The chat will start when you send the first message.
1Katika mwezi wa tatu tangu hapo, wana wa Isiraeli walipotoka katika nchi ya Misri, siku hiyohiyo wakafika nyikani kwa Sinai.
2Walipoondoka Refidimu, wakafika nyikani kwa Sinai; nao Waisiraeli wlipoyapiga makambi yao wakayapiga ng'ambo ya huku kwenye huo mlima.
3Naye Mose akaupanda huo mlima kwenda kwake Mungu, Bwana alipomwita huko mlimani, akamwambia: Hivi ndivyo, utakavyowaambia wao wa mlango wa Yakobo na kuwatangazia wana wa Isiraeli:
4Ninyi mmeyaona niliyowafanyizia Wamisri, nikawachukua ninyi, kama tai anavyowachukua watoto wake mabawani, nikawafikisha kwangu.[#5 Mose 32:11.]
5Sasa mtakapoisikia sauti yangu na kuliangalia Agano langu, mtakuwa watu wangu mwenyewe kuliko makabila yote ya watu, kwani ulimwengu wote ni wangu.[#5 Mose 7:6.]
6Ninyi mtakuwa ufalme wangu wenye watambikaji na taifa takatifu. Haya ndiyo maneno, utakayowaambia wana wa Isiraeli.[#3 Mose 19:2; 1 Petr. 2:9; Ufu. 1:6.]
7Mose aliporudi akawaita wazee wao hawa watu, akawaeleza haya maneno yote, Bwana aliyomwagiza.
8Watu wote wakaitikia pamoja kwamba: Yote, Bwana aliyoyasema, tutayafanya. Naye Mose akampelekea Bwana majibu haya ya watu;
9Bwana naye akamwambia Mose: Utaniona mimi, nikikujia katika wingu jeusi, hawa watu wasikie, nikisema na wewe, wakutegemee nawe kale na kale. Kisha Mose akamsimulia Bwana maneno yote ya watu.
10Kisha Bwana akamwambia Mose: Nenda kwao hawa watu, uwaeue leo na kesho, wazifue nazo nguo zao,
11wawe tayari siku ya tatu! Kwani hiyo siku ya tatu Bwana atashuka machoni pao watu wote kufika juu ya mlima wa Sinai.
12Tena uwakatie hawa watu mpaka wa kuuzunguka mlima na kuwaambia: Jiangalieni, msiupande mlima huu, wala msiuguse hapo chini yake! Kwani kila atakayeugusa mlima huu atakufa;[#2 Mose 34:3.]
13lakini mkono wa mwingine usimguse mtu huyo, ila auawe kwa kupigwa mawe au kwa kuchomwa mikuki, kama ni mtu au nyama, asiwepo tena! Lakini hapo, panda lenye mlio mrefu litakapopigwa, ndipo wao nao na waupande mlima huu![#Ebr. 12:18-20.]
14Kisha Mose akatelemka huko mlimani kwenda kwao hao watu, akawaeua watu, wakazifua nguo zao.
15Tena akawaambia: Msiwakaribie wake zenu, mpate kuwa tayari siku ya tatu![#1 Kor. 7:5.]
16Siku ya tatu ilipofika, ilipokuwa asubuhi, zikasikilika ngurumo, nao umeme ukapiga, nako mlimani juu kukawa na wingu jeusi, nao mlio wa baragumu lenye nguvu ukasikilika, nao watu wote waliokuwa makambini wakatetemeka.[#Ebr. 12:21.]
17Ndipo, Mose alipowatoa watu makambini, waje kukutana na Mungu, wakajipanga mlimani chini.
18Lakini mlima wote wa Sinai ulitoka moshi, kwa kuwa Bwana aliutelemkia kwa moto, nao moshi wake ukapanda, kama moshi wa tanuru, nao mlima wote ukatetemeka sana,
19nao mlio wa lile baragumu ukaendelea, ukazidi sana. Mose akasema, naye Mungu akamwitikia na kupaza sauti.[#Tume. 7:38.]
20Bwana alipokwisha kushuka huko kwenye mlima wa sinai na kufika kileleni juu ya mlima huu, Bwana akamwita Mose kufika kileleni juu ya mlima huu, naye Mose akapanda.
21Ndipo, Bwana alipomwambia Mose: Shuka, uwaonye hawa watu, wasijivunjie njia ya kufika kwa Bwana, wapate kumwona, wasife wengi miongoni mwao.
22Nao watambikaji watakaomkaribia Bwana, sharti wajieue, Bwana asije, akawaponda.
23Lakini Mose akamwambia Bwana: Hawa watu hawawezi kupanda mlimani kwa Sinai, kwani wewe mwenyewe umetuonya na kuniagiza kwamba: Kata mpaka wa mlima huu na kuueua, wasiuguse.
24Ndipo, Bwana alipomwambia: Nenda, ushuke! Kisha upande wewe, naye Haroni pamoja na wewe! Lakini watambikaji na watu wasijivunjie njia ya kupanda kwake Bwana, asije, akawaponda.
25Kisha Mose akatelemka kwenda kwao hao watu, akawaambia maneno hayo.