2 Mose 36

2 Mose 36

Mchango mwingi mno wa watu.

1Besaleli na Oholiabu na watu wote, Bwana aliowapa werevu wa kweli mioyoni mwao, watazifanya kazi hizo kwa huo werevu wa kweli na kwa utambuzi na kwa hivyo, wanavyojua kufanya kazi zote za utumishi wa Patakatifu, watafanya yote, Bwana aliyoyaagiza.

2Kisha Mose akawaita Besaleli na Oholiabu na watu wote waliokuwa werevu wa kweli mioyoni mwao, Bwana aliowapa werevu wa kweli mioyoni mwao, nao wote waliohimizwa na mioyo yao kuzijia hizo kazi, wazifanye.

3Wakachukua kwake Mose vipaji vyote vya tambiko, wana wa Isiraeli walivyovitoa vya kazi za utumishi wa Patakatifu, zipate kufanyika; nao walikuwa wakileta bado kwake vipaji, walivyovitoa kwa kupendezwa tu kila kulipokucha.

4Kisha wakaja wote waliokuwa werevu wa kweli wa kuzifanya hizo kazi zote za Patakatifu, kila mmoja wakitoka penye kazi zao, walizozifanya wao,

5wakamwambia Mose kwamba: Watu wanaleta mengi zaidi kabisa kuliko yanayotakiwa ya kuzimaliza hizo kazi, Bwana alizoagiza kuzifanya.

6Ndipo, Mose alipotoa amri, wakaitangaza makambini po pote kwa sauti kuu kwamba: Watu wote, waume kwa wake, wasijisumbue tena kutoa vipaji vya tambiko vya hapo Patakatifu! Ndivyo, watu walivyozuiliwa kuleta vitu tena.

7Nayo yaliyokuwapo hapo ya kuzifanya hizo kazi yakatosha kabisa kuzifanya hizo kazi zote pia, tena yakasalia.

Patakatifu panajengwa.

(8-19: 2 Mose 26:1-14.)

8Miongoni mwao waliofanya kazi wao wote waliokuwa werevu wa kweli mioyoni mwao wakalitengeneza Kao lenyewe kwa mapazia kumi yaliyoshonwa kwa nguo za bafta ngumu na kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu, nayo yalikuwa yenye mifano ya Makerubi, kama mafundi wa kufuma wanavyojua kuitengeneza; ndivyo, walivyofanya.

9Urefu wa pazia moja ulikuwa mikono ishirini na minane, nao upana wake ulikuwa mikono minne, kila pazia moja lilikuwa lenye kipimo hiki kimoja, kilikuwa cha mapazia yote.

10Akaunga mapazia matano kila moja na mwenzake kuwa moja, nayo matano ya pili akayaunga vivyo hivyo kila moja na mwenzake kuwa moja.

11Kisha akashona vitanzi vya nguo nyeusi za kifalme penye upindo wa nje wa kila pazia moja hapo, lilipoungwa na jingine; vivyo hivyo akavitia napo penye yupindo wa nje wa kila pazia la pili hapo, lilipoungwa nalo la kwanza.

12Akashona vitanzi hamsini katika kila pazia moja upande mmoja, na tena vitanzi hamsini katika upindo wa kila pazia la pili upande huo ulioungwa na pazia la kwanza; hivyo vitanzi vilielekeana kila kimoja na mwenzake.

13Kisha akafanya vifungo vya dhahabu hamsini, apate kuyafunga mapazia kila moja na mwenzake; kwa hivyo vifungo Kao likapata kuwa moja.

14Kisha akafanya mapazia ya nywele za mbuzi kuwa hema juu ya Kao lenyewe, akatengeneza mapazia kumi na moja.

15Urefu a kila pazia moja ulikuwa mikono thelathini, nao upana wa kila pazia moja ulikuwa mikono minne; hiki kipimo kimoja kilikuwa chao mapazia yote kumi na moja.

16Kisha akayaunga mapazia matano kuwa moja, nayo yale sita akayaunga kuwa moja.

17Kisha akashona vitanzi hamsini katika upindo wa nje wa kila pazia moja hapo, lilipoungwa na jingine; tena akashona vitanzi hamsini katika upindo wa nje wa kila pazia la pili hapo, lilipoungwa nalo la kwanza.

18Kisha akafanya vifungo vya shaba hamsini vya kuliungia hilo hema, liwe moja.

19Kisha akatengeneza chandalua cha hema kwa ngozi nyekundu za madume ya kondoo, tena akatengneza chandalua cha pili kwa ngozi za pomboo kuwa juu yake.

(20-30: 2 Mose 26:15-25.)

20Kisha akatengeneza mbao za Kao lenyewe za migunga zilizosimama.

21Urefu wa kila ubao ulikuwa mikono kumi, nao upana wake kila ubao mmoja ulikuwa mkono mmoja na nusu.

22Kila ubao mmoja ulikuwa na vigerezi viwili, navyo vilitazamana kila kimoja na mwenzake. Vivyo hivyo akavitengeneza kila ubao mmoja wa Kao lenyewe.

23Akazitengeneza hizo mbao za Kao lenyewe kuwa ishirini upande wa kusini, ndio upande wa juani.

24Chini ya hizi mbao ishirini akatengeneza viguu vya fedha arobaini, vikawa viguu viwili chini ya kila ubao mmoja vya kuvitilia vigerezi vyake viwili, vivyo hivyo chini ya kila ubao mmoja viguu viwili vya kuvitilia vigerezi vyake viwili.

25Hata upande wa pili wa Kao, ndio upande wa kaskazini, akatengeneza vilevile mbao ishirini,

26na viguu arobaini vya fedha, viguu viwili chini ya kila ubao mmoja, vivyo hivyo viwili chini ya kila ubao mmoja.

27Lakini upande wa nyuma wa Kao unaoelekea baharini akatengeneza mbao sita.

28Tena akatengeneza mbao mbili za pembeni mle Kaoni upande wa nyuma.

29Nazo zilikuwa kama pacha, toka chini viliendelea pamoja zote nzima mpaka juu penye pete la kwanza; hivyo ndivyo, alivyozitengeneza mbao zote mbili za hizo pembe mbili za nyuma.

30Hivyo zote pamoja zilikuwa mbao nane, navyo viguu vya fedha vilikuwa kumi na sita, viguu viwili chini ya kila ubao mmoja.

(31-34: 2 Mose 26:26-30.)

31Kisha akatengeneza misunguo ya migunga, mitano ya mbao za upande mmoja wa Kao,

32tena misunguo mitano ya mbao za upande wa pili wa Kao, tena misunguo mitano ya mbao za upande wa nyuma wa Kao unaoelekea baharini.

33Kisha akatengeneza msunguo wa katikati, upite katikati ya mbao toka mwisho wa huku hata mwisho wa huko.

34Nazo mbao akazifunikiza dhahabu, nayo mapete yao akayatengeneza kwa dhahabu, yalikuwa ya kutilia misunguo, nayo misunguo akaifunikiza dhahabu.

(35-38: 2 Mose 26:31-37.)

35Kisha akatengeneza pazia lililoshonwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu; lilikuwa kazi ya fundi wa kufuma, maana alilitengeneza kuwa lenye Makerubi.

36Kisha akalitengenezea nguzo nne za migunga, akazifunikiza dhahabu, navyo vifungo vyao vilikuwa vya dhahabu, kisha akazitengenezea miguu minne kwa kuyeyusha fedha.

37Napo hapo pa kuliingilia Hema akaweka guo kubwa lililotengenezwa kwa nguo za kifalme nyeusi na nyekundu na kwa nguo za bafta ngumu; nalo lilifumwa na mtu aliyejua kweli kufuma kwa nyuzi za rangi.

38Akalitengenezea nguzo tano zenye vifungo vyao. Kisha akazifunikiza dhahabu pamoja na vichwa vyao na vijiti vyao vya kuziungia, lakini miguu yao mitano ilikuwa ya shaba.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania