The chat will start when you send the first message.
1Nayo haya ndiyo maagizo na maongozi na maamuzi, Bwana Mungu wenu aliyoniagiza, niwafundishe ninyi, mpate kuyafanya katika nchi, mnayoivukia kuichukua, iwe yenu.
2Sharti umwogope Bwana Mungu wako, uyaangalie maongozi na maagizo yake yote, ninayokuagiza, wewe na wanao na wana wa wanao siku zote za maisha yako, kusudi siku zako zipate kuwa nyingi.
3Isiraeli, yasikie na kuyaangalia, uyafanye, kusudi uone mema, nanyi mpate kuwa wengi sana, kama Bwana Mungu wa baba zako alivyokuagia kukupa nchi ichuruzikayo maziwa na asali.
4*Sikia, Isiraeli: Bwana Mungu wetu ni Bwana peke yake.[#Mar. 12:29; 1 Kor. 8:4,6.]
5Nawe umpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote na kwa nguvu yako yote.[#5 Mose 10:12; Mat. 22:37.]
6Maneno haya, ninayokuagiza leo, sharti yawe moyoni mwako.[#5 Mose 11:18-20.]
7Jikaze kuwafundisha watoto wako na kuyasema nao ukikaa nyumbani mwako, ukienda safari zako, ukitaka kulala, hata ukiamka![#1 Mose 18:19.]
8Yafunge mkononi pako kuwa kielekezo, yawe napo pajini pako katikati ya macho yako![#2 Mose 13:9.]
9Yaandike vizingitini namo milangoni nyumbani mwako!
10Hapo Bwana Mungu wako atakapokuingiza katika hiyo nchi, aliyowaapia baba zako Aburahamu na Isaka na Yakobo, kwamba akupe wewe miji mikubwa mizuri, usiyoijenga,
11na nyumba zijaazo mema yote, usizozijaza, na visima vilivyochimbuliwa, usivyovichimbua, na mizabibu na michekele, usiyoipanda, basi, hapo utakapoila na kushiba,[#5 Mose 8:10.]
12jiangalie, usimsahau Bwana aliyekutoa katika nchi ya Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa!
13Mwogope Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye! Hapo utakapoapa litaje Jina lake!*[#5 Mose 10:20; Mat. 4:10.]
14Msifuate miungu mingine miongoni mwa miungu ya makabila yanayowazunguka!
15Kwani Bwana Mungu wako anayekaa katikati yako ni Mungu mwenye wivu; angalia, makali yake Bwana Mungu wako yasikuwakie, akakuangamiza, utoweke juu ya nchi.[#2 Mose 20:5.]
16Msimjaribu Bwana Mungu wenu, kama mlivyomjaribu kule Masa.[#2 Mose 17:2,7; Mat. 4:7.]
17Yaangalieni sana maagizo ya Bwana Mungu wenu na mashuhuda yake na maongozi yake, aliyoyaagiza!
18Yafanye yaongokayo nayo yafaayo machoni pake Bwana, kusudi uone mema, upate kuingia katika hiyo nchi njema, Bwana aliyowaapia baba zako, uichukue, iwe yako.
19Naye na akupe kuwakimbiza adui zako wote mbele yako, kama Bwana alivyosema.[#2 Mose 23:27-28.]
20Mwanao atakapokuuliza siku zijazo kesho kwamba: Nini maana yao haya mashuhuda na maongozi na maamuzi, Bwana Mungu wetu aliyowaagiza ninyi?[#2 Mose 13:14.]
21ndipo umwambie mwanao: Sisi tulikuwa watumwa wa Farao kule Misri, lakini Bwana akatutoa Misri kwa mkono wake wenye nguvu,
22Bwana alipofanya machoni petu kule Misri vielekezo na vioja vikubwa vilivyomwogopesha Farao na mlango wake wote.
23Ndivyo, alivyotutoa huko na kutuleta huku, atupe nchi hii, aliyowaapia baba zenu.
24Ndipo, Bwana alipotuagiza kuyafanya haya maongozi yote kwa kumcha Bwana Mungu wetu, tuone mema siku zote za maisha yetu, kama inavyoelekea leo.
25Nao wongofu wetu ndio huu wa kujiangalia, tuyafanye haya maagizo yote mbele ya Bwana Mungu wetu, kama alivyotuagiza.