The chat will start when you send the first message.
1Watu watakapogombana na waende shaurini, waamuliwe, mwamuzi akimtokeza asiyekosa kuwa hakukosa, naye aliyekosa kuwa amekosa.
2Huyo mkosaji akipaswa na kupigwa, mwamuzi na amlaze chini, wampige mbele yake fimbo zilizoyapasa maovu yake, nazo zihesabiwe.
3Wakiisha kumpiga 40 wasiendelee! Kwani wakiendelea kumpiga kuzipita hizo, mapigo yatazidi, naye ndugu yako atabezwa machoni pako.[#2 Kor. 11:24.]
4Ng'ombe mwenye kupura ngano usimfunge kinywa![#1 Kor. 9:9; 1 Tim. 5:18.]
5Ndugu wakikaa pamoja, mmoja wao akafa pasipo kuacha mwana wa kiume, mkewe yule aliyekufa asiolewe nje na mtu mgeni, ila ndugu yake mumewe sharti amwingilie na kumchukua kuwa mkewe, amsimikie ndugu yake unyumba.[#Ruti 4:5; Mat. 22:24.]
6Naye mwana wa kwanza, huyu mwanamke atakayemzaa, sharti amwandike kwa jina la ndugu yake aliyekufa, hilo jina lake lisifutwe kwao Waisiraeli.
7Lakini yule mtu asipopendezwa kumchukua mkewe ndugu yake, huyu mke wa ndugu yake na apande kwenda langoni kwa wazee, awaambie: Ndugu yake mume wangu amekataa kumwinulia ndugu yake jina kwao Waisiraeli, asipotaka kumsimikia unyumba kwa kunichukua.
8Kisha wazee wa mji huo na wamwite, waseme naye. Atakaposimama na kusema: Sipendezwi kumchukua,
9yule mkewe ndugu yake na amkaribie machoni pao wazee, amvue kiatu mguuni pake na kumtemea mate usoni, kisha na aseme kwamba: Mtu asiyeijenga nyumba ya ndugu yake na afanyiziwe hivyo!
10Kwa hiyo na aitwe jina lake kwao Waisiraeli: Nyumba ya mvuliwa kiatu.
11Watu wawili walio ndugu wakipigana, naye mkewe mmoja wao akaja kumponya mumewe mkononi mwake anayempiga, akaupeleka mkono wake na kumkamata penye soni,
12sharti umkate huo mkono wake pasipo kumwonea huruma.
13Mfukoni mwako usiwe na vyuma vya kupimia vya namna mbili, vikubwa na vidogo.[#3 Mose 19:35-36.]
14Wala nyumbani mwako usiwe na pishi za namna mbili, kubwa na ndogo.
15Vyuma vyako vya kupimia sharti viwe vizima vilivyo sawasawa, nazo pishi zako ziwe nzima zilizo sawasawa, siku zako zipate kuwa nyingi katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa.
16Kwani Bwana Mungu wako huwachukia wanaoyafanya hayo yote, wao wote wafanyao mapotovu.[#Mika 6:11.]
17Yakumbuke, Waamaleki waliyokufanyizia njiani, mlipotoka Misri![#2 Mose 17:8-16.]
18Walikushambulia njiani, wakawauwa wote waliokufuata nyuma kwa kuwa wanyonge, nawe ulikuwa umechoka, ukataka kuzimia roho, lakini wao hawakumwogopa Mungu.
19Kwa hiyo hapo, Bwana Mungu wako atakapokutulizia adui zako wote watakaokuzunguka pande zote katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, uichukue, iwe fungu lako mwenyewe, hapo sharti utoweshe ukumbusho wa Waamaleki chini ya mbingu; usivisahau![#1 Sam. 15:2-3.]