Ezekieli 1

Ezekieli 1

Utukufu wa Mungu unamtokea Ezekieli.

1Ikawa siku ya tano ya mwezi wa nne katika mwaka wa 30, nilipokuwa katikati ya mateka waliohamishwa kwenye mto wa Kebari, ndipo, mbingu zilipofunuka, nikaona maono ya Mungu.[#Ez. 10:15.]

2Siku hiyo ya tano ya mwezi huo ilikuwa ya mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yoyakini.[#2 Fal. 24:15.]

3Ndipo, neno la Bwana lilipomjia Ezekieli, mwana wa Buzi; naye alikuwa mtambikaji katika nchi ya Wakasidi kwenye mto wa Kebari, nao mkono wake Bwana ulikuwa juu yake.

4Nilipotazama nikaona upepo wenye nguvu uliotoka kaskazini na wingu kubwa lililowaka mioto iliyokamatana na kumetameta po pote, namo ndani yake mlikuwamo kilichofanana na shaba iliyong'aa sana mle motoni katikati.[#Ez. 10; Ufu. 4:6-8.]

5Humo ndani katikati mkaonekana yaliyokuwa kama nyama wanne, nao nilipozitazama sura zao, zilikuwa kama mifano ya mtu.

6Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, tena kila mmoja alikuwa na mabawa manne.

7Miguu yao ilikuwa imenyoka, lakini nyayo za miguu yao zilikuwa kama nyayo za ndama, zikametuka kama shaba iliyokatuliwa sana.

8Chini ya mabawa yao kulikuwa na mikono ya kimtu pande zote nne. Nyuso zao na mabawa yao hao wanne yalikuwa hivyo:

9mabawa yao yalikuwa yanashikana kila moja na bawa lenziwe; nao walipokwenda hawakuzigeuza nyuso zao, ila kila mmoja alikwenda na kufuata hapo, uso wake ulipoelekea.

10Nyuso zao mifano yao ilikuwa hivyo: mbele ni uso wa mtu, kuumeni kwao hao wanne ni uso wa simba, kushotoni kwao hao wanne ni uso wa ng'ombe, tena kwao hao wanne nyuma yao ni uso wa tai.

11Nayo mabawa yao yalikuwa yamejitanda juu, kwake kila mmoja mawili yalishikana, mawili yaliifunika miili yao.

12Kila mmoja wakaenda na kufuata hapo, uso wake lulipowlekea; roho zao zilikotaka kwenda, ndiko, walikokwenda tu pasipo kuzigeuza nyuso.[#Ez. 1:20.]

13Nazo sura za hao nyama nilipozitazama, zilifanana kuwa kama makaa ya moto yaliyowaka kwa mfano wa mienge iliyokwenda huko na huko katikati yao hao nyama, nao moto huo ulikuwa umeng'aa kabisa, hata umeme ulitoka humo motoni.

14Kisha hao nyama wakapiga mbio kwenda na kurudi, vikaonekana kuwa kama umeme.

15Nilipowatazama hao nyama mara nikaona gurudumu moja huku nchini kando yao hao nyama pande zote nne.

16Nilipoyatazama hayo magurudumu, jinsi yalivyotengenezwa, jinsi yalivyokuwa, yalikuwa kama kito cha Tarsisi, yote manne mfano wao ulikuwa huo mmoja; nilipoyatazama tena, jinsi yalivyotengenezwa, yalionekana kuwa kama gurudumu moja lililomo ndani ya gurudumu lenziwe.

17Yalipokwenda yalikwenda panda zote nne pasipo kugeuka katika mwendo wao wa kwenda mbele tu.

18Vikuku vyao vilikuwa virefu mno vya kuogopesha; tena hivi vikuku vilijaa macho po pote kwao yote manne.

19Wale nyama walipokwenda, hayo magurudumu yalikwenda nayo kando; tena hao nyama walipochukuliwa juu kutoka katika nchi, hayo magurudumu yakachukuliwa juu nayo.

20Roho zao hao zilikotaka kwenda, ndiko, walikokwenda; roho zao zilipotaka kwenda huko, nayo magurudumu yalichukuliwa kwenda pamoja nao, kwani roho za hao nyama zilikuwa namo katika magurudumu.[#Ez. 1:12.]

21Hao walipokwenda, nayo yalikwenda; hao waliposimama, nayo yalisimama; hao walipochukuliwa juu kutoka katika nchi, nayo magurudumu yalichukuliwa kwenda pamoja nao, kwani roho za hao nyama zilikuwa namo katika magurudumu.

22Juu ya vichwa vyao hao nyama kulikuwako lililofanana na ukingo, mfano wake ulikuwa kama ulanga uangazikao vizuri mno, mtu aogope kuutazama, nao ulikuwa umetandwa juu penye vichwa vyao.[#2 Mose 24:10.]

23Chini ya huo ukingo mabawa yao yalikuwa yamenyoka, kila moja kikielekea lenziwe, kila nyama mmoja mabawa mawili yalikuwa ya kujifunikia juu, tena mabawa mawili yalikuwa ya kujifunikia miili yao.

24Nikazisikia sauti za mabawa yao, nazo zilikuwa kama sauti za maji mengi au kama shindo la Mwenyezi. Walipokwenda sauti za kuvuma zilikuwa kama za uvumi wa makambi ya vikosi vya askari. Waliposimama huyalegeza mabawa yao.

25Kisha waliposimama na kuyalegeza mabawa yao, kulikuwa na uvumi huko kwenye ukingo uliokuwa juu ya vichwa vyao.

26Tena juu ya ukingo uliokuwa juu ya vichwa vyao kulionekana kilichokuwa kama kito cha Safiro, nacho kilifanana na kiti cha kifalme; tena katika hicho kilichofanana na kiti cha kifalme kulionekana aliyefanana na mtu, anakikalia.[#Ez. 1:22.]

27Nilipotazama tena nikaona ndani yake kilichofanana na shaba iliyong'aa sana, kilionekana kuwa kama moto uliofungiwa nyumbani po pote. Tena hapo palipokuwa kama kiuno chake mpaka juu, tena toka hapo palipofanana kuwa kama kiuno chake mpaka chini nilipopatazama nikaona kuwa kama moto uung'aao kabisa po pote.

28Ulionekana kuwa kama upindi ulioko mawinguni siku ya mvua, ndivyo, kuangazika kwake kulivyokuwa po pote; huu ndio mfano wa utukufu wake Bwana. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mwenye kusema.[#Ufu. 4:3.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania