5 Mose 20

5 Mose 20

Mambo ya vita.

1Utakapotoka kwenda vitani kupigana na adui zako, ukaona farasi na magari na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope! Kwani Bwana Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri kukuleta huku yuko pamoja na wewe.

2Tena hapo, mapigano yatakapokuwa karibu, mtambikaji na awakaribie ninyi kusema na watu.

3Awaambie: Sikilizeni, Waisiraeli! Ninyi leo mnakwenda kupigana na adui zenu, lakini kwa hiyo mioyo yenu isilegee, msiwaogope na kutetemeka, wala msiwastuke.

4Kwani Bwana Mungu wenu atakwenda pamoja nanyi kuwapigania na adui zenu, awaokoe.

5Kisha wenye amri na waseme na watu na kuwaambia: Kama yuko mtu aliyejenga nyumba mpya, naye hajaieua, bado, na aende kurudi nyumbani kwake, asife katika mapigano, mtu mwingine akiieua.[#5 Mose 16:18.]

6Au kama yuko mtu aliyepanda shamba la mizabibu naye hajalilimbua, na aende kurudi nyumbani kwake, asife katika mapigano, mtu mwingine akalilimbua.[#3 Mose 19:24-25; 5 Mose 28:30.]

7Au kama yuko mtu aliyeposa mwanamke, naye hajamwoa, na aende kurudi nyumbani kwake, asife katika mapigano, mwingine akamwoa.[#5 Mose 24:5.]

8Kisha mwenye amri na aendelee kusema na watu na kuwaambia: kama yuko mtu mwoga mwenye moyo uliolegea, na aende kurudi nyumbani kwake, asiiyeyushe mioyo ya ndugu zake kuwa, kama moyo wake ulivyo.[#Amu. 7:3.]

9Nao wenye amri watakapokwisha kusema na watu, na waweke wakuu wa vikosi kuwatangulia watu.

Watakavyoifanyizia miji ya adui.

10Utakapokaribia mji kupigana nao, kwanza uulize mapatano.[#4 Mose 21:21-22.]

11Watakapokuitikia kwa kutaka mapatano, wakakufungulia malango, basi, watu wote watakaoonekana humo watakufanyizia kazi za nguvu na kukutumikia hivyo.

12Lakini watakapokataa kukuitikia mapatano wakitaka kupigana na wewe, basi, na uusonge.

13Bwana Mungu wako atakapoutia mikononi mwako, sharti uwapige wa kiume wote waliomo kwa ukali wa upanga.[#4 Mose 31:7,17.]

14Lakini wanawake na watoto na nyama wa kufuga nayo yote yatakayokuwa humo mjini na ujitwalie yote pia kuwa mateka yako ya humo mjini, nawe utaweza kula mateka ya adui zako, Bwana Mungu wako atakayokupa.

15Hivyo ndivyo, utakavyoifanyizia miji yote iliyoko mbali sana kutoka kwako, isiyo miongoni mwa miji ya wamizimu hawa wa huku.

16Lakini katika miji ya haya makabila, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako mwenyewe, usiponye hata mmoja avutaye pumzi.[#Yos. 10:40.]

17Ila sharti uwatie mwiko kabisa wa kuwapo hao Wahiti na Waamori na Wakanaani na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza,[#5 Mose 7:1-2.]

18kusudi wasiwafundishe ninyi kuyafanya hayo matapisho yote, waliyoifanyizia miungu yao, ninyi mkamkosea Bwana Mungu wenu.

19Utakapokaa siku nyingi kwa kusonga mji na kupigana nao, upate kuuteka, usiiharibu miti yake na kuikata kwa shoka, ila ule matunda yao, kwa hiyo usiikate. Au miti ya shambani ni watu, uiendee kuisonga nayo usoni pako?

20Hiyo miti tu, utakayoijua, ya kuwa siyo miti izaayo matunda, na uiharibu na kuikata, uitumie ya kuujengea boma mji huo unaopigana na wewe, hata uanguke.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania