2 Mose 29

2 Mose 29

Kuwaeua watambikaji.

(1-35: 3 Mose 8:1-32.)

1Hili ndilo jambo, utakalowafanyia, uwaeue kuwa watambikaji wangu: chukua dume la ng'ombe aliye kijana bado na madume mawili ya kondoo wasio na kilema,

2na mikate isiyochachwa na maandazi yasiyochachwa yaliyotiwa mafuta na maandazi membamba yasiyochachwa, yaliyopakwa mafuta juu tu; haya yote uyatengeneze kwa unga mwembamba wa ngano.

3Kisha yote uyatie katika kikapu kimoja, uyapeleke humo kikapuni pamoja na yule dume la ng'ombe na wale madume mawili ya kondoo.

4Kisha umfikishe Haroni pamoja na wanawe hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, uwaoshe kwa maji.

5Kisha yachukue hayo mavazi, umvike Haroni shati na kanzu na kisibau na kibati cha kifuani, kisha umfunge kisibau kwa masombo ya kisibau.

6Kisha umvike kilemba kichwani pake na kulitia lile bamba takatifu katika kilemba chake.[#2 Mose 28:36; 39:30.]

7Kisha chukua mafuta ya kumpaka, umpake na kuyamimina kichwani pake.[#2 Mose 30:25.]

8Kisha nao wanawe uwafikishe, uwavike shati;

9kisha uwafunge mishipi, yeye Haroni na wanawe, uwafunge vilemba virefu; ndipo, utambikaji utakapokuwa wao kwa hayo maongozi ya kale na kale. Kisha umjaze Haroni gao lake, nao wanawe uwajaze magao yao.[#2 Mose 29:2; 28:41.]

10Kisha umlete dume la ng'ombe, afike hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano; ndipo Haroni na wanawe wambandikie huyo dume la ng'ombe mikono yao kichwani pake.

11Kisha umchinje huyo dume la ng'ombe mbele ya Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.

12Kisha uchukue damu kidogo ya huyo dume la ng'ombe, uzipake pembe za meza ya kutambikia kwa kidole chako, nayo damu yote nyingine umwagie msingi wa meza ya kutambikia.

13Kisha yachukue mafuta yote yanayoufunika utumbo na kipande cha ini kilicho pamoja na mafigo yake mawili nayo mafuta yanayoshikamana nayo, uyachome moto hapo mezani pa kutambikia.[#2 Mose 29:22.]

14Lakini nyama zake huyo dume la ng'ombe na ngozi yake na mavi yake uyateketeze kwa moto nje ya makambi, maana ni ng'ombe ya tambiko ya weuo.[#3 Mose 4:11-12.]

15Kisha wale madume ya kondoo chukua mmoja, naye Haroni na wanawe na wambandikie huyo dume la kondoo mikono yao kichwani pake

16Kisha umchinje huyo dume la kondoo, nayo damu yake ichukue, uinyunyizie meza ya kutambikia pande zote.

17Kisha huyo dume la kondoo umchangue kuwa vipande viwili, kisha uuoshe utumbo wake na miguu yake, upate kuviweka juu y vile vipande vyake na juu ya kichwa chake.

18Huyo dume la kondoo wote umchome moto hapo mezani pa kutambikia kuwa ng'ombe ya tambiko ya Bwana ya kuteketezwa nzima, ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana.

19Kisha mchukue yule dume la kondoo wa pili, naye Haroni na wanawe na wambadikie huyo dume la kondoo mikono yao kichwani pake.

20Kisha umchinje huyo dume la kondoo, uchukue damu yake kidogo, uwapake Haroni na wanawe pembe za chini za masikio yao ya kuume na vidole gumba vya mikono yao ya kuume na vidole gumba vya miguu yao ya kuume, nayo damu nyingine uinyunyizie meza ya kutambikia pande zote.

21Kisha uchukue damu kidogo iliyoko mezani pa kutambikia na mafuta ya kupaka kidogo umnyunyizie Haroni na mavazi yake, kisha uwanyunyizie nao wanawe na mavazi ya wanawe; ndivyo, anavyoeuliwa yeye pamoja na mavazi yake, tena ndivyo, nao wanawe wanavyoeuliwa pamoja na mavazi yao.

22Kisha uyachukue mafuta ya huyo dume la kondoo ni mkia na mafuta yaliyoufunika utumbo na kile kipande cha ini na mafigo yake mawili pamoja na mafuta yanayoshikamana nayo na paja la kuume, maana ni dume la kondoo apasaye siku ya kujazwa gao.

23Uchukue tena katika kikapu cha mikate isiyochachwa kilichowekwa mbele ya Bwana mkate mmoja na andazi moja lililotiwa mafuta na andazi jembamba moja.[#3 Mose 3:3-4.]

24Haya yote uyaweke mikononi mwa Haroni namo mikononi mwa wanawe, uyapitishe motoni mbele ya Bwana.

25Kisha uyachukue mikoni mwao uyachome moto mezani pa kutambikia kuwa moshi juu ya ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa, hivyo yatakuwa mbele ya Bwana mnuko wa moto wa kumpendeza Bwana.

26Kisha uchukue kidari cha dume la kondoo la Haroni la kulijaza gao lake, ukipitishe mbele ya Bwana; kisha kitakuwa fungu lako.

27Ndivyo, utakavyokitakasa kidari kuwa kipaji cha tambiko cha kupitishwa motoni, hata paja kuwa kipaji cha tambiko cha kunyanyuliwa, maana kidari kilipitishwa motoni, nalo paja lilinyanyuliwa kuwa lake Bwana; nacho hicho kidari pamoja na hilo paja yalitoka kwa dume la kondoo wa Haroni na wa wanawe aliyetolewa kuyajaza magao yao.[#4 Mose 18:18.]

28Hii na iwe haki yao Haroni na wanawe ya kale na kale kuyapata kwa wana wa Isiraeli, kwani ndio vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa, na viwe vyao, wana wa Isiraeli watakapotoa ng'ombe za tambiko za shukrani, maana vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa ni vyake Bwana.

29Nayo mavazi matakatifu ya Haroni na yawe ya wwanawe, watakapomfuata, wayavae watakapopakwa mafuta ya kujazwa magao yao.[#2 Mose 29:9.]

30Mwanawe atakayepata utambikaji sharti ayavae siku saba, apate kuingia katika Hema la Mkutano na kutumikia Patakatifu.

31Lakini huyo dume la kondoo aliyetolewa kuwajaza magao sharti umchukue, uzitokose nyama zake mahali patakatifu.

32Naye Haroni na wanawe na wazile nyama zake huyu dume la kondoo pamoja na mikate iliyomo katika kikapu hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.

33Na wazile, kwa kuwa ndizo, walizopatiwa upozi nazo, wapate kujazwa magao pamoja na kueuliwa; lakini mgeni hana ruhusa kuzila, kwani ni takatifu.

34Kama ziko nyama zitakazosalia zilizokuwa za kuwajaza magao, au kama iko mikate itakayosalia mpaka kesho, sharti uyateketeze hayo masao kwa moto, yasiliwe na mtu, kwani ni matakatifu nayo.

35Sharti uwafanyizie Haroni na wanawe hivyo vyote, nilivyokuagiza, ukiwajaza magao yao siku saba.

36Kila siku utatoa dume la ng'ombe aliye kijana bado kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo kumpatia upozi, uieue nayo meza ya kutambikia kwa kuwapatia upozi hapo; kisha umpake mafuta ya kumfanya kuwa mtakatifu.

37Siku saba nayo meza ya kutambikia uipatie upozi na kuitakasa, ndipo, meza ya kutambikia itakapokuwa takatifu yenyewe, naye kila atakayeigusa sharti awe ametolewa kuwa mtakatifu.

Ng'ombe za tambiko za kila siku.

(38-42: 4 Mose 28:3-8.)

38Nayo haya ndiyo, utolee mezani pa kutambikia: wana kondoo wawili wa mwaka mmoja kila siku pasipo kukoma.

39Mwana kondoo mmoja umtoe asubuhi, naye mwana kondoo wa pili umtoe saa za jioni.[#Sh. 141:2.]

40Tena pamoja na kila mwana kondoo utoe vibaba vitatu vya unga mwembamba uliochanganywa na kibaba kimoja cha mafuta yaliyotwangwa vema, tena kibaba kimoja cha mvinyo kuwa kinywaji cha tambiko.

41Naye mwana kondoo wa pili na umtoe saa za jioni pamoja na kilaji cha tambiko kama asubuhi; huo utakuwa moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana.

42Hizi na ziwe ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, wao wa vizazi vyenu watakazozitoa siku zote mbele ya Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano; hapo ndipo, nitakapokutana nanyi, napo ndipo, nitakaposema na wewe.

43Hapo ndipo, nitakapokutana kweli na wana wa Isiraeli, nalo Hema litapata kuwa takatifu kwa ajili ya utukufu wangu.[#2 Mose 20:24.]

44Mimi nitalitakasa Hema la Mkutano na meza ya kutambikia, naye Haroni na wanawe nitawatakasa, wapate kuwa watambikaji wangu.

45Nami nitakaa katikati ya wana wa Isiraeli, niwe Mungu wao.

46Nao watajua, ya kuwa mimi Bwana ni Mungu wao aliyewatoa katika nchi ya Misri, nikae katikati yao, mimi Bwana niliye Mungu wao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania