5 Mose 24

5 Mose 24

Cheti cha kuachana.

1Mtu akichukua mwanamke na kumwoa, naye halafu asipompendeza machoni pake, kwa kuwa ameona kwake neno lisilofaa, na amwandikie cheti cha kuachana na kumpa mkononi mwake, kisha na amtume kwenda zake na kutoka nyumbani mwake.[#Mat. 5:31-32; 19:7.]

2Atakapokwisha kutoka nyumbani mwake, na aende zake kuwa mke wa mtu mwingine.

3Naye huyu mumewe wa pili atakapochukizwa naye, na amwandikie naye cheti cha kuachana na kumpa mkononi mwake, kisha naye na amtume kwenda zake na kutoka nyumbani mwake. Hata itakapokuwa, huyu mumewe wa pili aliyemchukua kuwa mkewe afe,

4bwana wake wa kwanza aliyemtuma kwenda kwao hana ruhusa kumchukua kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa uchafu, kwani haya humchukiza Bwana. Kwa hiyo usiikoseshe hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako.

Maongozi menginemengine.

5Mtu akichukua mwanamke mpya asitoke kwenda vitani, wala asifanyishwe kazi yo yote nyingine, sharti mwaka mmoja aachwe tu kukaa nyumbani mwake, amfurahishe mkewe, aliyemchukua.[#5 Mose 20:7.]

6Mtu usimtoze mawe ya kusagia, wala hilo la juu tu kuwa rehani, kwani hivyo ungemtoza yule mtu roho kuwa rehani.

7Atakapoonekana mtu atakayemwiba mwingine kwao wana wa Isiraeli, amtumie kuwa mtumwa au amwuze, mwizi huyu hana budi kuuawa; ndivyo, utakavyouondoa ubaya huo katikati yako.[#2 Mose 21:16.]

8Jiangalie, utakapopatwa na pigo la ukoma! Yaangalie sana na kuyafanya yote sawasawa, kama watambikaji Walawi watakavyowafunza ninyi! Kama nilivyowaagiza wao, yaangalieni, myafanye vivyo hivyo![#3 Mose 13; 14:2.]

9Yakumbuke, Bwana Mungu wako aliyomfanyizia Miriamu njiani, mlipotoka Misri.[#4 Mose 12:10-15.]

10Utakapomkopesha mwenzako cho chote, alichokukopa, usiingie nyumbani mwake kumtoza roho yake,

11ila usimame nje, yule mtu uliyemkopesha wewe akutolee rehani yake huko nje.

12Naye kama ni mtu mnyonge, usilale na rehani yake,

13ila umrudishie rehani yake, jua litakapokuchwa, apate kulala na nguo yake ya kujifunika, akubariki. Hii itakupatia wongofu machoni pake Bwana Mungu wako.[#2 Mose 22:26.]

14Usimkorofishe mtu wa kazi aliye mkiwa na mkosefu wa mali, kama ni wa ndugu zako au mmojawapo wa wageni watakaokaa katika nchi yako malangoni pako,[#3 Mose 19:13.]

15ila umpe mshahara wake siku iyo hiyo, jua lisije kuchwa, akiwa hajapata, kwani ni mkiwa, huutaka sana wa kujitunza, asimlilie Bwana kwa ajili yako, ukawa mwenye kujikosesha.

16Baba asiuawe kwa ajili ya mwana, wala mwana asiuawe kwa ajili ya baba, ila kila mtu auawe kwa ajili ya kosa lake mwenyewe.[#2 Fal. 14:6; Ez. 18:19-20.]

17Usipotoe shauri la mgeni wala la mwana aliyefiwa na wazazi, wala mjane usimtoze nguo yake kuwa rehani![#2 Mose 22:21-22.]

18Nawe kumbuka, ya kama ulikuwa mtumwa huko Misri, Bwana Mungu wako akakukomboa na kukutoa huko. Kwa sababu hii mimi ninakuagiza kuyafanya haya.[#5 Mose 16:12.]

19Utakapoyavuna mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda mmoja shambani, usirudi kuuchukua, ila uache, uwe wa mgeni au wa mwana aliyefiwa na wazazi au wa mjane, Bwana Mungu wako akubarikie kazi zote za mikono yako.[#3 Mose 19:9-10.]

20Utakapoupukutisha mchekele wako usiurudie tena kuyapukutisha nayo matawi yake, matunda yao na yawe ya mgeni au ya mwana aliyefiwa na wazazi au ya mjane.

21Utakapochuma mizabibuni kwako, usiirudie mizabibu kuiokoteza. Na iwe ya mgeni au ya mwana aliyefiwa na wazazi au ya mjane.

22Nawe kumbuka, ya kama ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri! Kwa sababu hii mimi ninakuagiza kuyafanya haya.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania