The chat will start when you send the first message.
1Mose akaenda, akawaambia Waisiraeli wote maneno haya,[#5 Mose 34:7; 4 Mose 20:12.]
2akawaambia: Mimi leo ni mwenye miaka 120, siwezi tena kuingia na kutoka, naye Bwana aliniambia: Hutauvuka huu Yordani.
3Bwana Mungu wako atakutangulia mwenyewe, ukivuka; naye ndiye atakayeyaangamiza mataifa hayo mbele yako, upate kuzichukua nchi zao. Naye Yosua ndiye atakayekuvukisha, kama Bwana alivyosema.[#5 Mose 3:28.]
4Naye Bwana atawafanyizia, kama alivyowafanyizia Sihoni na Ogi, wale wafalme wa Waamori, na wenyeji wa nchi zao, aliowaangamiza.[#4 Mose 21:21-35.]
5Bwana atawatoa mbele yenu, mwafanyizie na kulifuata agizo, nililowaagiza ninyi.[#5 Mose 7:2.]
6Jipeni mioyo, mpate nguvu, msiwaogope, wala msiwastuke! Kwani Bwana Mungu wako atakwenda pamoja na wewe, hataondoka kwako, wala hatakuacha.
7Kisha Mose akamwita Yosua, akamwambia machoni pao Waisiraeli wote: Jipe moyo, upate nguvu! Kwani wewe utaingia na watu hawa katika nchi hiyo, Bwana aliyowaapia baba zao kuwapa, kisha utawagawia mafungu yao ya nchi.[#Yos. 1:6.]
8Naye Bwana mwenyewe atakutangulia, awe pamoja na wewe; hataondoka kwako, wala hatakuacha; usiogope, wala usiingiwe na vituko!
9Mose akayaandika Maonyo haya, akawapa watambikaji, wana wa Lawi waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana, na wazee wote wa Waisiraeli.
10Kisha Mose akawaagiza kwamba: Kila miaka saba itakapopita, mwaka wa kuachilia madeni utakapotimia, penye sikukuu ya Vibanda,[#5 Mose 15:1.]
11Waisiraeli wote watakapokuja kumtokea Bwana Mungu wako mahali pale, atakapopachagua, ndipo, utakapoyasoma Maonyo haya masikioni pao Waisiraeli wote.
12Hapo uwakutanishe watu wote, waume na wake na wana na wageni watakaokuwako malangoni pako, wayasikie, wapate kujifunza, wamwogope Bwana Mungu wenu, wayaangalie na kuyafanya maneno yote ya Maonyo haya.
13Nao wana wao wasioyajua na wayasikie, wapate kujifunza, wamwogope Bwana Mungu wenu siku zote, mtakazokuwako katika hiyo nchi, mnayoivukia Yordani, mpate kuichukua, iwe yenu.
14Bwana akamwambia Mose: Tazama, siku zako zimetimia, upate kufa! Mwite Yosua, mwende kusimama Hemani mwa Mkutano, nipate kumwagiza kazi. Ndipo, Mose na Yosua walipokwenda kusimama Hemani mwa Mkutano.
15Bwana akatokea mle Hemani katika wingu lililokuwa kama nguzo, nalo hilo wingu lililokuwa kama nguzo likasimama hapo pa kuliingilia Hema.[#2 Mose 40:34.]
16Bwana akamwambia Mose: Tazama, unakwenda kulala na baba zako. Kisha watu wataondoka kwenda kufanya ugoni wa kufuata miungu migeni ya nchi hiyo, watakayoiingia, lakini mimi wataniacha na kulivunja Agano, nililolifanya nao.
17Siku hiyo makali yangu yatawawakia, nami nitawaacha na kuuficha uso wangu, wasiuone; kisha wataliwa na kupatwa na mabaya mengi ya kuwasonga. Siku hiyo watasema: Kumbe haya mabaya hayakutupata, kwa kuwa Mungu wetu hayumo katikati yetu?
18Lakini mimi nitauficha uso wangu kabisa siku hiyo kwa ajili ya mabaya yote, waliyoyafanya walipoigeukia hiyo miungu mingine.
19Sasa jiandikieni wimbo huu, mwafundishe wana wa Isiraeli na kuutia vinywani mwao, kusudi wimbo huu uwe shahidi wangu kwao wana wa Isiraeli![#5 Mose 32.]
20Kwani nitawaingiza katika hiyo nchi, niliyowaapia baba zao, ichuruzikayo maziwa na asali. Lakini watakapokula na kushiba na kunenepa, ndipo, watakapogeukia miungu mingine, waitumikie na kunibeza mimi na kulivunja Agano langu.[#5 Mose 32:15.]
21Kisha hapo, mabaya mengi ya kuwasonga yatakapowapata, wimbo huu na uwajibu na kuwashuhudia, kwani hautasahauliwa vinywani mwao walio uzao wako. Kwani ninayajua mawazo yao, wanayoyatunga leo, kwa kuwa sijawaingiza bado katika hiyo nchi, niliyowaapia.[#Sh. 139:2.]
22Siku iyo hiyo Mose akauandika wimbo huo, akawafundisha wana wa Isiraeli kuuimba.
23Naye Yosua, mwana wa Nuni, Bwana akamwagiza kwamba: Jipe moyo, upate nguvu! Kwani wewe utawaingiza wana wa Isiraeli katika hiyo nchi, niliyowaapia; nami nitakuwa pamoja na wewe.
24Mose alipokwisha kuyaandika maneno ya Maonyo haya katika kitabu na kuyamaliza yote,
25Mose akawaagiza Walawi waliolichukua Sanduku la Agano la Bwana kwamba:
26Kichukueni kitabu cha Maonyo haya, mkiweke kando ndani ya Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu, kiwe humo ndani shahidi wako!
27Kwani ninaujua ukatavu wako na ugumu wa ukosi wako; tazameni, siku hizi za leo, ninapokuwa bado mwenye uzima pamoja nanyi, mmekuwa wenye kumkataa Bwana. Tena itakuwaje, nitakapokwisha kufa?
28Wakusanyeni mbele yangu wazee wote wa mashina yenu na wakuu wenu, niyaseme masikioni pao hayo maneno ya kuwatajia mbingu na nchi kuwa mashahidi.[#5 Mose 32:1.]
29Kwani ninajua, ya kama hapo, nitakapokwisha kufa, mtafanya mabaya sana mkiondoka katika njia, niliyowaagiza; kwa hiyo ubaya utawapata siku za mwisho, kwani mtayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bana, mmkasirishe kwa kazi za mikono yenu.
30Kisha Mose akayasema maneno ya wimbo huu masikioni pao wa mkutano wote wa Waisiraeli na kuyamaliza yote.