The chat will start when you send the first message.
1Nilipoyatazama tena makorofi yanayofanywa chini ya jua, niliona machozi yao waliokorofishwa, lakini sikuona aliyewatuliza mioyo; namo mikononi mwao waliowakorofisha zimo nguvu, kwa hiyo kwao hakuna atakayewatuliza mioyo.
2Kwa sababu hii nikawawazia wafu waliokufa kale kuwa wenye shangwe kuliko wao wanaoishi bado wenye maisha.[#Iy. 3:11.]
3Lakini niliyemwazia kuwa amepata mema kuliko wao wote wawili, ni yule asiyepata bado kuzaliwa, kwa kuwa hakuyaona hayo matendo mabaya yanayofanywa chini ya jua.[#Mbiu. 6:3.]
4Tena niliona, ya kuwa masumbuko yote na kufanikiwa kote katika kazi hutoka katika wivu, mtu anaomwonea mwenziwe; hayo nayo ni ya bure na kuukimbilia upepo.
5Mjinga hukaa na kuifunga mikono yake; basi, hujila mwenyewe.[#Fano. 6:10.]
6Kiganja kimoja kikijaa matulivu ni vema kuliko magao yote mawili yakijaa masumbufu ya kuukimbilia upepo.[#Fano. 15:16.]
7Nikatazama na mengine yaliyo ya bure chini ya jua:[#Mbiu. 2:12.]
8kama mtu yuko peke yake pasipo mwenziwe wa pili wala mwana wala ndugu, hakomi kabisa kujisumbua, wala jicho lake halishibi kuzitazama mali, naye husema: Mimi ninamsumbukia nani na kujinyima mwenyewe mema yote? Basi, hayo nayo ni ya bure na utumishi mbaya.
9Kuwa wawili kunafaa kuliko kuwa mmoja tu, kwa kuwa hao hupata mshahara mwema wa masumbuko yao.
10Kwani wakianguka, mmoja humwinua mwenziwe lakini mtu aliye peke yake akianguka, ni vibaya, maana hana mwenziwe wa kumwinua.
11Tena wawili wakilala pamoja hutiana jasho; lakini aliye peke yake atawezaje kupata jasho?
12Tena aliye peke yake mtu humshinda, lakini wawili wataweza kusimama mbele yake. Nayo kamba yenye nyuzi tatu haikatiki upesi.
13Kijana mkiwa mwenye werevu wa kweli ni mwema kuliko mfalme mzee, akiwa mjinga asiyejua kuonyeka tena.
14Kwani itakuwa, yule atoke kifungoni, apate ufalme, naye aliyezaliwa katika ufalme wake awe mkiwa.[#1 Mose 41:14.]
15Nikawaona wote walioishi na kutembea chini ya jua, wakirudi upande wa huyo kijana wa pili aliyesimama mahali pake yule.
16Nao watu wote, aliowaongoza wote pia, hawakuhesabika. Lakini watakaokuwako nyuma yake hawatamfurahia. Kwa hiyo nayo yalikuwa ya bure na kuukimbilia upepo.[#Mbiu. 1:14.]