The chat will start when you send the first message.
1Wewe mchukue kaka yako Haroni pamoja na wanawe, uwafikishe kwako ukiwatoa katikati ya wana wa Isiraeli kuwa watambikaji wangu, yeye Haroni na Nadabu na Abihu na Elazari na Itamari, wanawe Haroni.[#1 Mambo 23:13; 2 Mose 6:23.]
2Umtengenezee kaka yako Haroni mavazi matakatifu ya kumpatia macheo na utukufu.
3Wewe sema nao walio werevu wa kweli mioyoni mwao, niliowapa roho yenye werevu mwingi ulio wa kweli, wamtengenezee Haroni mavazi ya kumweulia, apate kuwa mtambikaji wangu.[#2 Mose 31:3.]
4Nayo mavazi, watakayomfanyizia, ni haya: kibati cha kifuani na kisibau na kanzu na shati ya nguo ya kunguru na kilemba na mshipi. Haya mavazi matakatifu na wamtengenezee kaka yako Haroni, hata wanawe, wawe watambikaji wangu.
5Nao wale mafundi na watumie nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta.
6Kwa kukitengeneza kisibau na watumie dhahabu na nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na nguo za bafta ngumu, kiwe kazi ya ufundi wa kweli.
7Kiwe chenye vipande viwili vinavyounganika mabegani, penye ncha zake mbili ndipo kifungike.
8Nayo masombo yake ya kukifunga kifuani pake yawe ya kazi iyo hiyo. Yatengenezwe kwa dhahabu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu.
9Kisha uchukue vito viwili vya oniki, uchore humo majina ya wana wa Isiraeli.
10Majina yao sita katika kito kimoja, nayo yale majina sita yaliyosalia katika kito cha pili, kama walivyofuatana kuzaliwa.
11Kazi hii ya kuchora katika kito na uifanyishe mafundi wanaojua kuchora muhuri. Ndivyo, utakavyoyachora majina ya wanawe Isiraeli katika hivyo vito viwili; kisha uvizungushie vikingo vya dhahabu vya kuvishika.
12Kisha hivi vito viwili utavibandika penye vile vipande viwili vya mabegani vya kisibau kuwa vito vya kumkumbushia wana wa Isiraeli; hivyo ndivyo, Haroni atakavyoyachukua majina yao juu ya mabega yake mawili mbele ya Bwana, ayakumbuke.
13Kisha utengeneze nguo zilizofumwa kwa nyuzi za dhahabu tu.
14Tena tengeneza vikufu viwili vya dhahabu tupu vinavyofanana na kamba nyembamba kwa kuwa kama kamba zilizosokotwa. Kisha hivi vikufu vinavyofanana na kamba uvitie penye zile nguo zilizofumwa kwa nyuzi za dhahabu tu.
15Kisha kitengeneze kibati cha maamuzi cha kifuani, nacho kiwe kazi ya ufundi wa kweli. Ukitengeneze kuwa kazi nzuri kama ile ya kisibau, ukitumia kwa kukitengeneza dhahabu na nguo za kifame nyeusi na nyekundu na nguo za bafta ngumu.
16Pande zake zote ziwe sawasawa, tena kiwe kimekunjwa kuwa kuwili, urefu wake uwe shibiri, nao upana, wake uwe shibiri.
17Ukijaze vito na kuviweka kuwa mistari minne ya vito ya kukijaza chote. Mstari wa kwanza: sardio, topazio na sumarato, ndio mstari wa kwanza.
18Mstari wa pili: almasi nyekundu, safiro na yaspi;
19mstari wa tatu: hiakinto, akate na ametisto;
20mstari wa nne: krisolito, oniki na berilo. Vitakapotiwa viwe vimezungushiwa vyote vikingo vya dhahabu vya kuvishika.
21Kwa hesabu ya majina ya wanawe Isiraeli viwe kumi na viwili vikiyafuata hayo majina yao, kila kimoja chao kipate jina lake moja katika hayo mashina kumi na mawili, likichorwa humo, kama kazi ya muhuri ilivyo.
22Tena utengeneze kwa dhahabu tupu vikufu vinavyofanana na kamba zilizosokotwa vya kutia penye kibati cha kifuani.
23Kisha utengeneze pete mbili kwa dhahabu za kutia penye kibati cha kifuani, kisha uzitie hizo pete mbili penye zile ncha mbili za juu za kibati cha kifuani.
24Kisha hivyo vikufu vya dhahabu vinavyofanana na kamba uvifunge katika hizo pete mbili, ulizozitia katika ncha za juu za kibati cha kifuani.
25Kisha hiyo miisho mingine miwili ya hivi vikufu viwili vinavyofanana na kamba uifunge katika vile vikingo viwili vya dhahabu, kisha uvifunge penye vipande vya mabegani vya kisibau upande wake wa mbele.
26Kisha utengeneze tena pete mbili za dhahabu, uzitie penye zile ncha mbili za chini za kibati cha kifuani katika ukingo wake ulioko upande wa ndani unaokielekea kisibau.
27Kisha utengeneze tena pete mbili za dhahabu, uzitie katika vipande vile viwili vya mabegani vya kisibau chini upande wake wa mbele papo hapo, vile vipande vinapounganika, juu ya masombo ya kisibau.
28Kisha na wakifunge kibati cha kifuani kwa kamba ya nguo nyeusi ya kifalme, wakiitia katika pete zake, tena katika pete za kisibau, kibati cha kifuani kipate kukaa juu ya masombo ya kisibau, kisiweze kusogeasogea hapo pake penye kisibau.
29Hivyo ndivyo, Haroni atakavyoyachukua majina ya wanawe Isiraeli katika kibati cha maamuzi cha kifuani juu ya moyo wake atakapoingia Patakatifu, yakumbukwe usoni pa Bwana siku zote.
30Tena utie katika kibati cha maamuzi cha kifuani Urimu na Tumimu (Mwanga na Kweli), ziwe juu ya moyo wake Haroni, atakapotokea usoni pa Bwana. Ndivyo, Haroni atakavyoyachukua maamuzi ya wana wa Isiraeli juu ya moyo wake usoni pa Bwana.[#3 Mose 8:8; 4 Mose 27:21; 5 Mose 33:8; 1 Sam. 28:6.]
31Kanzu ikipasayo hicho kisibau uitengeneze yote nzima kwa nguo nyeusi ya kifalme.
32Upande wake wa kichwani iwe na tundu katikati; hili tundu lizungukwe na taraza iliyotengenezwa na mfuma nguo; hili tundu lake liwe kama tundu la shati ya chuma ya mpiga vita, isipasuke.
33Penye upindo wake wa chini utatia komamanga za nguo za kifalme nyeusi na nyekundu kuuzunguka upindo wake wa chini po pote, tena katikati yao utie po pote vikengele vidogo vya dhahabu,
34viwe hivyo: kikengele cha dhahabu na komamanga, tena kikengele cha dhahabu na komamanga, vivyo hivyo po pote kuuzunguka upindo wote wa chini wa kanzu.
35Naye Haroni sharti aivae akitumika, milio yake isikilike, akiingia Patakatifu kutokea usoni pa Bwana, hata akitoka, asife.[#2 Mose 30:21; 3 Mose 16:2-13.]
36Kisha utengeneze bamba la dhahabu tupu la pajini, uchore humo kuwa ama machoro ya muhuri: Mtakatifu wa Bwana!
37Ulifunge kwa kamba ya nguo nyeusi ya kifalme katika kilemba, kiwe mbele ya kilemba.
38Na kiwe juu ya paji la Haroni, yeye Haroni azichukue manza, wana wa Isiraeli watakazozikora kwa ajili ya vipaji vyao vitakatifu, watakavyomtolea Mungu kuwa vipaji vyao vitakatifu. Na liwe juu ya paji lake siku zote kuwapatia upendeleo machoni pa Bwana.
39Tena na ufume shati ya bafta kuwa kama nguo ya kunguru, tena utengeneze kilemba cha nguo ya bafta, utengeneze nao mshipi, uwe kazi ya fundi ajuaye kufuma kwa nyuzi za rangi.
40Nao wana wa Haroni uwatengenezee shati, tena uwatengenezee mishipi, tena uwatengenezee vilemba virefu kuwapatia macheo na utukufu.
41Kisha umvike kaka yako Haroni mavazi hayo, hata wanawe, uwapake mafuta pamoja na kuwajaza magao yao, ukiwaeua, wapate kuwa watambikaji wangu.[#3 Mose 8:12; 2 Mose 29:9-24.]
42Watengenezee nazo suruali nyeupe za ukonge za kuzifunika nyama za miili zitiazo soni, zikitoka viunoni na kufika magotini.
43Haroni na wanawe sharti wazivae wakiingia katika Hema la Mkutano au wakiikaribia meza ya kutambikia pale Patakatifu, wasife kwa kukora manza. Maongozi haya yawe ya kale na kale kwake nako kwao wa uzao wake wajao nyuma yake.