2 Mose 40

2 Mose 40

Kulieua Hema Takatifu.

(1-33: 2 Mose 25-31.)

1Bwana akamwambia Mose kwamba:

2Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza ulisimamishe Kao la Hema la Mkutano.

3Humo ndani uliweke Sanduku la Ushahidi, kisha ulitungike pazia mbele ya Sanduku.

4Kisha iingize meza na kuyatandika juu yake yanayopasa kuwekwa hapo, kisha kiingize kinara na kuziweka taa zake juu yake.

5Kisha iweke meza ya dhahabu ya kuvukizia mbele ya Sanduku la Ushahidi na kulitungika pazia pa kuliingilia Kao.

6Kisha iweke meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko mbele ya hapo pa kuliingilia Kao la Hema la Mkutano.

7Kisha uliweke birika katikati ya hema la Mkutano na meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko na kulitia maji.

8Kisha Kao ulizungushie ua na kulitungika guo la pazia la langoni kwa ua.

9Kisha yachukue mafuta ya kupaka, ulipake Kao lenyewe nayo yote yaliyomo; ndivyo, ulieue pamoja na vyombo vyake vyote kuwa vitakatifu.

10Kisha ipake mafuta meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, uieue, hiyo meza ya kutambikia ipate kuwa takatifu yenyewe.

11Kisha birika lipake mafuta nalo wekeo lake, ulieue.

12Kisha mwite Haroni nao wanawe, wafike hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, kisha waambie wajiogeshe majini.

13Kisha umvike Haroni mavazi matakatifu na kumpaka mafuta; hivi ndivyo, utakavyomweua, apate kuwa mtambikaji wangu.

14Kisha wafikishe wanawe karibu, uwavike shati,

15kisha wapake nao mafuta, kama ulivyompaka baba yao mafuta, wapate kuwa watambikaji wangu. Huko kuwapaka mafuta kutawapatia utambikaji wa kale na kale kwa vizazi vyao.

16Mose akayafanya yote; kama Bwana alivyomwagiza, ndivyo, alivyoyafanya yote sawasawa.

17Ikawa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, ndipo, Kao liliposimamishwa.

18Mose alipolisimamisha Kao akaiweka miguu yake, akatia humo mbao zake, akazitia misunguo yake na kuzisimamisha nguzo zake.

19Kisha akaweka juu ya Hema chandalua chake, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

20Kisha akauchukua ushahidi, akauweka Sandukuni, akatia nayo mipiko penye Sanduku, akakiweka Kiti cha Upozi juu ya Sanduku.

21Kisha akaliingiza Sanduku Kaoni ndani, akalitungika lile guo kubwa la pazia, lilifiche Sanduku la Ushahidi, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

22Kisha akapeleka meza ndani ya Hema la Mkutano, akaiweka upande wa kaskazini wa Kao nje ya pazia,

23kisha akamwekea Bwana juu yake mikate na kuitandika mistari mistari, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

24Kisha akakiweka kinara Hemani mwa Mkutano upande wa kusini wa Kao, kuielekea meza.

25Kisha akaziweka taa zake juu yake mbele ya Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

26Kisha akaiweka meza ya dhahabu ya kuvukizia katika Hema la Mkutano mbele ya pazia.

27Akavukizia juu yake mavukizo yanukayo vizuri, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

28Kisha akalitungika pazia hapo pa kuliingilia Kao.

29Kisha akaiweka meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko penye kuliingilia Kao la Hema la Mkutano, akatoa juu yake ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na vilaji vya tambiko, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

30Kisha akaliweka birika katikati ya Hema la Mkutano na meza ya kutambikia na kutia humo maji ya kujioshea.

31Kisha Mose na Haroni na wanawe wakajiosha humo mikono yao na miguu yao.

32Kila walipoliingia Hema la Mkutano, napo kila walipoikaribia meza ya kutambikia wakajiosha, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

33Kisha akausimamisha ua wa kulizunguka Kao na meza ya kutambikia, kisha akalitungika pazia langoni kwa ua. Ndivyo, Mose alivyozimaliza hizi kazi.

Utukufu wa Bwana unalijaza Kao lake.

34Kisha lile wingu likalifunika Hema la Mkutano, nao utukufu wa Bwana ukajaa Kaoni.[#2 Mose 13:21; 4 Mose 19:15-22; 1 Fal. 8:10-11; Yes. 4:5.]

35Naye Mose hakuweza kuliingia Hema la Mkutano, kwa kuwa wingu lililikalia, nao utukufu wa Bwana ulijaa Hemani.[#Ez. 43:5.]

36Hilo wingu lilipoondoka penye Kao, ndipo, wana wa Isiraeli walipoondoka kwenda safari yao; ndivyo, vilivyokuwa katika hizo safari zao zote.[#4 Mose 10:34-36.]

37Lakini wingu lisipoondoka, hawakuondoka nao kwenda safari mpaka siku hiyo, lilipoondoka tena.

38Kwani wingu la Bwana lililikalia Kao mchana, lakini usiku ulikuwamo moto, nao wote walio wa mlango wa Isiraeli wakauona katika safari zao zote.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania