The chat will start when you send the first message.
1Bwana Mungu wako atakapokuingiza katika nchi hiyo, utakayoiingia kuichukua, iwe yako, ndpo, atakapong'oa huko mbele yako mataifa mengi, Wahiti na Wagirgasi na Waamori na Wakanaani na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi, ndio mataifa saba yaliyo yenye watu wengi na yenye nguvu kuliko wewe.[#5 Mose 31:3.]
2Bwana Mungu wako atakapowatoa mbele yako, uwapige, sharti uwatie mwiko kabisa wa kuwapo, usifanye agano nao, wala usiwahurumie.[#4 Mose 21:2.]
3Wala usioane nao: mwanao wa kike usimpe mwana wa kiume wa kwao, wala mwana wa kike wa kwao usimpe mwanao wa kiume.[#2 Mose 23:32; 34:15-16.]
4Kwani ataugeuza moyo wa mwanao, aache kunifuata, watumikie miungu mingine; ndipo, makali ya Bwana yatakapokuwakia, akuangamize upesi.
5Ila mwafanyizie hivyo: pao pa kutambikia sharti mpabomoe, nazo nguzo zao za mawe za kutambikia mzivunje, nayo miti yao ya Ashera mwikate, navyo vinyago vyao vya kuchongwa mviteketeze kwa moto.[#5 Mose 12:2-3.]
6Kwani wewe ndiwe kabila takatifu la Bwana Mungu wako; wewe Bwana Mungu wako alikuchagua katika makabila yote yaliyoko huku nchini, uwe kabila lake mwenyewe.[#2 Mose 19:5-6.]
7Bwana hakushikamana nanyi na kuwachagua, kwa kuwa m wengi kuliko makabila mengine, kwani mlikuwa wachache kuliko makabila yote,[#Ef. 2:8.]
8ila kwa kuwa Bwana aliwapenda ninyi, akataka kukitimiza kiapo, alichowaapia baba zenu, kwa hiyo Bwana aliwatoa ninyi kwa mkono wake wenye nguvu, akawakomboa mkononi mwa Farao, mfalme wa Misri, na kuwatoa nyumbani, mlimokuwa watumwa.
9Kwa hiyo jua, ya kuwa Bwana Mungu wako ni Mungu kweli, ni Mungu mwelekevu anayeyatimiza maagano na magawio kwao wampendao na kuyashika maagizo yake, akifikishe hata kizazi cha maelfu.[#2 Mose 20:6.]
10Lakini wao wamchukiao huwalipisha waziwazi na kuwaangamiza, hakawii kumlipisha waziwazi amchukiaye.
11Kwa hiyo yaangalieni maagizo na maongozi na maamuzi, mimi ninayokuagiza leo kuyafanya.[#5 Mose 5:32; 6:17.]
12Itakuwa, mtakapoyasikia haya maamuzi na kuyaangalia, myafanye, naye Bwana Mungu wako atakutimilizia maagano na magawio, aliyowaapia baba zako.[#2 Mose 23:22-31.]
13Ndipo, atakapokupenda, akubariki na kukufanya kuwa wengi, ayabariki nayo mazao ya tumbo lako nayo mazao ya shamba lako, ngano zako na mvinyo zako mbichi na mafuta yako na ndama wako na wana kondoo wako, watakaozaliwa katika nchi hiyo, Bwana aliyowaapia baba zako kukupa.
14Utakuwa umebarikiwa kuliko makabila yote, hatakuwa kwako mtu, wala mume, wala mke asiyezaa, nao nyama wenu wa kufuga watakuwa vivyo hivyo.
15Nao ugonjwa wote Bwana atauondoa kwako, hata hayo maradhi mabaya ya Misri, unayoyajua, atayazuia kwako, atayafikisha tu kwao wote wakuchukiao.
16Nayo makabila yote, Bwana Mungu wako atakayokupa, uyale, usiyaonee huruma kabisa, wala usiitumikie miungu yao, kwani hii itakuwa tanzi la kukunasa.[#Yos. 23:13.]
17Napo, utakaposema moyoni mwako: Mataifa haya ni mengi ya kunishinda, nitawezaje kuyafukuza?[#4 Mose 13:31; 14:1-4.]
18Usiwaogope, ila yakumbuke sana, Bwana Mungu wako aliyomfanyizia Farao nao Wamisri wote.
19Yakumbuke hayo majaribu makuu, macho yako yaliyoyaona, navyo vielekezo na vioja, nacho kiganja chake chenye nguvu, nao mkono, Bwana Mungu wako alioukunjua alipokutoa. Hivyo ndivyo, Bwana Mungu wako atakavyoyafanyizia makabila yote, wewe unayoyaogopa.[#5 Mose 4:34.]
20Tena Bwana Mungu wako atatuma mavu kwao, waangamie nao watakaosalia kwa kujificha, usiwaone.[#2 Mose 23:28-30.]
21Usiwastuke! Kwani Bwana Mungu wako yuko katikati yako, naye ni Mungu mkubwa anayeogopesha.
22Yeye Bwana Mungu wako atayang'oa hayo mataifa mbele yako moja kwa moja, kwani hutaweza kuwamaliza upesi, nyama wa porini wasizidi kuwa wengi kwako.
23Bwana Mungu wako atawatoa mbele yako na kuwahangaisha mahangaiko makubwa, hata waishe kuangamizwa.
24Nao wafalme wao atawatia mikononi mwako, nawe sharti uyatoweshe majina yao chini ya mbingu; hakuna atakayeweza kusimama mbele yako, mpaka uwaangamize.
25Vinyago vya miungu yao vya kuchongwa sharti mviteketeze kwa moto, usitamani kuzichukua fedha na dhahabu vilizotiwa, usinaswe nazo, kwani zinamchukiza Bwana Mungu wako.
26Wala usiingize nyumbani mwako machukizo kama hayo, usitiwe nawe mwiko wa kuwapo kama wao, ila na yakuchukize kabisa na kukutapisha kwa kuwa yenye mwiko.[#Yos. 7:11.]