5 Mose 23

5 Mose 23

Wasioweza nao wanaoweza kupokelewa katika mkutano wa Waisiraeli.

1Katika mkutano wa Bwana asiingie mume aliyekomeshwa kuzaa kwa kupondwa au kwa kukatwa.

2Katika mkutano wa Bwana asiingie mwana wa ugoni wa ndugu na ndugu; ijapo awe wa kizazi chake cha kumi, asiingie katika mkutano wa Bwana.

3Mwamoni wala Mmoabu asiingie katika mkutano wa Bwana, ijapo awe wa kizazi chao cha kumi, kale na kale na wasiingie katika mkutano wa Bwana.

4Kwa kuwa hapo, mlipotoka Misri, hawakuwaendea na kuwapelekea ninyi wala chakula wala maji, tena walimkodisha Bileamu, mwanawe Beori, na kumtoa Petori ulioko Mesopotamia, aje, akuapize.[#4 Mose 22:5-6.]

5Lakini Bwana Mungu wako akakataa kumsikia Bileamu, akakugeuzia kiapizo chake kuwa mbaraka kwa hivyo, Bwana Mungu wako alivyokupenda.

6Nawe usiwatafutie utengemano wala mema yo yote siku zako zote kale na kale!

7Lakini Mwedomu usichukizwe naye; kwani ni ndugu yako. Wala Mmisri usichukizwe naye, kwani ulikuwa mgeni katika nchi yake.[#1 Mose 25:25-26.]

8Wana wao watakaozaliwa wa kizazi cha tatu wataweza kuingia katika mkutano wa Bwana.

Maagizo menginemengine.

9Utakapotoka makambini kuwaendea adui zako, jiangalie, usifanye kibaya cho chote!

10Atakapokuwako kwako mtu asiye mwenye kutakata kwa jambo lililompata na usiku, sharti atoke kwenda nje ya makambi, asiingie ndani ya makambi.[#3 Mose 15:16,18.]

11Itakapokuwa saa ya jioni, ajiogeshe majini, kisha jua litakapokuchwa, aweza kuingia ndani ya makambi.

12Tena huko nje ya makambi uwe na mahali pa kuendea chooni.

13Namo katika vyombo vyako uwe na muo; napo utakapokwenda chooni huko nje, kwanza ufukue nao kishimo, upate kukaa, kisha uyafunike yaliyokutoka.

14Kwani Bwana Mungu wako hutembea katikati ya malango yako, akuponye na kuwatia adui zako mikononi mwako. Kwa hiyo makambi yako sharti yawe matakatifu, asione kwako cho chote kisichofaa, akarudi nyuma na kukuacha.[#3 Mose 26:12.]

15Mtumwa aliyekukimbilia, ajiponye mikononi mwa bwana wake, usimrudishe kwake yule bwana wake.

16Na akae kwako mahali, atakapojichagulia po pote penye malango yako patakapokuwa pema machoni pake, nawe usimsumbue.[#2 Mose 22:21.]

17Katika wana wa kike wa Kiisiraeli wasiwe wagoni wa Patakatifu, wala katika wana wa kiume wa Kiisiraeli wasiwe wagoni wa Patakatifu.[#3 Mose 19:29; 1 Fal. 14:24.]

18Wala usiingize Nyumbani mwa Bwana Mungu wako mshahara wa ugoni wala fedha za kuuza mbwa, ijapo ziwe za kiapo cho chote, kwani Bwana Mungu wako huzikataa zote mbili kwa kuchukizwa nazo.[#3 Mose 18:22; Ufu. 22:15.]

19Usimkopeshe ndugu yako, ujipatie faida ya fedha au faida ya chakula au faida ya cho chote, watu wanachokikopeshea faida.[#2 Mose 22:25; 3 Mose 25:36.]

20Asiye wa Kiisiraeli na umkopeshe, ujipatie faida, lakini ndugu yako usimkopeshe, ujipatie faida, kusudi Bwana Mungu wako akubarikie kazi zote, mikono yako itakazozifanya katika hiyo nchi, utakayoiingia kuichukua, iwe yako.

21Utakapoapa kiapo cha kumpa Bwana Mungu wako cho chote usikawie kukitimiza, kwani Bwana Mungu wako atakitafuta kwako, nawe usipompa utakuwa kama mwenye kujikosesha.[#4 Mose 30:3.]

22Lakini utakapoacha kuapa hivyo hukosi.

23Lakini yaliyokwisha kutoka midomoni mwako sharti uyaangalie na kuyafanya, kama ulivyomwapia Bwana Mungu wako kwa kuyapenda mwenyewe uliyoyasema kwa kinywa chako.

24Utakapoingia mizabibuni kwa mwenzako utaweza kula zabibu, kama roho yako itakavyopenda, hata ushibe, lakini usitie nyingine chomboni.

25Utakapoingia penye ngano za mwenzako zilizoiva utaweza kukonyoa masuke kwa mkono wako, lakini usiyakatekate mabua ya mwenzako kwa mundu.[#Mat. 12:1.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania