Mpiga mbiu 12

Mpiga mbiu 12

Mkumbuke Mungu katika ujana, akutulize moyo katika uzee!

1Mkumbuke Muumbaji wako ukingali kijana bado, siku mbaya zikiwa hazijafika, wala miaka haijakupata bado, unayoisema: Hii sipendezwi nayo!

2Jua na mchana na mwezi na nyota zikiwa hazijaguiwa bado na giza, mawingu mengine yakitokea, mvua ikiisha kupita:

3siku hizo walinda nyumba watatetemeka, nao waume wenye nguvu watapindika, nao wanawake wasagao watakomesha kazi kwa kuwa wachache, nao wake waliochungulia madirishani wataguiwa na giza.

4Nayo milango ielekeayo njiani itafungwa, nacho kishindo cha mawe ya kusagia kitakuwa kidogo; ndipo, watu watakapoamka, jogoo akiwika, nao waimbaji wote wa kike watazipunguza sauti zao.

5Ndipo, watu watakapoogopa kupanda juu, nako njiani wataona mastusho; ni siku zile, mlozi unapochanua maua, mapanzi wasipoweza kuruka kwa kushiba, nacho kiungo cha pilipili kisipofaa kitu; kwani hapo mtu huiendea nyumba yake, atakamokaa kale na kale, nao waombolezaji humjia mara kwa mara.

6Kwani siku ziko karibu, kamba ya fedha itakapokatika, chano cha dhahabu kitakapopondeka, mtungi utakapovunjika kisimani, gurudumu la kutekea maji litakapokatika na kuangukia mlemle shimoni.

7Ndipo, nalo vumbi litakaporudi mchangani, lilikokuwa, nayo roho itarudi kwake Mungu aliyeitoa.[#Mbiu. 3:20; 1 Mose 3:19; Mbiu. 1:2.]

8Mpiga mbiu asema: Yote ni ya bure kabisa, yote pia ni ya bure.

Kumcha Mungu huyapita yote mengine.

9Jingine ni hili: huyu mpiga mbiu hakuwa mwerevu wa kweli yeye tu, ila nao watu aliwafundisha ujuzi, akawa mwenye mawazo makuu ya kuchunguza mambo, akatunga mafumbo mengi.[#1 Fal. 4:32.]

10Yeye mpiga mbiu alitafuta, aone maneno yapendezayo; nayo maneno yaliyokuwa ya kweli, yaliyoongoka, yakaandikwa.

11Maneno ya werevu wa kweli ni kama fimbo za wachungaji au kama misumari iliyopigiliwa vema; wenye kuyakusanya waliyapata kwa mchungaji mmoja.[#Ebr. 4:12.]

12Jingine lililoko ni hili: onyeka, mwanangu, usijitie katika kazi hiyo! Kutengeneza vitabu ni kwingi mno, hakukomi, nako kujifunza mengi huchokesha mwili.

13Na tusikie neno linaloyachanganya yote: Mche Mungu na kuyaangalia maagizo yake! Kwani hivi ndivyo vinavyompasa kila mtu.[#1 Tim. 1:5.]

14Kwani matendo yote Mungu atayatakia shauri, nayo yaliyofichwa, kama ni mema, au kama ni mabaya.[#Rom. 2:16; 1 Kor. 4:5.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania