The chat will start when you send the first message.
1Hayo yote yatakapokujia, hayo ya mbaraka nayo ya kiapizo, niliyoyaweka mbele yako, nawe utakapoyaingiza moyoni mwako katika wamizimu wote, Bwana Mungu wako atakapokukumba kwenda kwao,[#5 Mose 28.]
2napo utakaporudi kwa Bwana Mungu wako, uisikie sauti yake na kuyafuata yote, mimi ninayokuagiza leo, uyafanye wewe na wanao kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote,[#3 Mose 26:40.]
3ndipo, Bwana Mungu wako atakapoyafungua mafungo yako kwa kukuhurumia, akukutanishe tena na kukutoa katika makabila yote, Bwana Mungu wako alikokutawanya.[#Yer. 29:14; 32:37; Amo. 9:14.]
4Ijapo, uwe umekumbwa kwenda hata mapeoni kwa mbingu, huko nako Bwana Mungu wako atakukusanya na kukuchukua huko,
5Bwana Mungu wako akupeleke katika nchi, baba zako waliyoichukua, iwe yao, uichukue nawe, iwe yako, kisha atakukalisha vema na kukufanya kuwa wengi kuliko baba zako.
6Naye Bwana Mungu wako atautahiri moyo wako nayo mioyo yao wa uzao wako, mmpende Bwana Mungu wenu kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote, mpate kupona.[#5 Mose 10:16; Yer. 4:4; Ez. 11:19; Rom. 2:29; Kol. 2:11.]
7Kisha Bwana Mungu wako atavitimiza hivyo viapizo vyote, viwapate adui zako na wachukivu wako waliokufukuza.
8Lakini wewe utaisikia tena sauti ya Bwana, uyafanye maagizo yake yote, mimi ninayokuagiza leo.
9Ndipo, Bwana Mungu wako atakapokupatia mema mengi ya kuyasaza katika kazi zote za mikono yako na katika mazao ya tumbo lako na katika mazao ya nyama wako wa kufuga na katika mazao ya mashamba yako, kwani Bwana atakufurahia tena, akupatie mema, kama alivyowafurahia baba zako.
10Hayo utayapata utakapoisikia sauti ya Bwana Mungu wako, uyaangalie magizo na maongozi yake yaliyoandikwa katika kitabu cha Maonyo haya, utakapomrudia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.
11Kwani hili agizo, mimi ninalokuagiza leo, silo gumu, usiweze kulifanya, wala haliko mbali, usiweze kulifikia:
12haliko mbinguni, useme: Yuko nani atakayetupandia mbinguni kulichukua na kutuletea, tulisikie, tupate kulifanya?[#Rom. 10:6-8.]
13Wala haliko ng'ambo ya bahari, useme: Yuko nani atakayetuvukia bahari kwenda ng'ambo ya huko kulichukua na kutuletea, tulisikie, tupate kulifanya?
14Kwani neno hilo linakukalia karibu sana, limo kinywani mwako namo moyoni mwako, upate kulifanya.
15Tazama, nimeweka leo mbele yako maisha na mema, tena kifo na mabaya.[#5 Mose 11:26; 28:2,15.]
16Mimi ninakuagiza leo kumpenda Bwana Mungu wako na kuzishika njia zake na kuyaangalia maagizo yake na maongozi yake na maamuzi yake, ndipo, utakapopona, watu wako wawe wengi, naye Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi hiyo, wewe unayokwenda kuichukia, iwe yako.
17Lakini moyo wako utakapogeuka, usisikie, utadanganyika, utambikie miungu mingine na kuitumikia.
18Nami ninawatangazia leo hivi: Mtaangamia kabisa, msikae siku nyingi katika hiyo nchi, unayouvukia Yordani, uiingie na kuichukua, iwe yako.[#5 Mose 4:26.]
19Ninawatajia leo hivi mbingu na nchi kuwa mashahidi, ya kuwa nimeweka mbele yako maisha na kifo, mbaraka na kiapizo, ukayachagua maisha, upate kuishi wewe nao wa uzao wako,[#5 Mose 4:26.]
20mkimpenda Bwana Mungu wenu, mwisikie sauti yake na kugandamana naye; kwani humu ndimo, yalimo maisha yako na wingi wa siku zako za kukaa katika hiyo nchi, Bwana aliyowaapia baba zako Aburahamu na Isaka na Yakobo kuwapa.