka kupita katika nchi yako na kwenda njiani tu, nisiondoke njiani kwenda wala kuumeni wala kushotoni.
28Chakula utaniuzia kwa fedha, nipate kula, nayo maji utanipa kwa fedha, nipate kunywa ninataka kupita tu kwa miguu yangu.
29Hivyo ndivyo, walivyonifanyizia nao wana wa Esau wanaokaa Seiri, nao Wamoabu wanaokaa Ari; fanya hivyo nawe, mpaka nitakapouvuka Yordani, niingie nchi, Bwana Mungu wetu aliyotupa.
30Lakini Sihoni, mfalme wa Hesiboni, hakutaka kutupa ruhusa ya kupita kwake, kwa kuwa Bwana Mungu wako alimpa mawazo magumu rohoni na kuushupaza moyo wake, apate kumtia mikononi mwako, kama inavyoelekea sasa.
31Ndipo, Bwana aliponiambia: Tazama, nimeanza kumtoa Sihoni na nchi yake mbele yako. Nawe anza kuichukua nchi yake, iwe yako!
32Sihoni alipotoka asubuhi, yeye pamoja na watu wake wote, wapigane nasi kule Yasa,
33Bwana Mungu wetu akamtoa mbele yetu, tukampiga, yeye na wanawe na watu wake wote,
34tukaiteka miji yake yote siku hizo, tukawatia mwiko wa kuwapo wote pia waliokuwamo mijini, wanawaume na wanawake na watoto, hatukusaza hata mmoja aliyeweza kukimbia.
35Ni nyama tu wa kufuga na nyara za miji, tuliyoiteka, ndizo tulizojichukulia.
36Toka Aroeri ulioko ukingoni kwenye kijito cha Arnoni, katika miji iliyoko kule kwenye kijito mpaka Gileadi haukuwako mji wenye boma refu la kutushinda, yote pia Bwana Mungu wetu aliitoa mbele yetu.
37Nchi ya wana wa Amoni tu hukuikaribia, ile nchi yote iliyoko kando ya kijito cha Yakobo pamoja na miji ya milimani; kwani hiyo yote Bwana Mungu wetu alitukataza kuichukua.