5 Mose 27

5 Mose 27

Mawe ya kuwakumbushia Waisiraeli Maonyo.

1Mose pamoja na wazee wa Waisiraeli wakawaagiza watu kwamba: Yaangalieni maagizo yote, mimi ninayowaagiza leo![#Yos. 8:30-35.]

2Siku hiyo, mtakapouvuka Yordani kwenda katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa, ujisimikie mawe makubwa na kuyapaka chokaa!

3Kisha uyaandike maneno yote ya Maonyo haya utakapokwisha kuvuka, kusudi upate kuingia katika nchi hiyo, Bwana Mungu wako atakayokupa. Nayo ni nchi ichuruzikayo maziwa na asali, kama Bwana Mungu wa baba zako alivyokuambia.

4Hapo mtakapouvuka Yordani yasimikeni mlimani kwa Ebali mawe haya, ninayowaagiza leo, kisha myapake chokaa!

5Kisha umjengee huko Bwana Mungu wako mahali pa kumtambikia, napo pajengwe kwa mawe yasiyochongwa kwa chuma cho chote.[#2 Mose 20:25.]

6Hapo pa kumtambikia Bwana Mungu wako sharti upajenge kwa mawe yaliyo mazima, kisha umtolee Bwana Mungu wako juu yake ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima.

7Uchinje nazo ng'ombe za tambiko za shukrani, upate kula huko na kumfurahia Bwana Mungu wako.[#5 Mose 12:7.]

8Nayo yale mawe uyaandike maneno yote ya haya Maonyo na kuyachora vema!

9Kisha Mose na watambikaji Walawi wakawaambia Waisiraeli wote kwamba: Nyamaza kimya, Isiraeli, upate kusikia! Leo hivi umepata kuwa ukoo wake Bwana Mungu wako.[#5 Mose 26:18-19.]

10Kwa hiyo isikie sauti ya Bwana Mungu wako, uyafanye maagizo yake na maongozi yake, mimi ninayokuagiza leo!

Maapizo ya mlimani kwa Ebali.

11Siku hiyo Mose akawaagiza watu kwamba:

12Hawa na waende kusimama mlimani kwa Gerizimu na kuwabariki hawa watu, mtakapokwisha kuuvuka Yordani: Simeoni na Lawi na Yuda na Isakari na Yosefu na Benyamini.[#5 Mose 11:29.]

13Nao hao na waende kusimama mlimani kwa Ebali na kuapiza: Rubeni na Gadi na Aseri na Zebuluni na Dani na Nafutali.

14Kisha Walawi na waanze kusema na kuwaambia watu wote wa Waisiraeli kwa kupaza sauti:

15Na awe ameapizwa mtu atakayefanya kinyago cha kuchonga au cha kuyeyusha na kuvisimamisha na kufichaficha! Kwani Bwana huchukizwa navyo, navyo ni kazi za mikono ya fundi. Nao watu wote na waitikie: Amin![#2 Mose 20:23; 34:17.]

16Na awe ameapizwa atakayembeza baba yake na mama yake! Nao watu wote na waitikie: Amin![#2 Mose 21:17.]

17Na awe ameapizwa atakayeusogeza mpaka wa mwenzake! Nao watu wote na waitikie: Amin![#5 Mose 19:14.]

18Na awe ameapizwa atakayempoteza kipofu njiani! Nao watu wote na waitikie: Amin![#3 Mose 19:14.]

19Na awe ameapizwa atakayepotoa shauri la mgeni au la mwana aliyefiwa na wazazi au la mjane! Nao watu wote na waitikie: Amin![#2 Mose 22:21-22.]

20Na awe ameapizwa atakayelala na mkewe baba yake! Kwani huko atazifunua nguo za baba yake. Nao watu wote na waitikie: Amin![#3 Mose 18:8.]

21Na awe ameapizwa atakayelala na nyama wo wote! Nao watu wote na waitikie: Amin![#2 Mose 22:19.]

22Na awe ameapizwa atakayelala na umbu lake aliye binti baba yake au binti mama yake! Nao watu wote na waitikie: Amin![#3 Mose 18:9,11.]

23Na awe ameapizwa atakayelala na mkwewe! Nao watu wote na waitikie: Amin![#3 Mose 18:17.]

24Na awe ameapizwa atakayempiga mwenzake mahali panapojificha! Nao watu wote na waititike: Amin![#4 Mose 35:20.]

25Na awe ameapizwa atakayechukua mapenyezo, ampige mtu na kuimwaga damu yake asiyekosa! Nao watu wote na waitikie: Amin![#2 Mose 23:8; 5 Mose 16:19.]

26Na awe ameapizwa asiyeyasimamisha maneno ya Maonyo haya na kuyafanya! Nao watu wote na waitikie: Amin![#Gal. 3:10.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania