5 Mose 8

5 Mose 8

Waisiraeli wanahimizwa kumshukuru Mungu.

1Maagizo yote, mimi ninayokuagiza leo, sharti myaangalie, myafanye, mpate kupona na kuwa wengi na kuiingia hiyo nchi, Bwana aliyowaapia baba zenu, mwichukue, iwe yenu.[#5 Mose 13:3; Amu. 2:22.]

2Zikumbuke njia zote, Bwana Mungu wako alizokuendesha nyikani hii miaka 40, akunyenyekeze na kukujaribu, ayajue yaliyomo moyoni mwako, kama utayaangalia maagizo yake, au kama utayakataa.

3Akakunyenyekeza na kukutia njaa, lakini kisha akakulisha Mana, usizozijua wewe, wala baba zako hawakuzijua, akajulisha, ya kama mtu hataishi kwa chakula tu, ila kwa kila neno linalotoka kinywani mwa Bwana.[#2 Mose 16:13-15; Mat. 4:4.]

4Nguo zako hazikuchakaa mwilini pako, wala miguu yako haikuvimba hii miaka 40.[#5 Mose 29:5.]

5Hapo ujue moyoni mwako, ya kuwa Bwana Mungu wako anakuchapa, kama mtu anavyomchapa mwanawe.[#5 Mose 1:31.]

6Kwa hiyo yaangalie maagizo ya Bwana Mungu wako, upate kuzishika njia zake na kumcha.

7Kwani Bwana Mungu wako ndiye atakayekuingiza katika nchi hiyo njema iliyo nchi yenye vijito na visima na viziwa vya maji yatokeayo mabondeni na vilimani.

8Ni nchi yenye ngano na mawele na mizabibu na mikuyu na mikomamanga, ni nchi yenye michekele iletayo mafuta, nazo asali ziko.

9Ni nchi, utakakokula chakula na kushiba sana, kwani hutakosa cho chote; ni nchi yenye mawe ya chuma, nazo shaba utazichimbua ndani ya milima yake.

10Kwa hiyo utakapokula na kushiba sharti umtukuze Bwana Mungu wako kwa ajili ya nchi hiyo njema, aliyokupa.

11Jiangalie, usimsahau Bwana Mungu wako, ukiacha kuyaangalia maagizo yake na maamuzi yake na maongozi yake, mimi ninayokuagiza leo.

12Hapo, utakapokula na kushiba, tena utakapojenga nyumba nzuri na kukaa humo,

13tena ng'ombe na mbuzi na kondoo wako watakapokuwa wengi, nazo fedha na dhahabu zako zitakapokuwa nyingi, nazo mali zako zote zitakapokuwa nyingi,

14jiangalie, moyo wako usijikuze, ukamsahau Bwana Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri nyumbani, mlimokuwa watumwa!

15Naye ndiye aliyekuongoza katika ile nyika kubwa inayoogopesha sana kwa nyoka za moto na kwa nge walioko na kwa kiu iliyoko nyingi, kwa kuwa hakuna maji; lakini yeye alikutolea maji katika mwamba mgumu sana.[#4 Mose 21:6; 2 Mose 17:6.]

16Akakulisha nyikani Mana, baba zako wasizozijua, akunyenyekeze na kukujaribu, apate kukufanyizia mema, yawe ya mwisho ya kukupa.

17kama sivyo, ungalisema moyoni mwako: Nguvu zangu na uwezo wa mikono yangu ndizo zilizonipatia mali hizi.

18Mkumbuke Bwana Mungu wako, kwani yeye ndiye anayekupa nguvu za kujipatia mali, alishikize Agano lake, alilowaapia baba zako, kama inavyoelekea leo.[#5 Mose 4:31.]

19Lakini itakapokuwa, umsahau Bwana Mungu wako na kufuata miungu mingine, uitumikie na kuitambikia, ninawashuhudia leo, ya kuwa mtaangamia kabisa.

20Kama Bwana alivyoyaangamiza yale mataifa mbele yenu, ndivyo, mtakavyoangamia nanyi, kwa kuwa hamkuisikiliza sauti ya Bwana Mungu wenu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania