The chat will start when you send the first message.
1Mose akawapazia sauti Waisiraeli wote, akawaambia: Sikieni, Waisiraeli, maongozi na maamuzi, mimi ninayoyasema leo masikioni mwenu, mjifundishe na kuyaangalia, mpate kuyafanya!
2Bwana Mungu wetu alifanya Agano na sisi kule Horebu;[#2 Mose 19:5; 5 Mose 29:1.]
3Agano hilo Bwana hakulifanya na baba zetu, ila na sisi wenyewe tuliopo leo hapa sote wenye uzima.[#5 Mose 29:14-15.]
4Huko mlimani Bwana alisema nasi uso kwa uso toka motoni.[#2 Mose 19:19; 5 Mose 5:24.]
5Siku hiyo mimi nilisimama katikati ya Bwana nanyi, niwatangazie Neno la Bwana, kwani mliuogopa ule moto, kwa hiyo hamkupanda mlimani; naye alisema:[#2 Mose 19:16.]
(6-31: 2 Mose 20.)6Mimi ndimi Bwana Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa.
7Usiwe na miungu mingine ila mimi![#5 Mose 11:16,28.]
8Usijifanyie kinyago, wala mfano wo wote wa vitu vilivyoko mbinguni juu, wala vilivyoko nchini chini, wala vilivyomo majini chini ya nchi![#5 Mose 27:15.]
9Usivitambikie, wala usivitumikie! Kwani mimi Bwana Mungu wako ni Mungu mwenye wivu; manza za baba nitazipatilizia wana, nikifikishe kizazi cha tatu na cha nne, kwao wanichukiao.
10Lakini nitawafanyizia mema, nikifikishe hata kizazi cha maelfu, kwao wanipendao na kuyashika maagizo yangu.
11Usilitaje Jina la Bwana Mungu wako bure! Kwani Bwana hatamwachilia alitajaye Jina lake bure.
12Ishike siku ya mapumziko kuitakasa, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza!
13Siku sita sharti ufanye kazi, uyamalize mambo yako yote!
14Lakini siku ya saba ndiyo ya kumpumzikia Bwana Mungu wako. Hapo usifanye kazi yo yote, wala wewe, wala mwanao wa kiume, wala wa kike, wala mtumishi wako wa kiume, wala wa kike, wala ng'ombe wako wala punda wako wala nyama wako ye yote wa kufuga, wala mgeni wako aliomo malangoni mwako, mtumishi wako wa kiume na wa kike apate kupumzika kama wewe!
15Sharti ukumbuke, ya kama ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, naye Bwana Mungu wako akakutoa huko kwa kutoa nguvu za kiganja chake na kwa kuukunjua mkono wake; kwa hiyo Bwana Mungu wako alikuagiza kuifanya siku ya mapumziko.[#5 Mose 15:15; 16:12; 24:18.]
16Mheshimu baba yako na mama yako, kama Bwana Mungu wako alivyokuagiza, siku zako zipate kuwa nyingi, nawe upate kuona mema katika nchi, akupayo Bwana Mungu wako!
17Usiue!
18Usizini!
19Usiibe!
20Usimshuhudie mwenzio uwongo!
21Usimtamani mke wa mwenzio!
Wala usiitamani nyumba ya mwenzio, wala shamba lake,
wala mtumishi wake wa kiume, wala wa kike,
wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote,
mwenzio alicho nacho!
22Maneno haya Bwana aliwaambia wao wote wa mkutano wenu kule mlimani kwa sauti kuu toka motoni mle winguni mwenye weusi, hakuongeza neno, kisha akayaandika katika mbao mbili za mawe, akanipa mimi.[#2 Mose 31:18.]
23Ikawa, mlipoisikia sauti toka gizani, nao mlima ulipowaka moto, mkanikaribia ninyi mliokuwa vichwa vya mashina yenu na wazee wenu,
24mkasema: Tazama, Bwana Mungu wetu ametuonyesha utukufu na ukuu wake, tukaisikia nayo sauti yake toka motoni, siku hii ya leo tumeona, ya kuwa Bwana anasema na mtu, naye hafi.[#5 Mose 4:33.]
25Sasa mbona tufe, moto huu mkubwa ukitula? Tukiendelea kuisikia tena sauti ya Bwana Mungu wetu hatuna budi kufa.
26Kwani yuko wapi mwingine mwenye mwili, ndiye aisikie kama sisi sauti ya Mungu Mwenye uzima, akisema toka motoni, kisha awepo mwenye uzima?
27Nenda wewe, uyasikilize yote, Bwana Mungu wetu atakayoyasema, kisha wewe tuambie yote, Bwama Mungu wetu aliyoyasema! Nasi tutakapoyasikia tutayafanya.
28Bwana alipozisikia sauti za maneno yenu, mliyoniambia, yeye Bwana akaniambia: Nimezisikia sauti za maneno ya watu hawa, waliyokuambia, hayo yote waliyoyasema ni mema.
29Laiti wangekuwa siku zote wenye mioyo inayoniogopa hivyo, wayaangalie maagizo yangu yote, wao na wana wao wapate kuona mema kale na kale![#4 Mose 11:29; 5 Mose 29:4.]
30Nenda, uwaambie: Rudini tu mahemani mwenu!
31Lakini wewe uje hapa kusimama kwangu, nikuambie maagizo na maongozi na maamuzi yote, utakayowafundisha, wayafanye katika nchi hiyo, mimi nitakayowapa, waichukue, iwe yao.
32Kwa hiyo angalieni, mfanye, kama Bwana Mungu wenu alivyowaagiza ninyi, msiondoke kwake kwenda wala kuumeni wala kushotoni![#5 Mose 4:2; 28:14; Yos. 1:7; Fano. 4:27.]
33Ila njia zote, Bwana Mungu wenu alizowaagiza ninyi, zishikeni na kuzifuata, mkae uzimani na kuona mema, nazo siku zenu ziwe nyingi katika nchi, mnayokwenda kuichukua, iwe yenu.