2 Mose 37

2 Mose 37

Vyombo vyake Patakatifu.

(1-9: 2 Mose 25:10-22.)

1Kisha Besaleli akalitengeneza Sanduku la mbao za migunga, urefu wake ulikuwa mikono miwili na nusu, nao upana wake ulikuwa mkono mmoja na nusu, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mkono mmoja na nusu.

2Akalifunikiza lote dhahabu tupu, upande wa ndani na upande wa nje, kisha akazungusha juu yake taji ya dhahabu.

3Kisha akatengeneza mapete manne kwa kuyeyusha dhahabu, akayatia penye pembe zake nne, mapete mawili upande wake mmoja, tena mapete mawili upande wake wa pili.

4Kisha akatengeneza mipiko ya migunga, nayo akaifunikiza dhahabu.

5Kisha akaitia mipiko hiyo katika yale mapete pande zote mbili za Sanduku, iwe ya kulichukulia Sanduku.

6Kisha akakitengeneza kifuniko kuwa Kiti cha Upozi cha dhahabu tupu, urefu wake ulikuwa mikono miwili na nusu, nao upana wake ulikuwa mkono mmoja na nusu.

7Kisha akatengeneza Makerubi mawili ya dhahabu, nayo yalitengenezwa kwa kuzifuafua hizo dhahabu, akayaweka pande zote mbili za mwisho wa Kiti cha Upozi:

8Kerubi moja akaliweka upande wa mwisho wa huku, nalo la pili upande wa mwisho wa huko. Ndivyo, alivyoyaweka hayo Makerubi pande zake zote mbili za mwisho wa Kiti cha Upozi.

9Nayo Makerubi yalikuwa yameyakunjua mabawa juu yakikifunika Kiti cha Upozi kwa mabawa yao, nazo nyuso zao zilikuwa zimeelekeana, hayo Makerubi yakikitazama Kiti cha Upozi kwa nyuso zao.

10Kisha akatengeneza meza kwa mbao za migunga, urefu wake ulikuwa mikono miwili, nao upana wake ulikuwa mkono mmoja, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mkono mmoja na nusu;

11akaifunikiza dhahabu tupu, kisha akazungusha juu yake taji ya dhahabu.

12Kisha akazungusha kando yake kibao cha kukingia chenye upana wa shibiri, nacho hicho kikingio akakizungushia taji ya dhahabu.

13Kisha akaitengenezea mapete manne kwa kuyeyusha dhahabu, nayo hayo mapete akayatia penye pembe zake nne zilizokuwa penye miguu yake minne.

14Hayo mapete yalikuwa papo hapo chini ya kikingio, wapate kutia humo mipiko ya kuichukulia hiyo meza.

15Kisha akatengeneza mipiko kwa migunga na kuifunikiza dhahabu, itumike ya kuichukulia hiyo meza.

16Kisha akatengeneza vyombo vya kuweka hapo mezani: vyano vyake na vijiko vyake na vikombe vyake na vitungi vyake vinavyotumikia vinywaji vya tambiko; vyote vilikuwa dhahabu tu.

(17-24: 2 Mose 25:31-39.)

17Kisha akatengeneza kinara cha dhahabu tupu; hicho kinara nacho akakitengeneza kwa kufuafua dhahabu, ikapata kukitoka chote kizima: shina lake na mti wake navyo vikombe vyake na vifundo vyake na maua yake, vyote pia vilikuwa vimetoka dhahabu iyo hiyo moja.

18Matawi sita yalitoka penye mbavu zake, matawi matatu ya kinara yalitoka penye ubavu mmoja, tena matawi matatu ya kinara yalitoka penye ubavu wa pili.

19Vikombe vitatu vilivyofanana na maua yao. Vivyo hivyo vilikuwa katika matawi yote sita yaliyotoka katika mti wa kinara.

20Lakini katika mti wa kinara vilikuwa vikombe vinne vilivyofanana na maua ya mlozi, yaani vifundo pamoja na maua yao.

21Tena kila mahali matawi mawili yalipotoka katika huo mti wake, chini yake kilikuwa kifundo kimoja; vilikuwa vivyo hivyo kila mahali, yalipotoka matawi mawili, nayo matawi yaliyotoka katika kinara yalikuwa sita.

22Vifundo na matawi yao yote ilikuwa kazi moja iliyoyatokeza yote pamoja kwa kuifua dhahabu iyo hiyo moja, nayo yalikuwa dhahabu tupu.

23Kisha akatengeneza taa zake saba; nazo koleo zake na makato yake yote yalikuwa dhahabu tupu.

24Alikitengeneza kinara pamoja na vyombo vyake kwa kipande cha dhahabu chenye uzito wa mizigo miwili.

(25-28: 2 Mose 30:1-5.)

25Kisha akatengeneza kwa migunga meza ya kuvukizia; urefu wake ulikuwa mkono mmoja, nao upana wake ulikuwa mkono mmoja, pande zote nne zilikuwa sawa, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mikono miwili.

26Akaifunikiza dhahabu tupu juu yake na kando yake pande zote na pembe zake, akazungusha juu yake taji ya dhahabu pande zote.

27Kisha akaitengenezea mapete mawili ya dhahabu, akayatia chini ya taji pande zake mbili penye mbavu zake mbili, yawe ya kutilia mipiko ya kuichukulia.

28Kisha akatengeneza mipiko kwa migunga, akaifunikiza dhahabu.

29Kisha akatengeneza mafuta matakatifu ya kupaka na mavukizo yanukayo vizuri yasiyochanganyika na mengine, kama mafundi wa kutengeneza manukato wanavyojua kuyatengeneza.[#2 Mose 30:25,35.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania