The chat will start when you send the first message.
1Haya ndiyo maneno ya Agano, Bwana aliyomwagiza Mose kulifanya na wana wa Isiraeli katika nchi ya Moabu, tena liko Agano lile, alilolifanya nao mlimani kwa Horebu.[#5 Mose 5:2.]
2Mose akawaita Waisiraeli wote, akawaambia: Ninyi mliona yote, Bwana aliyomfanyizia Farao, nao watumishi wake wote na wenyeji wote wa nchi yake machoni penu katika nchi ya Misri.[#2 Mose 19:4.]
3Yale majaribu makubwa macho yako yaliyaona kuwa vielekezo na vioja vikubwa.
4Lakini mpaka siku hii ya leo Bwana hajawapa ninyi mioyo inayovitambua, wala macho yanayoona, wala masikio yanayosikia.[#5 Mose 5:29; Yes. 6:9-10.]
5Nayo hiyo miaka 40, niliyowatembeza nyikani, nguo zenu hazikuchakaa miilini penu,[#5 Mose 8:2,4.]
6wala viatu vyako havikuchakaa miguuni pako; hamkula mikate, wala hamkunywa mvinyo au kileo kingine, mpate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu wenu.
7Mlipofika mahali hapa, Sihoni, mfalme wa Hesiboni, na Ogi, mfalme wa Basani, walitaka kupigana na sisi, nasi tukawapiga,[#4 Mose 21:21-35.]
8tukazichukua nchi zao, tukawapa wao Warubeni na Wagadi nao wa nusu la shina la Manase, ziwe mafungu yao.[#4 Mose 32.]
9Sasa yaangalieni maneno ya Agano hili na kuyafanya, mpate kufanikiwa mambo yote, mtakayoyafanya.
10Leo mnasimama nyote mbele ya Bwana Mungu wenu, walio vichwa vyenu vya mashina yenu, wazee wenu na wakuu wenu, nanyi nyote mlio waume wa Kiisiraeli,
11wana wenu na wake zenu na mgeni wako aliye makambini mwako naye mchanja kuni zako naye mchota maji yako.
12Huku ni kwamba, upate kuandamana nalo Agano la Bwana Mungu wako, analolifanya leo na wewe, nacho kiapo chake.
13Naye anakuweka leo kuwa ukoo wake, naye atakuwa Mungu wako, kama alivyokuambia, kama alivyowaapia nao baba zako Aburahamu na Isaka na Yakobo.
14Lakini si ninyi peke yenu, ninaofanya nao Agano hili na kuwaapia kiapo hiki,[#5 Mose 5:3.]
15ila ni wao wanaosimama leo hapa pamoja na sisi mbele ya Bwana Mungu wetu, tena ni wao nao wasiokuwapo leo hapa pamoja na sisi.
16Kwani ninyi mnajua wenyewe, jinsi tulivyokaa katika nchi ya Misri, tena tulivyopita katikati ya wamizimu, ambao mlipita kwao,
17mkayaona matapisho yao na vinyago vyao, walivyokuwa navyo, vilivyo miti tu na mawe au fedha na dhahabu.
18Lakini kwenu asiwe mtu mume wala mke wala mlango wala shina watakaoigeuza mioyo yao, wamwache Bwana Mungu wetu wakienda kuitumikia miungu ya hao wamizimu, lisichipuke kwenu shina litakalozaa majani yenye sumu na uchungu kama wa nyongo.[#Ebr. 12:15.]
19Mtu aliye hivyo atakapoyasikia maneno ya kiapizo hiki asijibariki mwenyewe moyoni mwake kwamba: Nitapata kutengemana, ijapo niendelee kuufuata ushupavu wa moyo wangu, kusudi niyapokonye mabichi na makavu.
20Aliye hivyo Bwana atakataa kabisa kumwondolea mabaya, ila hapo ndipo, makali ya Bwana pamoja na wivu wake yatakapowaka moto wenye moshi kwa kumkasirikia huyo mtu, navyo viapizo vyote vilivyoandikwa humu kitabuni vitamkalia, naye Bwana atalifuta jina lake chini ya mbingu.[#5 Mose 28:15-68.]
21Tena Bwana atamtenga na kumtoa katika mashina yote ya Isiraeli, apatwe na mabaya, vimtimilikie viapizo vyote vya Agano hili lililoandikwa katika kitabu cha Maonyo haya.
22Navyo vizazi vijavyo nyuma, ndio wana wenu watakaotokea nyuma yenu, nao wageni watakaotoka katika nchi ya mbali watayaona hayo mapigo ya nchi hii nayo magonjwa, Bwana aliyoiuguza;
23kwani nchi yake nzima ataiteketeza kwa mawe ya kiberiti na kwa chumvi, isiweze kupandwa wala kuotesha kijiti, wala majani yo yote yasiweze kumea huko, mwangamizo wake uwe kama ule wa Sodomu na wa Gomora, nao wa Adima na wa Seboimu, Bwana aliyoiangamiza kwa makali yake yaliyowaka moto.[#1 Mose 19:24; Hos. 11:8.]
24Watakapoviona wamizimu wote watauliza: Bwana akiifanyizia nchi hii mambo kama haya, ni kwa sababu gani? Makali makuu yawakayo moto hivyo yako na maana gani?
25Ndipo, watu watakapowaambia: Ni kwa kuwa waliliacha Agano la Bwana Mungu wa baba zao, alilolifanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri;
26wakaenda zao, wakatumikia miungu mingine na kuitambikia, nayo ni miungu, wasiyoijua, isiyowagawia kitu.
27Ndipo, makali ya Bwana yalipoiwakia nchi hii, akailetea viapizo vyote vilivyoandikwa humu kitabuni.
28Bwana akawang'oa katika nchi yao kwa makali yaliyowaka moto na kwa machafuko makubwa, akawatupa, wajiendee katika nchi nyingine, kama inavyoelekea leo.
29Mambo yaliyofunikwa ni yake Bwana Mungu wenu; lakini yaliyofunuliwa ni yetu sisi na ya wana wetu, tuyafanye maneno yote ya Maonyo haya.[#5 Mose 32:34; Sh. 147:19-20.]