Esteri 2

Esteri 2

Esteri anapata utukufu wa kifalme.

1Baada ya mambo hayo, makali ya mfalme Ahaswerosi yalipotulia, akamkumbuka Wasti nayo, aliyoyafanya, nalo shauri, alilokatiwa.

2Ndipo, vijana wa mfalme waliomtumikia waliposema: Watu na wamtafutie mfalme vijana wa kike, walio wanawali wenye sura nzuri!

3Mfalme na aweke wasimamizi katika majimbo yote ya ufalme wake, wawakusanye vijana wa kike wote walio wanawali wenye sura nzuri, wawapeleke Susani jumbani mwa mfalme na kuwatia chumbani mwa wanawake mkononi mwake Hegai aliye mtumishi wa mfalme wa nyumbani wa kuwaangalia wanawake, kisha wapewe vyombo vyao vya kutengenezea uzuri.

4Naye kijana atakayempendeza mfalme na awe mkewe mfalme mahali pa wasti. Neno hili likampendeza mfalme, akafanya hivyo.

5Mle Susani, mlimokuwa wa jumba la mfalme, mlikuwa na mtu wa Kiyuda, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi, mwana wa Simei, mwana wa Kisi, wa mlango wa Benyamini.[#1 Sam. 14:51.]

6Alitekwa Yerusalemu, akahamishwa pamoja na mateka waliohamishwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; naye aliyewahamisha alikuwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli.[#2 Fal. 24:15-16.]

7Yule alikuwa akimlea Hadasa (Kihagilo), ndiye Esteri (Nyota), binti wa mjomba wake, kwa sababu hakuwa na baba wala na mama. Huyu kijana wa kike alikuwa mwenye uso upendezao na mwenye mwili mzuri. Baba yake na mama yake walipokufa, Mordekai alimchukua, awe mwanawe.[#Est. 2:15.]

8Ikawa, agizo la mfalme, aliloliamrisha, lilipotangazwa, vijana wengi wa kike wakakusanywa Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme, wakatiwa mkononi mwake Hegai; ndipo, Esteri naye alipochukuliwa na kupelekwa nyumbani mwa mfalme, akatiwa mikononi mwa Hegai aliyewaangalia wanawake.

9Akamwona kijana huyu kuwa mzuri, akampendeza sana, kwa hiyo akajihimiza kumpa vyombo vyake vya kutengenezea uzuri na posho yake; kisha akampa vijana wa kike saba waliochaguliwa nyumbani mwa mfalme, akamkalisha pamoja na hao vijana wake nyumbani mwa wanawake katika chumba kilichokuwa kizuri zaidi.

10Lakini Esteri kakuujulisha ukoo wake wala mlango wake, kwa kuwa Mordekai alimkataza, asiujulishe.

11Naye Mordekai akatembea siku kwa siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ajue, kama Esteri hajambo, tena ayajue nayo yatakayompata.

12Siku zilipotimia, hao vijana wakapelekwa mmoja mmoja kwa mfalme Ahaswerosi; vikafanyika, walipokwisha kukaa huko miezi kumi na miwili na kuyafuata maongozi ya wanawake. Kwani hapo ndipo, zilipotimia siku za kutakaswa kwao: miezi sita walipakwa kwa mafuta ya manemane, miezi sita mingine kwa manukato mengine, wanawake waliyoyatumia ya kutengenezea uzuri.

13Basi, hayo yalipokwisha, kila mara kijana alipoingia kwa mfalme hupewa yote, aliyoyataka kwenda nayo kutoka mle nyumbani mwa wanawake kuingia nyumbani mwa mfalme.

14Huenda jioni, tena hurudi asubuhi kukaa katika nyumba ya pili ya wanawake mkononi mwa Sasagazi, mtumishi wa nyumbani mwa mfalme aliyewaangalia masuria; haingii tena kwa mfalme, isipokuwa mfalme amependezwa naye, akaagiza, aitwe kwa jina lake.

15Basi, ikatimia hata siku yake Esteri, mwana wa Abihaili, mjomba wake Mordekai aliyemchukua, awe mwanawe. Alipoingia kwa mfalme hakutaka kitu, ni vile tu, Hegai, mtumishi wa nyumbani mwa mfalme aliyewaangalia wanawake, alivyomwambia, aende navyo. Naye Esteri alikuwa anawapendeza wote waliomwona kwa macho yao.

16Huyu Esteri akapelekwa kwa mfalme Ahaswerosi nyumbani mwake mwa kifalme katika mwezi wa kumi, ndio mwezi wa Tebeti katika mwaka wa saba wa kutawala kwake.

17Mfalme akampenda Esteri kuliko wanawake wote, kwani aliona upendeleo na utu mbele yake kuliko wanawali wote, akamvika kilemba cha kifalme kichwani pake, akamweka kuwa mkewe mahali pa Wasti.

18Kisha mfalme akawafanyizia wakuu na watumishi wake wote karamu kubwa, ndio karamu ya Esteri. Tena akayapunguzia majimbo yake kodi, nao watu akawapa matunzo, kama inavyompasa mfalme.

19Walipokusanywa wanawali mara ya pili, Mordekai alikuwa akikaa langoni pa mfalme.

20Lakini Esteri alikuwa hajaujulisha mlango wake wala ukoo wake, kama Mordekai alivyomwagiza; kwani Esteri aliyafanya maagizo yake Mordekai kama hapo, alipomlea.[#Est. 2:10.]

Mordekai anavumbua njama ya kumwua mfalme.

21Siku zile, Mordekai alipokaa langoni pa mfalme, watumishi wawili wa mfalme wa nyumbani waliokuwa walinda mlango, ndio Bigitana na Teresi, wakakasirika sana, wakatafuta njia ya kumwua mfalme Ahaswerosi kwa mikono yao.

22Mordekai akapata kulijua shauri hilo, akamsimulia Esteri, mkewe mfalme, naye Esteri akamwambia mfalme katika jina la Mordekai.

23Kisha shauri hilo likanyatiwa, hata likavumbulikana, nao wale wawili wakatundikwa katika mti. Mambo haya yakaandikwa katika kitabu cha mambo ya siku machoni pa mfalme.[#Est. 6:1-2.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania