5 Mose 32

5 Mose 32

Wimbo wa Mose.

1Yasikilizeni, ninyi mbingu, nitakayoyasema!

Nawe nchi, yasikilize maneno ya kinywa changu!

2Mafunzo yangu na yatiririke kama maji ya mvua,

maneno yangu na yadondoke kama umande,,

kama manyunyu yanayonyunyiziwa majani mabichi,

kama matone ya mvua yanayotonea vijiti!

3Kwani nitalitangaza Jina la Bwana, nanyi mpeni ukuu aliye Mungu wetu!

4Ni mwamba, matendo yake humalizika, kwani njia zake zote huendelea sawa, ni Mungu mtegemevu asiye na upotovu, ni mwenye wongofu, tena ni mnyofu.

5Wasio watoto wake kwa kuwa wachafu, humfanyia mabaya, ndio kizazi chenye upotovu, hupenda kubisha.[#Yes. 1:2-4.]

6Mbona mnamlipa Bwana hivyo? M wapumbavu wasiojua maana? Kumbe siye baba yako aliyekununua? Siye aliyekufanya na kukutengeneza vema?[#2 Mose 4:22; Yes. 63:16; Mal. 1:6.]

7Zikumbuke siku za kale, uitambue miaka yao vizazi vilivyopita! Mwulize baba yako! Atakusimulia; waulize wazee! Nao watakuambia.[#Sh. 77:12.]

8Alioko huko juu alipoyagawia mataifa mafungu yao ya nchi, alipowatawanya wana wa watu, ndipo, alipoiweka mipaka ya makabila kwa hesabu yao wana wa Isiraeli.[#1 Mose 11:8; Tume. 17:26.]

9Kwani fungu lake Bwana ni huu ukoo wake, aliojipatia kwa kura kuwa wake, ndio wa Yakobo.

10Alimwona katika nchi ya nyikani isiyo ya watu, nayo ilikuwa inatisha kwa ngurumo za nyama wa jangwani, akamkingia pande zote na kumjengea; kama ni mboni ya jicho lake, ndivyo, alivyomlinda.[#Sh. 17:8; Zak. 2:8.]

11Alikuwa kama tai akitaka kuwainua hao wanawe kiotani na kupapatika juu yao hayo makinda yake; ndivyo, alivyoyakunjua mabawa yake, amchukue, ndivyo, alivyompeleka, akizikalia mbawa zake.[#2 Mose 19:4; Sh. 36:8.]

12Yeye Bwana peke yake ndiye aliyemwongoza, mungu mwingine wa ugenini hakuwa naye.

13Akampitisha juu ya nchi akimlisha mazao ya mashambani, akamnyonyesha asali ya ngomeni na mafuta ya mwambani[#Sh. 81:17.]

14na siagi za ng'ombe na maziwa ya kondoo, nayo mafuta yao wana kondoo, nayo ya madume ya kondoo wa Basani, nayo ya madume ya mbuzi, nayo mafuta menginemengine kama ya kiini cha ngano, ukanywa nazo mvinyo nyekundu zilizo damu za zabibu.

15Lakini Yeshuruni* aliponona akapiga mateke kwa kunona na kunenepa na kwa kushiba sana; ndipo, yeye alipomtupa Mungu, naye ndiye aliyemfanya; akambeza yule aliyekuwa mwamba wa wokovu wake.[#Yes. 44:2; 5 Mose 31:20.]

16Kwa kufuata miungu migeni wakamchokoza, kwa kufanya yaliyomchukiza wakamkasirisha.

17Ng'ombe za tambiko wakaitolea nayo mizimu isiyo Mungu, hata miungu mingine, wasiyoijua; kwa kuzushwa siku hizo za karibu ilikuwa mipya, nao baba zenu walikuwa hawakuipa macheo.

18Aliyekuzaa ukamwazia kuwa si kitu, naye ni mwamba; ukamsahau Mungu, ambaye ulizaliwa naye.

19Bwana alipoyaona akawatupa kwa kuwakasirikia wanawe wa kiume na wa kike.

20Akasema: Na niufiche uso wangu, wasiuone, mimi niuone mwisho wao, jinsi utakavyokuwa, kwani ndio kizazi chenye mapotovu, ndio wana wasiotegemeka.

21wamenichokoza kwa kufuata isiyo miungu, wakanikasirisha kwa kufanya yasiyo na maana, kwa hiyo nami na niwachokoze nikiwaletea watu wasio watu, na niwakasirishe nikiwaletea taifa la watu wasiojua maana.[#Yer. 2:11; Rom. 10:19.]

22Kwani uko moto uliowashwa na makali yangu, nao ukachoma na kufika hata kuzimuni kuliko chini ya nchi, ukaila nchi na mazao yake, nayo misingi ya milima ukaiunguza.

23Nitawapatia mabaya mengi, yawe chungu zima, nitaimaliza mishale yangu kwa kuwapiga.[#Sh. 91:5.]

24Itakapokuwa, wazimie roho kwa njaa tu, tena itakapokuwa, waliwe na moto ulio wa homa kali, itakapokuwa, wapatwe na magonjwa yenye uchungu, ndipo, nitakapotuma kwao nyama wenye meno makali na nyoka wenye sumu watambaao uvumbini.

25Upanga utawaua wana huko nje, namo nyumbani mwao yatakuwa mastusho; ndipo, watakapokufa vijana wa kiume na wa kike, hata wachanga pamoja na wazee.

26Ningesema: Na niwapeperushe, niwakomeshe watu, wasiwakumbuke tena.

27Lakini ninayaogopa matata ya adui, wale wapingani wao wasibishe kwamba: Mikono yetu ndiyo inayopasa kutukuzwa, kwani aliyeyafanya haya yote siye Bwana.

28Kwani ndio taifa la watu waliopotelewa na akili, kwa hiyo hakuna utambuzi unaooneka kwao.[#Yes. 27:11; Yer. 4:22.]

29Kama wangekuwa werevu wa kweli, wangeijua maana yao haya, wangeutambua nao mwisho utakaowapata wenyewe.

30Inawezekanaje, mtu mmoja akifukuza watu elfu, au wawili wakikimbiza watu maelfu kumi? Sio kwa sababu yule aliye mwamba wao amekwisha kuwauza? Sio kwa sababu Bwana amewatia mikononi mwao wengine?[#3 Mose 26:8,36,37.]

31Kwani mwamba wao wale si kama mwamba wetu, nao adui zetu wenyewe hawana budi kuviitikia.

32Kwani mizabibu yao ni ileile ya Sodomu, nayo mashamba yao ni yaleyale ya Gomora, maana zabibu zao ni zenye sumu, navyo vichala vyao ni vyenye uchungu.[#Yes. 1:10.]

33Kwa kuwa uchungu wa majoka nvinyo zao huwasha; kama sumu kali za pili zilivyo, ndivyo, zilivyo nazo.

34Kumbe haya hayakuwekwa na kufungiwa kwangu? Kumbe hayamo katika vilimbiko vyangu kwa kutiwa muhuri?[#5 Mose 29:29.]

35Lipizi ni langu mimi, ni mimi nitakayelipisha. Miguu yao itakapoteleza, ndipo, litakapokuwa, kwani siku ya mwangamizo wao iko karibu, nayo yatakayowapata yanapiga mbio kufika upesi.[#Sh. 94:1; Rom. 12:19; Ebr. 10:30.]

36Kwani Bwana atawaamulia walio ukoo wake, walio watumishi wake ndio, atakaowahurumia; atakapoziona nguvu za mikono yao kuwa zimekwisha kabisa, atakapoona, ya kama hakuna tena mwenye nguvu kwao wala kwao waliofungwa, wala kwao waliofunguliwa:[#1 Fal. 14:10.]

37ndipo, atakapouliza: Miungu yao iko wapi? Uko wapi mwamba wao, waliouegemea?

38Wako wapi walioyala mafuta ya ng'ombe zao za tambiko? Wako wapi waliozinywa mvinyo za vinywaji vyao vya tambiko? Na wainuke, wawasaidie ninyi wakija kwenu kuwakingia![#Amu. 10:14.]

39Tazameni sasa: Mimi kama nilivyokuwa, ndivyo, nilivyo, hakuna Mungu tena kuliko mimi! Mimi ni mwenye kuua na mwenye kurudisha uzimani, ni mwenye kupiga kidonda, nami ni mwenye kuponya, hakuna awezaye kuokoa mkononi mwangu.[#2 Mose 15:26; 5 Mose 4:35; 1 Sam. 2:6; Iy. 5:18; Yes. 45:5; Hos. 6:1-2.]

40Kwani nauinua mkono wangu kuuelekeza mbinguni kwamba: Hivyo nilivyo mwenye uzima kale na kale,[#2 Mose 6:8; Ez. 33:11.]

41nitakapounoa upanga wangu ulio wenye umeme, nao mkono wangu utakaposhika mapatilizo, ndipo, nitakapowalipiza wapingani wangu na kuwalipisha wachukivu wangu.

42Nitailewesha mishale yangu, izidi kunywa damu, nao upanga wangu utakula nyama, ni damu zao watakaouawa nazo zao watakaotekwa, ni nyama zao walio vichwa na watawalaji wa adui.

43Shangilieni, enyi wamizimu, pamoja nao walio ukoo wake! Kwani damu za watumishi wake huzilipizia kisasi, huwalipiza wapingani wake, awapatie upozi walio wenyeji wa nchi yake, walio ukoo wake.[#Rom. 15:10.]

44Mose akenda, akayasema maneno yote ya wimbo huu masikioni pa watu, yeye na Yosua, mwana wa Nuni.

45Mose alipokwisha kuwaambia Waisiraeli wote maneno haya yote,

46akawaambia: Yawekeni mioyoni mwenu maneno haya yote, mimi ninayowashuhudia leo, nanyi mwaagize wana wenu, wayaangalie na kuyafanya maneno yote ya Maonyo haya![#5 Mose 6:7.]

47Kwani hili si neno la kusimuliana tu ninyi kwa ninyi, ila ni uzima wenu. Nanyi mtakapolifanya neno hili, siku zenu zitakuwa nyingi za kukaa katika hiyo nchi, mnayoivukia Yordani, mwichukue, iwe yenu.[#3 Mose 18:5.]

Mose anafumbuliwa na Bwana, atakapokufa.

48Siku iyo hiyo Bwana akamwambia Mose kwamba:

49Kwenye milima hii ya Abarimu uupande huo mlima wa Nebo ulioko katika nchi ya Wamoabu, unaoelekea Yeriko, uitazame nchi ya Kanaani, mimi nitakayowapa wana wa Isiraeli, iwe yao.[#4 Mose 27:12; 33:48.]

50Utakapokwisha kuupanda mlima huo utakufa, uchukuliwe kwenda kwao walio ukoo wako, kama kaka yako Haroni alivyokufa mlimani kwa Hori na kuchukuliwa kwenda kwao walio ukoo wake.[#4 Mose 20:23-29.]

51Kwani mlikataa kunitii katikati ya wana wa Isiraeli kwenye Maji ya Magomvi kule Kadesi katika nyika ya Sini, mkaacha kunitakasa katikati ya wana wa Isiraeli.[#4 Mose 20:12-13.]

52Kwa sababu hii utaiona hiyo nchi mbele yako, lakini hutaingia katika hiyo nchi, nitakayowapa wana wa Isiraeli.[#5 Mose 34:4.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania