2 Mose 2

2 Mose 2

Kuzaliwa kwake Mose.

1Mtu wa mlango wa Lawi akaenda, akaoa mwanamke wa Kilawi.

2Huyo mwanamke akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume; naye alipomwona kuwa mtoto mzuri, akamficha miezi mitatu.[#2 Mose 6:20; Tume. 7:20; Ebr. 11:23.]

3Asipoweza kumficha tena, akamchukulia sanduku ya mafunjo, akayaziba kwa udongo wenye utomvu mweusi na kuyapata lami, akamweka mtoto humo ndani; kisha akaiweka hiyo sanduku katika manyasi kando ya mto mkubwa.

4Umbu lake mtoto akasimama mbali, aone yatakayompata.

Kukua kwake Mose nyumbani mwa Farao.

5Mara akatelemka binti Farao, aoge mtoni, vijakazi wake wakitembea kando ya jito. Yeye alipoiona hiyo sanduku katikati ya manyasi akatuma kijakazi wake mmoja kuichukua.

6Alipoifunua akamwona mtoto, naye huyu kitoto alikuwa akilia; naye akamhurumia, akasema: Ni mtoto wa Waebureo huyu.

7Ndipo, umbu lake mtoto alipomwuliza binti Farao: Niende kukuitia mnyonyeshaji wa Kiebureo, akunyonyeshee mtoto?

8Binti Farao akamwambia: Nenda! Ndipo, yule kijana wa kike alipokwenda, akamwita mamake mtoto.

9Naye binti Farao akamwambia: Mchukue huyu mtoto, uninyonyeshee! Nami nitakupa msahahara wako. Kisha huyo mwanamke akamchukua mtoto, akamnyonyesha.

10Mtoto alipokuwa mkubwa, akampeleka kwa binti Farao, naye akamwia mwanawe, akamwita jina lake Mose akisema: Kwani nilimtoa majini.

11Siku zile Mose alipokwisha kukua akatoka kwenda kwa ndugu zake; alipovitazama, walivyofanyishwa kazi ngumu, akaona Mmisri mmoja, akimpiga mmoja wao ndugu zake wa Kiebureo.[#Ebr. 11:24-25.]

12Ndipo, alipogeuka huko na huko, tena alipoona, ya kama hakuna mtu, akampiga yule Mmisri na kumwua, kisha akamfukia mchangani.[#Tume. 7:24.]

13Kesho yake alipotoka akaona, wawili wa Kiebureo wakipigana, akamwambia aliye mkorofi: Mbona unampiga mwenzako?

14Naye akajibu: Yuko nani aliyekuweka kuwa mkuu wa mwamuzi kwetu? Je? Wewe unataka kuniua nami, kama ulivyomwua yule Mmisri? Ndipo, Mose aliposhikwa na woga, akasema: Kumbe lile jambo limejulikana.[#Tume. 7:22-28,35.]

Kukimbia na kuoa kwake Mose.

15Farao alipolisikia neno hilo, akamtafuta Mose, amwue; lakini Mose akamkimbia Farao, asimwone, akaenda kukaa katika nchi ya Midiani, akakaa kwenye kisima.[#Ebr. 11:27.]

16Naye mtambikaji wa Midiani alikuwa na wana wa kike saba; hao walipokuja kuchota maji na kupajaza maji hapo, walipopatengeneza pa kunyweshea mbuzi na kondoo wa baba yao,[#2 Mose 3:1.]

17wakaja wachungaji wengine na kuwafukuza. Ndipo, Mose alipoinuka, akawasaidia akiwanywesha mbuzi na kondoo wao.[#1 Mose 29:10.]

18Walipofika kwa baba yao Reueli, akawauliza: Inakuwaje, mkifika leo, kukiwa mchana bado?

19Wakasema: Mtu wa Kimisri ametuponya mikononi mwa wale wachungaji, kisha akatuchotea maji, akawanywesha mbuzi na kondoo.

20Akawauliza wanawe: Yuko wapi? Mbona mmemwacha huko? Mwalikeni, ale nasi!

21Kisha Mose akapatana kukaa kwake yule mtu, akampa Mose mwanawe Sipora kuwa mkewe.

22Alipomzalia mtoto wa kiume, akamwita jina lake Gersomu (Mgeni wa Huku), kwani alisema: Nimekuwa mgeni katika nchi isiyo ya kwetu.[#2 Mose 18:3.]

Mungu anayasikia malalamiko ya Waisiraeli.

23Siku zilipopita nyingi, yule mfalme wa Misri akafa. Nao wana wa Isiraeli wakapiga kite pamoja na kulia kwa ajili ya utumwa wao, nayo hayo malalamiko yao yakapanda, yakafika kwake Mungu kwa ajili ya huo utumwa wao.[#2 Mose 3:7.]

24Mungu alipoyasikia hayo mauguzi yao, yeye Mungu akalikumbuka Agano lake, alilomwekea Aburahamu na Isaka na Yakobo.[#1 Mose 15:18; 26:3; 28:13-14.]

25Ndipo, Mungu alipowaonea machngu wana wa Isiraeli, kwani yeye Mungu aliwajua, walivyo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania