2 Mose 5

2 Mose 5

Farao anamkataa Bwana.

1Baadaye Mose na Haroni wakaenda, wakamwambia Farao: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu wa Isiraeli: Hawa watu walio ukoo wangu wape ruhusa kwenda kunifanyizia sikukuu nyikani![#2 Mose 3:18; 7:16; 8:1,20; 9:1,13.]

2Lakini Farao akasema: Bwana ni nani, nimsikie sauti yake na kuwapa Waisiraeli ruhusa kwenda? Simjui Bwana, wala sitawapa Waisiraeli ruhusa kwenda.[#Dan. 3:15.]

3Nao wakasema: Mungu wa Waebureo amekutana nasi, kwa hiyo tunataka kwenda nyikani safari ya siku tatu, tumtambikie Bwana Mungu wetu, asitupige kwa magonjwa yauayo wala kwa upanga.

4Lakini mfalme wa Misri akawaambia: Mbona ninyi Mose na Haroni mnataka kuwatoa tu watu hawa katika kazi zao? Nendeni kuzifanya hizo kazi zenu ngumu!

5Tena Farao akasema: Tazameni, jinsi watu hawa wa nchi hii walivyo wengi sasa! Nanyi mwataka kuwapumzisha, wasizifanye kazi zao ngumu.[#2 Mose 1:7,12.]

Waisiraeli wanateswa zaidi.

6Siku ile Farao akawaagiza wale wasimamizi wakali wa hao watu nao waangaliaji wao kwamba:

7Watu hawa msiwape tena majani makavu ya kuumbia matofali kama siku zote! Sharti waende wenyewe kujiokotea majani makavu.

8Lakini hesabu ya matofali, waliyoyafanya siku zote, sharti mwabandikie iyo hiyo, msiipunguguze! Kwani ndio walegevu, kwa hiyo hupiga kelele kwamba: Twende kumtambikia Mungu wetu!

9Kazi za utumwa sharti ziwalemee zaidi watu hawa, wakizifanya, wasitazamie maneno ya uwongo.

10Ndipo, wasimamizi wale wakali wa watu hao na waangaliaji wao walipowaambia watu kwamba: Hakuna tena atakayewapa ninyi majani makavu;

11nendeni wenyewe kujiokotea majani makavu po pote, mtakapoyaona! Lakini agano la kazi zenu halipunguki.

12Ndipo, watu hao walipotawanyika katika nchi nzima ya Misri kuokota majani makavu ya kuumbia matofali.

13Nao wasimamizi wakawahimiza kwa ukali wao kwamba: Zimalizeni kazi zenu za kuitimiza hesabu yao ya siku zote kama hapo, mlipopewa majani makavu!

14Nao waangaliaji wana wana wa Isiraeli, wale wasimamizi wakali wa Farao waliowawekea, wakapigwa kwa kwamba: Mbona hamkulitimiza jana na leo agano lenu la matofali la siku zote?

15Ndipo, waangaliaji wa wana wa Isiraeli walipokuja, wakamlilia Farao kwamba; Mbona unawafanyizia watumwa wako hivyo?

16Majani makavu watumwa wako hawapewi, lakini wanatuambia: Fanyeni matofali yayo hayo! Nasi watumwa wako tunapigwa, lakini wenye kukosa ni watu wako.

17Lakini akasema: Ninyi m walegevu, m walegevu kweli. Kawa sababu hii mnasema: Twende, tumtambikie Bwana!

18Sasa haya! Nendeni kuzifanya kazi zenu! Majani makavu hamtapewa, ila hesabu ya matofali iliyowekwa sharti mwitoe!

19Nao waangaliaji wa wana wa Isiraeli wakajiona, ya kuwa wamepatwa na mabaya kwa kuambiwa: Msiipunguze hesabu ya matofali ya siku zote!

20Walipotoka kwake Farao, wakamkuta Mose na Haroni waliosimama hapo na kuwangoja.

21Ndipo, walipowaambia: Bwana na awatazame ninyi, mlivyo, awapatilize! Kwani mmeufanya mnuko wetu kuwa mbaya puani mwake Farao namo puani mwao watumishi wake, mkawapa panga mikononi mwao, watuue.[#1 Mose 34:30.]

22Naye Mose akamrudia Bwana na kusema: Bwana, kwa nini unawafanyia watu hawa mabaya kama hayo? Ndiyo haya, uliyonituma?

23Kwani tangu hapo, nilipoingia kwake Farao kusema naye katika Jina lako, amezidi kuwafanyizia watu hawa mabaya, wewe nawe hukuwaponya kabisa wao walio ukoo wako.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania