5 Mose 21

5 Mose 21

Kujipozea damu ya mtu asiyejulikana mwuaji wake.

1Atakapoonekana mtu aliyeuawa katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe yako, naye akiwa analala porini, yule aliyemwua asijulikane,

2basi, wazee wako na waamuzi wako na watoke, wazipime njia za kwenda katika miji inayomzunguka yule mtu aliyeuawa.

3Wazee wa mji huo utakaokuwa karibu zaidi ya yule mtu aliyeuawa sharti wachukue mori ya ng'ombe asiyefanyishwa kazi bado, wala asiyevuta bado gari au jembe.

4Huyo mori wazee na wamtelemshe penye mto usiokupwa, pasipolimwa wala pasipopandwa, kisha wamvunje huyo mori shingo huko mtoni.

5Kisha watambikaji Walawi na waje huko, kwani Bwana Mungu wako aliwachagua kumtumikia na kubariki katika Jina lake Bwana, magomvi yote na mapigano yote yamalizwe kwa kusema kwao.[#5 Mose 17:8-9.]

6Kisha wazee wote wa mji huo ulio karibu zaidi ya yule mtu aliyeuawa na wainawe mikono yao juu ya huyo mori aliyevunjwa shingo huko mtoni[#Mat. 27:24.]

7na kusema kwa kupaza sauti: Mikono yetu haikuimwaga damu hii, wala macho yetu hayakuona, ilipomwagwa.

8Bwana, wapoze walio ukoo wako wa Isiraeli, uliowakomboa, usiwalipishe damu ya mtu asiyekora manza iliyomwagwa katikati yao walio ukoo wako wa Isiraeli! Ndipo, watakapopata upozi kwa ajili ya hiyo damu.

9Hivyo ndivyo, utakavyoondoa katikati yako damu ya mtu asiyekora manza, utakapoyafanya haya yaongokayo machoni pake Bwana.[#4 Mose 35:33.]

Wanawake waliotekwa.

10Utakapotoka kwenda kupigana na adui zako, naye Bwana Mungu wako atakapowatia mikononi mwako, uwachukue kuwa mateka.

11Nawe ukiona katika hayo mateka mwanamke mwenye mwili mzuri wa kupendezwa naye, basi, utamchukua kuwa mkeo.

12Kwa hiyo umwingize nyumbani mwako, ajinyoe nywele za kichwani pake, ajikate nazo kucha za vidoleni pake,

13azivue nazo nguo, alizokuwa amezivaa alipotekwa, akae nyumbani mwako na kumwombolezea baba yake na mama yake mwezi mzima, kisha utaingia kwake, uwe mumewe, naye awe mkeo.

14Lakini itakapokuwa, usipendezwe tena naye, utampa ruhusa, ajiendee, atakakopenda, lakini usimwuze kwa fedha, wala usimkorofishe, kwa kuwa ulimtumia kuwa mkeo.

Haki yake mwana wa kwanza.

15Itakuwa, mtu awe na wake wawili, naye mmoja atapendezwa naye, lakini wa pili atachukizwa naye, wakamzalia watoto, yule apendezwaye naye naye yule achukizwaye naye, naye mwana wa kwanza ni wake yule achukizwaye naye.[#1 Mose 29:30.]

16Baadaye siku zitakapotimia, awagawanyie wanawe mali zake, wazichukue, ziwe urithi wao, hataweza kumfanya mwanawe yule apendezwaye naye kuwa mwana wa kwanza mahali pake mwanawe wa kwanza aliyezaliwa naye yule achukizwaye naye,

17ila hana budi kumtokeza kuwa wa kwanza huyo mwana aliye wake mkewe achukizwaye naye, amgawie mafungu mawili ya mali zake zote zinazoonekana kwake, kwani huyo ni wa kwanza, nguvu zake ziliyemzaa; kwa hiyo haki ya kuzaliwa wa kwanza ni yake yeye.[#1 Mose 49:3.]

Wana wasiotii.

18Itakuwa, mtu awe na mwana mtundu na mkatavu asiyesikia wala sauti ya baba yake wala sauti ya mama yake, asisikie, ijapo wamchape,

19basi, baba yake na mama yake na wamkamate, wampeleke kwao wazee wa mji wao langoni pake,

20wawaambie wazee: Huyu mwana wetu ni mtundu na mkatavu, hazisikii sauti zetu, ni mlafi na mnywaji.

21Kisha watu wote wa huo mji wa kwao na wamtupie mawe, afe. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako, kwani Waisiraeli wote watakapovisikia wataogopa.[#5 Mose 13:10-11.]

Mizoga yao walionyongwa.

22Itakuwa, mtu aliyekora manza za kufa auawe, watu wakimtundika mtini.

23Lakini mzoga wake usikae hapo mtini usiku kucha, ila sharti umzike siku iyo hiyo, kwani aliyetundikwa ameapizwa na Mungu; huko ni kwamba: usiipatie uchafu nchi hiyo, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako mwenyewe.[#Yos. 8:29; 10:27; Gal. 3:13.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania