5 Mose 22

5 Mose 22

Maagizo mengine ya kupenda watu na nyama na mengine.

1Utakapoona, ng'ombe au kondoo wa ndugu yako wakipotea, usijifiche kuwa kama mtu asiyewaona, ila sharti uwarudishe kwake ndugu yako.[#2 Mose 23:4.]

2Kama huyo ndugu yako hakai karibu yako, usimjue, uwaweke nyumbani mwako, wakae kwako, mpaka ndugu yako awatafute; ndipo, utakapowarudisha kwake.

3Ndivyo ufanye hata utakapomwona punda wake au nguo zake au cho chote, ndugu yako atakachopotelewa nacho; wewe utakapokiona hutaweza kujificha kuwa kama mtu asiyeona.

4Utakapoona, punda wa ndugu yako au ng'ombe wake wakianguka njiani, usijifiche kuwa kama mtu asiyewaona, ila sharti umsaidie kuwainua.

5Mwanamke asivae cho chote cha mwanamume, wala mwanamume asivae nguo za kike! Kwani kila atakayefanya mambo kama hayo humchukiza Bwana Mungu wako.

6Utakapokuta kiota cha ndege njiani, kiko mbele yako katika mti au chini mchangani chenye makinda au chenye mayai, naye mama akiwaatamia makinda au mayai, usimchukue mama pamoja na watoto,

7ila umwache mama, ajiendee, uchukue watoto tu, upate kuona mema, nazo siku zako ziwe nyingi.[#3 Mose 22:28.]

8Utakapojenga nyumba mpya, sharti juu darini utengeneze kikingio, usifanye nyumbani mwako kuwa mwenye damu ya mtu, mtu akianguka huko.

9Shamba lako la mizabibu usilipande mbegu za namna mbili, lote pia lisiwe mali ya Patakatifu: mbegu, ulizozipanda, pamoja na mazao ya mizabibu.[#3 Mose 19:19.]

10Ukilima usitumie ng'ombe na punda pamoja.

11Usivae nguo iliyofumwa kwa kuchanganya nyuzi za manyoya ya kondoo na za pamba pamoja.[#3 Mose 19:19.]

12Jifanyizie vishada penye pembe zote nne za nguo zako za kijifunika![#4 Mose 15:38.]

Mapatilizo ya ugoni.

13Itakuwa, mtu amwoe mkewe na kuingia kwake, kisha achukizwe naye.

14Kwa hiyo atamsingizia mambo ya uwongo, ampatie jina baya na kusema: Nimemwoa mwanamke huyu; lakini nilipoingia kwake sikumwona kuwa mwanamwali.

15Vitakapokuwa hivyo, babake na mamake yule msichana na wamchukue na kumpeleka kwa wazee wa mji huo langoni pake pamoja nayo yanayoweza kuujulisha uwanawali wake.

16Naye babake yule msichana na awaambie wazee: Nimempa mwanangu mtu huyu kuwa mkewe, kisha akachukizwa naye;

17akamsingizia mambo ya uwongo kwamba: Sikumwona kuwa mwanamwali. Lakini yatazameni haya yanayoujulisha uwanawali wa mwanangu! Kisha waikunjue hiyo nguo mbele ya wazee wa mji huo.

18Kwa hiyo wazee wa mji huo na wamchukue yule mwanamume, wamchape.

19Kisha wamtoze fedha mia, wampe babake msichana, kwa kuwa yule alimpatia msichana wa Kiisiraeli jina baya; kisha awe mkewe, asiweze kumpa ruhusa kwenda zake siku zake zote.[#5 Mose 22:29.]

20Lakini lile neno likiwa la kweli, nayo yanayoujulisha uwanawali wake yasipoonekana,

21na wampeleke yule msichana hapo pa kuiingilia nyumba ya baba yake, hapo watu wa mji wote wampige mawe, hata afe, kwa kuwa alifanya ujinga mbaya kwao Waisiraeli wa kufanya ugoni nyumbani mwa baba yake. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako.[#1 Mose 34:7.]

22Mtu atakapooneka, ya kuwa amelala na mwanamke aliyeolewa na mwingine, sharti wafe wote wawili, yule mwanamume aliyelala na mwanamke, naye mwanamke. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo kwao Waisiraeli.[#3 Mose 20:10.]

23Mwanamwali akiisha kuposwa na mtu, tena mwingine aliyemkuta mjini akilala naye,

24sharti mwapeleke wote wawili langoni pa mji huo, mwapige mawe, hata wafe, yule kijana wa kike, kwa kuwa hakupiga kelele mjini, naye yule mwanamume, kwa kuwa amemkorofisha mchumba wa mwenzake. Hivyo ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako.

25Lakini mwanamume atakapomkuta shambani kijana wa kike aliyekwisha kuposwa, akamkamata kwa nguvu, akalala naye, basi, huyu mwanamume aliyelala naye atakufa peke yake,

26lakini yule kijana wa kike msimfanyizie neno, kwani yule kijana wa kike hakukosa neno lipasalo, auawe, kwa kuwa jambo hili ni sawasawa, kama mtu aliyemwinukia mwenziwe na kumwua, afe.

27Kwani alimkuta shambani, naye yule kijana wa kike aliyekwisha kuposwa alipolia, hakuwako aliyemwokoa.

28Mtu atakapoona mwanamwali asiyeposwa bado, akamshika na kulala naye, basi, wakionwa,

29yule mwanamume aliyelala naye sharti ampe babake yule kijana wa kike fedha hamsini, kisha sharti awe mkewe, kwa kuwa amemkorofisha, naye hana ruhusa kumwacha siku zake zote.[#2 Mose 22:16.]

30Mtu asimchukue mkewe baba yake, wala asiifunue pembe ya nguo zake![#3 Mose 18:8.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania