5 Mose 4

5 Mose 4

Mose anawahimiza Waisiraeli, wayaangalie Maonyo.

1Sasa Isiraeli, yasikilize maongozi na maamuzi, nitakayowafundisha, myafanye, mpate kupona na kuiingia na kuichukua hiyo nchi, Bwana Mungu wa baba zenu atakayowapa, iwe yenu.

2Hayo, mimi nitakayowaagiza, msiyaongeze, wala msiyapunguze, ila yaangalieni haya maagizo ya Bwana Mungu, mimi nitakayowaagiza ninyi![#5 Mose 12:32; Fano. 30:6; Ufu. 22:18-19.]

3Macho yenu yameyaona, Bwana aliyomfanyizia Baali-Peori, kwani wao wote waliomfuata Baali-Peori amewaangamiza Bwana Mungu wako, watoweke kwako.[#4 Mose 25:3-9.]

4Lakini ninyi mliogandamana na Bwana Mungu wenu mnaishi nyote hata leo.

5Tazameni, nimewafundisha ninyi maongozi na maamuzi, kama Bwana Mungu wangu alivyoniagiza; yafanyeni yayo hayo katika nchi hiyo, mtakayoiingia kuichukua, iwe yenu.

6Yaangalieni, myafanye! Kwani huo utakuwa werevu wenu wa kweli na utambuzi wenu machoni pao yale makabila watakayoyasikia hayo maongozi yenu yote, waseme; Kumbe watu hawa ni werevu wa kweli na watambuzi, kwa hiyo ni kabila kubwa.

7Kwani liko taifa gani kubwa, miungu yake inalolikalia karibu hivi, kama Bwana Mungu wetu alivyo karibu kwetu po pote, tunapomlilia?[#5 Mose 33:29; 2 Sam. 7:23.]

8Tena liko taifa gani kubwa lililo lenye maongozi na maamuzi yaongokayo kama haya maonyo yote, mimi ninayowatolea ninyi leo masikioni penu?

9Jiangalie tu na kuiangalia roho yako, usiyasahau kabisa hayo mambo, macho yako yaliyoyaona, yasiondoke moyoni mwako siku zote, utakazokuwapo. Nawe uyajulishe kwa wanao na kwa wana wa wanao![#Sh. 103:2.]

10Wakumbushe mambo ya siku ile, uliposimama mbele ya Bwana Mungu wako kule Horebu, Bwana aliponiambia: Kusanya kwangu watu hawa, niseme maneno yangu masikioni mwao, wajifunze kunicha siku zote, watakazokuwapo katika nchi, kisha wawafundishe wana wao nao.[#2 Mose 19:17; 5 Mose 6:7; 11:19.]

11Napo, mlipomkaribia na kusimama mlimani chini, mlima ukawaka moto mpaka juu ndani ya mbinguni, kukawa na giza na mawingu meusi kabisa.

12Ndipo, Bwana aliposema nanyi toka motoni, nanyi mkazisikia sauti za maneno yake, lakini hakuna mwenye mwili, mliyemwona, ni kuzisikia hizo sauti tu.

13Ndivyo, alivyowatangazia Agano lake, alilowaagiza kulifanya, yale maagizo kumi, kisha akayaandika katika mbao mbili za mawe.[#2 Mose 31:18.]

14Mimi nami Bwana akaniagiza siku hizo kuwafundisha maongozi na maamuzi, myafanye katika hiyo nchi, mnayotaka kuivukia, mwichukue, iwe yenu.

15Ziangalieni sana roho zenu! Kwani hamkuona mwenye mwili ye yote siku hiyo, Bwana aliposema nanyi kule Horebu toka motoni.

16Msijiponze na kujifanyizia kinyago cho chote cha kuchongwa, wala cha kuyeyushwa, wala cha kuchorwa maweni kwa mfano wa mtu mume au mke,[#2 Mose 20:4.]

17wala kwa mfano wo wote wa nyama wa huku nchini, wala kwa mfano wo wote wa ndege mwenye mabawa ya kurukia angani,

18wala kwa mfano wo wote wa dudu atambaaye mchangani, wala kwa mfano wo wote wa samaki wa majini chini ya nchi!

19Wala usiyainue macho yako na kuyaelekeza mbinguni, ulitazame jua na mwezi na nyota, hivyo vikosi vya mbinguni, usijaribiwe kuviangukia na kuvitumikia, kwa kuwa Bwana Mungu wako aliviwekea makabila yote pia yaliyoko chini ya mbingu yote nzima.[#5 Mose 17:3.]

20Lakini ninyi Bwana aliwachukua na kuwatoa katika tanuru ya kuyeyushia vyuma, ndio Misri, mwe kabila llilo lake yeye mwenyewe, kama inavyoelekea leo.[#2 Mose 19:5-6.]

21Kisha Bwana akanikasiria mimi kwa ajili yenu, akaapa, kwamba nisiuvuke Yordani, nisiingie hiyo nchi njema, Bwana Mungu wako atakayokupa wewe, iwe fungu lako mwenyewe.[#5 Mose 3:26.]

22Kwa hiyo mimi nitakufa katika nchi hii pasipo kuuvuka Yordani; lakini ninyi mtauvuka, mwichukue hiyo nchi njema, iwe yenu.

23Jiangalieni, msilisahau Agano la Bwana Mungu wenu, alilolifanya nanyi, msijifanyizie kinyago cho chote cha kuchongwa, wala cha kuyeyushwa kwa mfano wo wote, Bwana Mungu wako aliokukataza.

24Kwani Bwana Mungu wako ni moto ulao, yeye ni Mungu mwenye wivu.[#2 Mose 20:5; 5 Mose 9:3; Yes. 10:17; Ebr. 12:29.]

25Mtakapozaa wana na wana wa wana, mwe wazee katika nchi hiyo, msijiponze na kujifanyizia kinyago cho chote cha kuchongwa, wala cha kuyeyushwa, kwani hivyo mtafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana Mungu wenu, mmkasirishe.

26Kwa hiyo nazitaja mbingu na nchi, ziwashuhudie leo hivi, ya kama hivyo mtaangamia upesi na kutoweka katika nchi hiyo, mnayovukia Yordani, mje kuichukua, iwe yenu, hamtakaa siku nyingi ndani yake, ila mtaangamizwa kabisa.[#5 Mose 30:19; 31:28; 32:1.]

27Yeye Bwana atawatawanya katika makabila mengine, msalie wachache wanaohesabika upesi kwao wamizimu, Bwana atakakowapeleka.

28Huko ndiko, mtakakotumikia miungu iliyo kazi za mikono ya watu, iliyo miti na mawe, isiyoona, isiyosikia, isiyokula, isiyonusa.[#5 Mose 28:36; Sh. 115:4-7.]

29Lakini mtakapomtafuta huko Bwana Mungu wenu mtamwona, ukimtafuta kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.[#Sh. 27:8; Yer. 29:13-14.]

30Utakaposongeka kwa kupatwa na mambo hayo yote siku zile za mwisho, ndipo, utakaporudi kwa Bwana Mungu wako, uzisikilize sauti zake.[#3 Mose 26:40.]

31Kwani Bwama Mungu wako ni Mungu mwenye huruma, hatakuacha kabisa, wala hatakuangamiza kabisa, wala hatalisahau Agano, alilowaapia baba zako.

32Uliza tu mambo ya siku za kale zilizokuwa mbele yako tangu siku ile, Mungu alipomwumba Adamu na kumweka katika nchi, tena chunguza tangu mwisho wa huku wa mbingu hata mwisho wa huko wa mbingu, kama lilifanyika, au kama lilisikilika jambo kubwa kama hili.

33Wako watu walioisikia sauti ya Mungu, akisema toka motoni, kama wewe ulivyoisikia, kisha wawepo wenye uzima?[#2 Mose 20:1,19.]

34Au Mungu alijaribu hata penginepo kuja kujichukulia taifa moja katikati ya mataifa mengine kwa majaribu na kwa vielekezo na kwa vioja na kwa kupiga vita na kwa kutoa nguvu za kiganja chake na kwa kuukunjua mkono wake na kwa matisho makuu yanayoogopesha, kama Bwana Mungu wenu alivyowafanyizia ninyi kule Misri machoni pako?

35Wewe ulionyeshwa hayo, upate kujua, ya kuwa Bwana ni Mungu, hakuna mwingine tena, asipokuwa yeye peke yake.[#5 Mose 32:39.]

36Uliisikia sauti yake, ikitoka mbinguni, ipate kukuonya, nako huku nchini alikuonyesha moto wake mkubwa, nako kutoka humo motoni ukaisikia sauti yake.

37Kwa kuwa aliwapenda baba zako, akawachagua halafu wao wa uzao wao, akakutoa Misri kwa nguvu zake kuu akikuongoza kwa uso wake,[#2 Mose 33:14.]

38afukuze mbele yako mataifa makubwa yenye nguvu za kukushinda wewe, akuingize kwao na kukupa nchi yao, iwe yako, kama inavyoelekea leo.

39siku hii ya leo yajue na kuyaweka moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu mbinguni juu na huku nchini chini, hakuna mwingine tena.

40Kwa hiyo yaangalieni maongozi yake na maagizo yake, mimi ninayokuagiza leo, upate kuona mema wewe na wanao watakaokuwapo nyuma yako, siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi, akupayo Bwana Mungu wako, iwe yako siku zote.

Miji mitatu ya kuikimbilia.

41Kisha Mose akatenga miji mitatu ng'ambo ya Yordani ya maawioni kwa jua,[#4 Mose 35:6-29; 5 Mose 19:2-13.]

42mtu apate kuikimbilia, kama amemwua mwenziwe pasipo kujua, naye alipokuwa si mchukivu wake tangu zamani, basi, atakapokimbilia mmojawapo hiyo miji, awe amepona.

43Nayo ni hii: Beseri wa nyikani katika nchi ya tambarare kwa Warubeni na Ramoti wa Gileadi kwa Wagadi na Golani wa Basani kwa Wamanase.

44Haya ndiyo maonyo, Mose aliyowawekea wana wa Isiraeli;

45tena ndiyo mashuhuda na maongozi na maamuzi, Mose aliyowaambia wana wa Isiraeli, walipotoka Misri.

46Aliyasema ng'ambo ya huku ya Yordani katika bonde linaloelekea Beti-Peori katika nchi ya Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekaa Hesiboni, Mose na wana wa Isiraeli waliyempiga walipotoka Misri.

47Nayo nchi yake wakaichukua, iwe yao, hata nchi ya Ogi, mfalme wa Basani; hawa wafalme wawili wa Waamori ndio waliokaa ng'ambo ya Yordani ya maawioni kwa jua,

48toka Aroeri ulioko ukingoni kwenye kijito cha Arnoni mpaka milimani kwa Sioni, ndio Hermoni,[#5 Mose 3:8-9.]

49nayo nyika yote ya ng'ambo ya Yordani ya maawioni kwa jua mpaka kwenye bahari ya nyikani chini ya matelemko ya Pisiga.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania