The chat will start when you send the first message.
1Utakapoingia katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, iwe fungu lako, utakapoichukua na kukaa huko,[#2 Mose 23:19; 34:26; 3 Mose 2:14.]
2sharti uchukue malimbuko ya mazao yote ya hiyo nchi, utakayoyatoa katika hiyo nchi yako, Bwana Mungu wako atakayokupa. Kisha uyaweke kikapuni, uende mahali pale, Bwana Mungu wako atakapopachagua kuwa pa kulikalishia Jina lake.
3Utakapofika umwendee mtambikaji atakayekuwapo siku hizo, umwambie: Leo hivi ninamshuhudia Bwana Mungu wako, ya kama nimeingia katika hiyo nchi, Bwana aliyowaapia baba zetu kutupa sisi.
4Ndipo, mtambikaji atakapokichukua hicho kikapu mkononi mwako, akiweke mbele ya hapo pa kumtambikia Bwana Mungu wako.
5Kisha uanze kusema mbele ya Bwana Mungu wako kwamba: Baba yangu alikuwa Mshami mwenye kutangatanga, akashuka Misri, akakaa huko ugenini pamoja na watu wachache, akapata kuwa huko taifa kubwa yenye nguvu na watu wengi.[#1 Mose 46:5.]
6Lakini Wamisri wakatufanyizia mabaya, wakatutesa na kutufanyisha kazi ngumu za utumwa.
7Ndipo, tulipomlilia Bwana, Mungu wa baba zetu, naye Bwana akazisikia sauti zetu, akayaona mateso yetu na masumbuko yetu na masongano yetu,
8Bwana akatutoa katika nchi ya Misri kwa kutoa nguvu za kiganja chake na kwa kuukunjua mkono wake na kwa mambo makuu yaliyostusha na kwa vielekezo na kwa vioja,[#5 Mose 5:15.]
9akatuingiza mahali hapa, akatupa nchi hii, nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali.
10Sasa tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya nchi hii, wewe Bwana uliyonipa. Kisha yaweke mbele ya Bwana Mungu wako na kumwangukia Bwana Mungu wako.
11Ndivyo, utakavyoyafurahia mema yote, Bwana Mungu wako aliyokupa wewe na mlango wako, uyafurahie wewe pamoja na Mlawi na mgeni atakayekaa kwako.[#5 Mose 16:11,14.]
12Katika mwaka wa tatu, ndio mwaka wa kutolea mafungu ya kumi, utakapokwisha kuyatoa mafungu ya kumi yote ya mapato yako, umpe Mlawi na mgeni na mwana aliyefiwa na wazazi na mjane, wayale malangoni pako, hata washibe.[#5 Mose 14:27-29.]
13Kisha useme mbele ya Bwana Mungu wako: Nimeyaondoa nyumbani mwangu yaliyo matakatifu, nikampa Mlawi na mgeni na mwana aliyefiwa na wazazi na mjane, nikayafanya maagizo yako yote sawasawa, kama ulivyoniagiza, sikupita agizo lako lo lote, wala sikusahau mojawapo.
14Nilipolala tanga sikuyala hata kidogo, wala nilipokuwa mwenye uchafu sikuyaondoa hata kidogo, wala sikutoa mengine kumpa mwenzangu aliyefiwa, ila nimeisikia sauti ya Bwana Mungu wangu, nikayafanya yote, kama ulivyoniagiza.
15Chungulia toka mbinguni penye Kao lako takatifu, uwabariki walio ukoo wako wa Isiraeli nayo nchi hii, uliyotupa, kama ulivyowaapia baba zetu. Nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali.
16Leo hivi Bwana Mungu wako anakuagiza kufanya maongozi haya na maamuzi haya, uyaangalie, upate kuyafanya kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.
17Nawe umesema leo, ya kama unamtaka Bwana, awe Mungu wako, ya kama unataka kuzishika njia zake na kuyaangalia maongozi yake na maagizo yake na maamuzi yake na kuisikia sauti yake.
18Naye Bwana amekuambia leo, ya kama anakutaka, uwe ukoo wake ulio wake mwenyewe, kama alivyokuagia, tena ya kama anakutaka, uyaangalie maagizo yake yote;
19tena ya kama anataka kukufanya kuwa mkuu kuliko mataifa yote, aliowafanya, upate matukuzo na jina la utukufu kuliko wao, ni kwamba: upate kuwa ukoo mtakatifu wa Bwana Mungu wako, kama alivyosema.[#5 Mose 4:6; 28:1.]