Ezekieli 16

Ezekieli 16

Wayerusalemu wanafanana na mwanamke mgoni.

(Taz. Ez. 23.)

1Neno la Bwana likanijia la kwamba:

2Mwana wa mtu, wajulishe Wayerusalemu machukizo yao

3ukiwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyouambia Yerusalemu: Nchi ya Kanaani ndiko kwenu kwa mwanzo wako na kwa kuzaliwa kwako; baba yako ni Mwamori, mama yako ni Mhiti.

4Nako kuzaliwa kwako kulikuwa hivyo: siku ulipozaliwa hukukatwa kitovu, wala hukuogoshwa maji, utakate, wala hukupakwa chumvi hata kidogo, wala hukuvikwa nguo za kitoto.

5Halikuwako jicho lililokuonea uchungu wa hukufanyizia moja tu la mambo hayo kwa lililokuonea uchungu wa kukufanyizia moja tu la mambo hayo kwa kukuhurumia, ila ulitupwa shambani, kwa kuwa waliichukia roho yako siku, ulipozaliwa.

6Nikapita hapo, ulipokuwa, nikakuona ulivyogaagaa katika damu yako nikakuambia: Hivyo, unavyolala katika damu yako, uwe mzima! Nikakuambia kweli: Hivyo unavyolala katika damu yako, uwe mzima!

7Nitakupa kuwa maelfu na maelfu, kama majani ya shambani yalivyo mengi. Ndipo, ulipokua na kuendelea hivyo, mpaka ukawa mkubwa, ukapata kuwa mzuri zaidi, maziwa yako yakapata nguvu nazo nywele zako zikaota sana, lakini wewe ulikuwa ungaliko uchi bado pasipo kufunikwa na nguo.

8Nikapita hapo, ulipokuwa, nikakuona, ya kuwa siku zako za kuvunja ungo zimetimia, nikakutandia guo langu la kujifunika, nikaufunika uchi wako, nikakuapia na kukufanya agano na wewe, nawe ukawa wangu; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#2 Mose 19:5; Ruti 3:9.]

9Kisha nikakuogesha maji na kukumwagia mengi, damu yako ikutoke kabisa, nikakupaka mafuta.

10Nikakuvika nguo za rangi, nikakupa hata viatu vya ngozi ya pomboo, nikakufunga nao mharuma wa bafta, nikakupa ukaya wa hariri.

11Kisha nikakupamba kwa mapambo: nikakupa vikuku vya kuvaa mikononi pako na mkufu wa shingoni pako.

12Nikakupa navyo vipini vya puani na mapete ya masikioni na kilemba chenye utukufu kichwani pako.

13Hivyo ulipata mapambo ya dhahabu na ya fedha na mavazi ya bafta na ya hariri na ya nguo za rangi, ukala vikate vya unga uliopepetwa vema sana na asali na mafuta, ukawa mzuri sanasana, ukafanikiwa kupata macheo ya kifalme.

14Uvumi wako ukatoka, ukaenea kwa mataifa, kuwa uzuri wako ndio uzuri uliotimilika kabisa kwa ajili ya urembo, niliokutia; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Omb. 2:15.]

15Lakini ukajiegemezea uzuri wako, ukafanya ugoni, kila aliyepita ukamtupiatupia mapendeleo yako, ukawa wake.[#2 Mose 34:16.]

16Ukachukua mavazi yako, ukajitengenezea pa kutambikia milimani, ukapapamba nguo za rangi; ndiko, ulikofanyizia ugoni usiokuwa kale, wala hautakuwa tena.

17Kisha ukayachukua mapambo yako matukufu yaliyo dhahabu zangu na fedha zangu, nilizokupa, ukajitengenezea vinyago vya kiume, ukafanya ugoni navyo.

18Ukayachukua nayo mavazi yako ya nguo za rangi, ukavivika, ukavipelekea nayo mafuta yangu na uvumba wangu kuwa mbele yao.

19Hata vikate vyangu, nilivyokupa vya unga uliopepetwa vema sana, na mafuta na asali, niliyokulisha, ukayatoa mbele yao kuwa uvukizo wenye mnuko wa kupendeza. Ndivyo, ilivyokuwa kweli; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

20Ukawachukua nao wanao wa kiume na wa kike, uliowazaa, wawe wangu, ukawatoa kuwa ng'ombe zao za tambiko na chakula chao. Je? Ugoni wako haukutosha,[#2 Fal. 16:3; Yer. 7:31.]

21ukiwachinja wanangu, ukawatoa na kuwapitisha motoni, wawe wao?

22Ulipoyafanya machukizo yako yote na ugoni wako wote hukuzikumbuka siku za utoto wako za kuwa uchi pasipo kufunikwa na nguo, ulipokuwa unagaagaa katika damu yako?[#Ez. 16:6-7.]

23Kwa kuwa umekwisha kuyafanya hayo mabaya yako yote, yatakupata! Yatakupata kweli! ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

24Kisha ukajijengea nyumba ya vinyago, uwanjani po pote ukajitengenezea pa kutambikia.

25Pembeni po pote penye barabara ukajenga pako pa kutambikia, nao uzuri wako ukautumia, mpaka ukiwa chukizo, ukimpanulia kila aliyepita miguu yako, ukauzidisha ugoni wako.

26Ukafanya ugoni nao Wamisri, uliokaa nao, walio wenye miili mikubwa, ukauzidisha ugoni, kusudi unikasirishe.

27Mara nikakukunjulia mkono wangu, nikakupunguzia yakupasayo, nikakutia mikononi mwao wakuchukiao, wakufanyie wayatakayo, ni wale wanawake wa Kifilisti waliopatwa na soni kwa ajili ya njia zako zenye uzinzi.

28Ukafanya ugoni nao wana wa Asuri, kwa kuwa hujashiba bao; ukafanya ugoni nao, lakini hapo napo hukushiba.

29Ukauzidisha ugoni wako katika nchi ya Kanaani mpaka huko, Wakasidi wanakokaa, lakini hapo napo hukushiba.

30Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Kweli moyo wako ulikuwa unatamani sana kupendwa, ukiyafanya hayo yote yanayofanywa na mwanamke mgoni asiyejua soni.

31Ilikuwa hapo, ulipovojenga vyumba vyako vya vinyago po pote barabarani pembeni, ulipopatengeneza pako pa kutambikia uwanjani po pote. Tena hukuwa kama mwanamke mgoni aubeuaye mshahara.[#Ez. 16:24-25.]

32U mwanamke avunjaye unyumba, achukuaye wageni na kumwacha mumewe.

33Watu huwapa wanawake wagoni mapenyezo, lakini wewe huwapa wote wanaokupenda matunzo yako; ukiwagawia hayo, unataka, wakujie na kutoka po pote, wafanye ugoni na wewe.

34Kwako, ukifanya ugoni, mambo yamegeuka, yasiwe kama kwa wanawake wengine: wewe hutakiwi ugoni wakikufuatafuata, ila huwapa mshahara wewe, usipewe mwenyewe mshahara; hivyo ndivyo, vilivyogeuka.

Mapatilizo ya Yerusalemu

35Kwa hiyo, wewe mwanamke mgoni, lisikie neno la Bwana:

36Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa mapesa yako yamemwagwa, tena kwa kuwa unapofanya ugoni nao wote wakupendao hujifunulia nguo machoni pao, wauone uchi wako, hata kwenye magogo ya kutambikia yachukizayo, tena kwa kuwa umezimwaga damu za wanao, unaowapa, wawe wao:

37kwa hiyo utaniona, nikiwakusanya wote waliokupenda, ndio uliowapendeza, nao wote uliowapenda, nao wote uliowachukia, hao wote nitawakusanya, wakujie na kutoka po pote, kisha nitaufunua uchi wako wote.[#Yer. 13:22,26.]

38Kisha nitakupatiliza mapatilizo ya wanawake wavunjao unyumba nayo yao waliomwaga damu; hivyo nitakutoa, damu yako imwagwe kwa makali yenye moto na kwa wivu.

39Tena nitakutia mikononi mwao, wavivunje vyumba vyako vya vinyago, wapabomoe pako pa kutambikia, wakuvue nayo mavazi yako na kuyachukua mapambo yako matukufu, kisha wakuache, ukiwa mwenye uchi pasipo kujifunika kwa nguo.

40Kisha watakukusanyikia mkutano mkubwa, watakupiga mawe, kisha watakukatakata kwa panga zao.

41Nazo nyumba zako wataziteketeza kwa moto, wakutimilizie mapatilizo machoni pa wanawake wengi. Hivyo ndivyo, nitakavyokukomesha, usifanye ugoni tena, wala usilipe mshahara wa ugoni.

42Hivyo nitayatimiza kwako makali yangu yenye moto, wivu wangu uondoke kwako, nipate kutulia, nisikasirike tena.[#Ez. 5:13.]

43Kwa kuwa hukuzikumbuka siku za utoto wako, ukanichafua roho kwa kuyafanya hayo yote, kwa ajili ya hayo yote utaniona nami, nikikutwika njia yako kichwani; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Je? Hukuyaongeza machukizo yako yote kwa kufanya uzinzi?

44Itakuwa kila atumiaye mafumbo atakuambia fumbo hilo la kwamba: Kama mama alivyo, ndivyo, mwanawe wa kike alivyo.

45Wewe ndiwe mwana wa mama yako aliyemkumba mumewe pamoja na watoto wake, tena ndiwe dada ya ndugu zako wa kike waliowakumba waume zao pamoja na watoto wao; mama yenu ni Mhiti, naye baba yenu ni Mwamori.[#Ez. 16:3.]

46Dada yako mkubwa akaaye kushotoni kwako ni Samaria, yeye mwenyewe na wanawe; naye dada yako mdogo akaaye kuumeni kwako ni Sodomu na wanawe.[#Ez. 23:4.]

47Wewe kwanza hukuzifuata njia zao, wala hukufanya machukizo kama yao. Lakini ilikuwa punje kidogo tu, kisha ukafanya mabaya yaliyo makuu kuliko yao katika njia zako zote.

48Hivyo, nilivyo Mwenye uzima, ndivyo, asemavyo Bwana Mungu, dada yako mdogo Sodomu na wanawe hawakufanya mabaya, kama wewe na wanao mlivyofanya.

49Tazama, hayo, dada yako mdogo Sodomu na wanawe waliyoyafanya, yalikuwa maovu: majivuno na shibe za vyakula na utulivu wa kutengemana tu; hayo alikuwa nayo yeye mwenyewe na wanawe, lakini hawakuishikiza mikono ya wanyonge wala ya wakiwa.

50Wakajikuza, wakafanya yaliyo machukizo machoni pangu, nikawaondoa, nilipoyaona.[#1 Mose 18:20.]

51Naye Samaria makosa yake hayafiki kuwa nusu ya makosa yako wewe, ukayazidisha machukizo yako kuwa mengi kuliko yao; hivyo umetokeza, ya kuwa dada zako ni waongofu kuliko wewe kwa ajili ya machukizo yako yote, uliyoyafanya.

52Basi, wewe nawe shikwa na soni mwenyewe kama dada zako, ulipowaumbua! Kwa hivyo, ulivyokosa na kufanya machukizo kuliko wao, wameonekana kuwa waongofu kuliko wewe. Kwa hiyo wewe nawe iva uso kwa kushikwa na soni ikupasayo, kwa kuwa umewatokeza dada zako kuwa waongofu.

Yerusalemu utapokewa tena na Mungu.

53Itakuwa, nitakapoyafungua tena mafungo yao: mafungo ya Sodomu na ya wanawe wa kike nayo mafungo ya Samaria na ya wanawe wa kike, kisha nayo mafungo yako wewe, uwe katikati yao,[#Ez. 11:17.]

54kusudi upate kushikwa na soni ikupasayo; ndipo, utakapoona soni kweli kwa ajili yao yote, uliyoyafanya na kuwapatia wale matulizo ya mioyo yao.

55Hapo dada zako Sodomu na wanawe watakapokuwa tena, kama walivyokuwa kale, naye Samaria na wanawe watakapokuwa tena, kama walivyokuwa kale, ndipo, wewe nawe na wanao mtakapokuwa, kama mlivyokuwa kale.

56Je? Jina lake dada yako mdogo Sodomu halikuwa kinywani mwako la kutishia siku zile, ulipokuwa mwenye majivuno?

57Ni hapo, mabaya yako yalipokuwa hayajafunuliwa bado, kama yalivyofunuka siku zile, wanawake wa Ushami walipokutukana pamoja nao wote wanaokaa na kukuzunguka, ndio wanawake wa Wafilisti waliokubeza po pote.

58Hivyo ndivyo, ulivyotwikwa uzinzi wako na machukizo yako; ndivyo, asemavyo Bwana.

59Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Ninakufanyizia, kama wewe ulivyofanya; kiapo ulikibeua, ukalivunja agano.

60Lakini mimi nitalikumbuka agano, nililolifanya na wewe siku zile za utoto wako, nikusimikie agano la kale na kale.[#3 Mose 26:45; Hos. 2:15; Yer. 31:31-34; Ez. 37:26.]

61Ndipo, utakapozikumbuka njia zako na kuona soni utakapowachukua dada zako walio wakubwa kuliko wewe nao walio wadogo kuliko wewe, nitakapowatoa, nikupe wawe wanao, lakini sitavifanya kwa ajili ya agano lako.[#Ez. 20:43.]

62Ndipo, mimi nitakapolisimika lile agano, nitakalolifanya na wewe, upate kujua, ya kuwa mimi ni Bwana.

63Itakuwa hivyo, kusudi uyakumbuke hayo na kuiva uso, usikifumbue kinywa chako tena kwa ajili ya soni, utakayoiona, mimi nitakapokupoza kwa ajili yao yote, uliyoyafanya; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Ez. 36:31-32.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania