2 Mose 23

2 Mose 23

Maagizo ya upendo na mengine.

1Usivumishe habari za uwongo ukifanya bia na mwovu kuwa shahidi wa kukorofisha wengine.[#2 Mose 20:16.]

2Usiwe upande wao walio wengi, wakitaka kufanya mabaya. Wal shaurini usiwafuate walio wengi, ukimpotoa mwenzako.

3Wala usimpendelee mnyonge shaurini.[#3 Mose 19:15.]

4Ukikuta ng'ombe wa mchukivu wako au punda wake, akipotea, sharti umrudishe kwake.[#Luk. 6:27.]

5Ukimwona punda wa mchukivu wako, ya kuwa ameanguka kwa kulemewa na mzigo wake, usiwaache peke yao, ila yaache mambo yako, usaidiane navyo.

6Usilipotoe shauri la mwenzako aliye mkiwa, akipatwa na neno.[#5 Mose 27:19.]

7Jitenge kabisa nayo yaliyo ya uwongo! Usiue mtu asiyekora manza, aliye mwongofu! Kwani aliye mwovu sitamtokeza kuwa hakukosa.

8Usitwae mapenyezo! Kwani mapenyezo huyapofusha macho yao waonao, tena huyapotoa maneno ya waongofu.[#5 Mose 16:19; 27:25.]

9Wageni msiwakorofishe! Kwani wenyewe mnaijua mioyo ya wageni, ilivyo, kwani mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.[#2 Mose 22:21.]

10Miaka sita upande mbegu katika nchi yako na kuyavuna mapato yake![#3 Mose 25; 5 Mose 15:1-11.]

11Katika mwaka wa saba utaiacha tu, ipate kupumzika na kutulia; wakiwa walio wa ukoo wako na waile, nayo yatakayosalia na wayale nyama wa porini; vivyo hivyo uifanyizie nayo mizabibu yako na michekele yako!

12Siku sita na uzifanye kazi zako! Lakini siku ya saba sharti upumzike, ng'ombe wako na punda wako wapate kutulia, naye mwana wa kijakazi wako pamoja na mgeni wapate kupumzika.[#2 Mose 20:8-11.]

13Yote niliyowaambia yaangalieni! Majina ya miungu mingine msiyataje, yasisikiwe vinvywani mwenu![#Yos. 23:7.]

(14-19: 2 Mose 34:18-26; 3 Mose 23; 5 Mose 16.)

14Kila mwaka unifanyizie sikukuu mara tatu!

15Sikukuu ya Mikate isiyochachwa uiangalie: siku saba ule mikate isiyochachwa, kama nilivyokuagiza, nazo siku zake zilizowekwa ni za mwezi wa Abibu, kwani ndio, uliotoka Misri; lakini wasitokee mbele yangu mikono mitupu![#2 Mose 12:15.]

16Tena sikukuu ya Mavuno ya malimbuko ya kazi za kupanda shambani; tena mwisho wa mwaka sikukuu ya kukusanya, utakapoyakusanya shambani mapato ya kazi zako.

17Kila mwaka mara tatu waume wako wote sharti watokee mbele ya Bwana Mungu.

18Damu za ng'ombe zangu za tambiko usizitoe pamoja na mikate iliyochachwa! Wala mafuta ya sikukuu yangu yasilale usiku kucha![#2 Mose 12:10.]

19Malimbuko ya kwanza ya shamba lako sharti uyapeleke Nyumbani mwa Bwana Mungu wako! Kitoto cha mbuzi usikipike katika maziwa ya mama yake.[#5 Mose 26:1-11; 14:21; 2 Mose 22:29.]

Kiagio cha kuwafukuza Wakanaani mbele ya Waisiraeli.

20Utaniona, nikimtuma malaika wangu, akutangulie na kukuangalia njiani, akufikishe mahali pale, nilipokutengenezea.[#2 Mose 14:19.]

21Jiangalieni hapo, alipo, uisikilize sauti yake, usimchokoze! Kwani hatawaondolea makosa yenu mabaya, nalo Jina langu limo mwake.[#Yes. 63:9-10.]

22lakini ukiisikiliza vema sauti yake, uyafanye yote, nitakayoyasema, mimi nitakuwa adui yao adui zako, niwasonge wakusongao.

23Kwani malaika wangu atakutangulia, akufikishe kwao Waamori na Wahiti na Waperizi na Wakanaani na Wahiwi na Wayebusi, nami nitawatowesha.

24Usiiangukie miungu yao, wala usiitumikie, wala usiyafanye, wao wanayoyafanya, ila mziangushe na kuzivunja kabisa nguzo zao za kutambikia.[#2 Mose 20:5; 3 Mose 18:3.]

25Mtumikieni Bwana Mungu wenu! Ndipo, atakapokibariki chakula chako na maji yako, hata magonjwa yote nitayaondoa kwako.[#2 Mose 15:26.]

26Katika nchi yako hatakuwako mwanamke mwenye kuharibu mimba au mgumba, nayo hesabu ya siku zako za kuwapo nitaitimiza yote.

27Mbele yako nitayatanguliza mastusho yangu ya kuzimiza roho za watu wote, utakaowafikia; hivyo nitafanya adui zako wote wakuonyeshe visogo vyao.

28Nitatanguliza mavu mbele yako, niwafukuze Wahiwi na Wakanaani na Wahiti mbele yako.[#5 Mose 1:44; 7:20.]

29Lakini sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja, nchi isiwe mapori matupu, wala nyama wa porini wasiwe wengi, wakakusumbua.[#Yos. 24:12.]

30Ila nitawafukuza mbele yako kidogo kidogo, hata mtakapokuwa wengi wa kuichukua hiyo nchi, iwe yenu.

31Nami nitakukatia mipaka kutoka kwenye Bahari kwenda kwenye bahari ya Wafilisti, tena kutoka nyikani kwenda hata kwenye lile jito kubwa, kwani wenyeji wa nchi hiyo nitawatia mikononi mwenu, uwafukuze mbele yako.[#1 Mose 15:18.]

32Lakini usifanye agano wala nao wenyewe, wala na miungu yao![#5 Mose 7:2.]

33Wasikae katika nchi yako, wasikukoseshe, unikosee mimi; lakini utakapoitumikia miungu yao, itakuwia tanzi.[#Amu. 2:3.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania