The chat will start when you send the first message.
1Watu walipoona, ya kuwa Mose anakawia kushuka mlimani, watu wakamkusanyikia Haroni, wakamwambia: Haya! Tufanyie miungu itakayotuongoza! Kwani hatuyajui yaliyompata huyo Mose aliyetutoa katika nchi ya Misri.
2Haroni akawaambia: Ziondoeni pete za dhahabu masikioni kwa wake zenu na kwa wana wenu wa kiume na wa kike, mniletee!
3Ndipo, watu wote walipoziondoa pete za dhahabu za masikioni kwao, wakampelekea Haroni.
4Akazichukua mikononi mwao, akazivunjavunja kwa patasi, akaziyeyusha, akazitengeneza kuwa ndama. Ndipo, waliposema: Huyu ndiye Mungu wako, Isiraeli, aliyekutoa katika nchi ya Misri.[#1 Fal. 12:28; Sh. 106:19-20; Tume. 7:41.]
5Haroni alipoyaona, akajenga mbele yake pa kutambikia, kisha Haroni akatangaza kwamba: Kesho ni sikukuu ya Bwana.
6Kesho yake wakaamka na mapema, wakatoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima pamoja na kuleta ng'ombe za tambiko za shukrani. Kisha watu wakakalia kula na kunywa, kisha wakainukia kucheza.[#1 Kor. 10:7.]
7Lakini Bwana akamwambia Mose: Nenda kushuka! Kwani wao walio ukoo wako, uliowatoa katika nchi ya Misri, wamefanya mabaya
8Wakiondoka upesi katika njia, niliyowaagiza; wamejitengenezea ndama kwa kuyeyusha dhahabu, wakaiangukia na kuitambikia wakisema: Huyu ndiye Mungu wako, Isiraeli, aliyekutoa katika nchi ya Misri.[#2 Mose 20:4,23; 32:4.]
9Bwana akamwambia Mose: Nikiwatazama watu hawa ninawaona kuwa watu wenye kosi ngumu.
10Sasa niache, makali yangu yawawakie moto, uwale! Kisha nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa.[#1 Mose 14:11-20.]
11Lakini Mose akambembeleza Bwana Mungu wake kwamba: Bwana, mbona utayaacha makali yako, yawawakie watu wako, uliowatoa katika nchi ya Misri kwa uwezo mkuu na kwa mkono ulio na nguvu?
12Mbona unataka, Wamisri waseme kwamba: Aliwatoa kwa ubaya, awaue milimani na kuwatowesha juu ya nchi? Geuka na kuyaacha makali yako yanayowaka moto, uwahurumie walio ukoo wako kwa ajili ya mabaya, waliyoyafanya!
13Wakumbuke watumishi wako, Aburahamu na Isaka na Isiraeli, uliowaapia ukijitaja mwenyewe na kuwaambia: Wa uzao wenu nitawafanya kuwa wengi kama nyota za mbinguni, nayo nchi hiyo yote, niliyoisema, nitawapa wao wa uzao wenu, waichukue kuwa yao kale na kale.[#1 Mose 22:16-17; 26:4; 28:14.]
14Ndipo, Bwana alipogeuza moyo, asiwafanyie hayo mabaya, aliyoyasema, ya kuwa atawafanyizia wao walio ukoo wake.
15Kisha Mose akageuka, akatelemka mlimani akizishika zile mbao mbili za Ushahidi mkononi mwake, nazo hizo mbao zilikuwa zimeandikwa pande zao zote mbili, kweli zilikuwa zimeandikwa huku na huko.
16Tena hizi mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu mwenyewe yaliyochorwa humo mbaoni.[#2 Mose 31:18.]
17Yosua alipozisikia sauti za makelele, watu waliyoyapiga, akamwambia Mose: Yako makelele makambini kama ya vita.
18Akajibu: Haya siyo makelele ya wapiga vita walioshinda, wala siyo makelele yao walioshindwa, mimi ninasikia tu sauti zao wanaoitikiana na kuimba.
19Mose alipoyafikia makambi karibu na kuona, jinsi hiyo ndama ilivyochezewa, ndipo, makali yake yalipowaka, akazitupa zile mbao, alizozishika mikononi mwake, akazivunja mlimani chini.
20Kisha akaichukua hiyo ndama, waliyoitengeza, akaitekeketeza kwa moto, akaipondaponda kuwa majivu, akayamwaga majini, akawapa wana wa Isiraeli, wayanywe.
21Kisha Mose akamwuliza Haroni: Watu hawa wamekukosea nini, ukiwakosesha kosa kubwa kama hili?
22Haroni akamwambia: Bwana wangu, makali yako yasiwake moto! Unawajua watu hawa, ya kuwa ni wabaya.
23Waliniambia: Tufanyie miungu itakayotuongoza! Kwani hatuyajui yaliyompata huyo Mose aliyetutoa katika nchi ya Misri.
24Nikawaambia: Kila mwenye dhahabu na aziondoe kwake, anipe mimi! Basi, waliponipa, nikazitupa motoni, ikatoka ndama hii.
25Mose alipoona, ya kuwa watu wanajikweza sana, kwa kuwa Haroni amewakweza, wafyozwe vibaya nao wawainukiao,
26ndipo, Mose alipokwenda kusimama langoni penye makambi, akasema: Aliye wa Bwana na aje kwangu! Ndipo, wana wa Lawi walipokusanyika wote kwake,
27akawaambia: Hivi ndivyo, alivyosema Bwana Mungu wa Isiraeli: Jifungeni kila mtu upanga wake kiunoni pake, mzunguke makambini kwenda na kurudi toka lango la huku hata lango la huko, mkiua kila mtu ndugu yake naye mwenzake naye rafiki yake!
28Wana wa Lawi wakayafanya, Mose aliyowaambia, wakauawa siku hiyo watu wa ukoo huo kama 3000.
29Kisha Mose akawaambia: Yajazeni leo magao yenu, mwe wa Bwana, maana kila mmoja wenu hakumjua wala mtoto wake wala ndugu yake; Bwana na awape leo mbaraka![#2 Mose 28:41; 4 Mose 3:6-10; 5 Mose 33:8-11.]
30Ikawa kesho yake, ndipo, Mose alipowaambia watu: Ninyi mmekosa kosa kubwa; sasa nitapanda kwenda kwa Bwana, nitazame, kama nitaweza kuwapatia upozi kwa ajili ya kosa lenu.
31Mose aliporudi kwa Bwana akamwambia: Watu wa ukoo huu wamekosa kosa kubwa wakijifanyizia mungu wa dhahabu.[#Sh. 69:29; Dan. 12:1; Luk. 10:20; Rom. 9:3.]
32Lakini sasa uwaondolee kosa lao! Kama haiwezekani, lifute jina langu katika Kitabu chako, ulichokiandika!
33Naye Bwana akamwambia Mose: Anikoseaye ndiye, nitakayemfuta katika Kitabu changu.
34Sasa nenda, uwapeleke watu hawa hapo, nilipokuambia! Naye malaika wangu utamwona, akikutangulia. Lakini siku yangu ya mapatilizo itakapofika, nitawapatilizia hili kosa lao.
35Ndivyo, Bwana alivyowapiga watu wa huo ukoo kwa kuifanya hiyo ndama, Haroni aliyoifanya.