The chat will start when you send the first message.
1Basi, tunga ombolezo la kumwombolezea mkuu wa Isiraeli!
2Sema: Mama yako alikuwa nani? Simba mke! Alilala kwenye masimba, kwenye wana wa simba katikati aliwakuza wanawe.
3Hao wanawe mmoja wao, alipokwisha kumlea, akawa kijana wa simba, akajifunza kunyafua nyama, aliowakamata, akala nao watu.
4Wamizimu walipoyasikia, walimchimbia mwina, akanaswa humo, wakamtia pete puani, wakampeleka katika nchi ya Misri.[#2 Fal. 23:30-34.]
5Mama yake alipoona, ya kuwa alimngojea bure, kingojeo chake kikapotea; kisha akachukua mwingine katika wanawe, akamtunza, awe kijana wa simba.
6Akajiendea kwenye masimba kati, akawa kijana wa simba, akajifunza kunyafua nyama aliowakamata, akala nao watu.[#2 Fal. 24:8-9.]
7Akayajua majumba yao, akaiangamiza miji yao, nchi akaigeuza kuwa peke yake tu, waliojaa huko wakitoweka kwa kuziogopa sauti za ngurumo zake.
8Ndipo, wamizimu walipotoka katika nchi zao, wakajipanga na kumzunguka, wakamtegea nyavu zao, wakamchimbia nao mwina, akanaswa humo.
9Kisha wakamtia pete puani, wakamtia katika tundu kubwa, wakampeleka kwa mfalme wa Babeli, wakampeleka kweli, mpaka wakamweka bomani, kusudi sauti zake zisisikilike tena katika miji ya Isiraeli.
10Mama yako alikuwa kama mzabibu shambani kwa mizabibu yako uliopandwa penye maji, ukazaa matunda, ukawa na matawi mengi, kwani ulikuwa penye maji mengi.[#Ez. 17:6.]
11Ukapata hata fimbo zenye nguvu zilizofaa kuwa bakora za watawala nchi, ukawa mrefu kwa kimo chake, ukayapita majani ya miti iliyoko, ukaonekana mbali kwa urefu wake na kwa wingi wa matawi yake.
12Kisha ukang'olewa kwa makali yenye moto, ukatupwa chini, upepo uliotoka maawioni kwa jua ukayanyausha matunda yake, matawi yake yenye nguvu yakavunjwa, yakakauka, kisha moto ukayala.[#Ez. 15:4.]
13Kisha ukapandwa nyikani katika nchi kavu yenye kiu.
14Moto ukatoka katika zile fimbo za matawi yake, ukayala matunda yake, haikuwako tena kwake fimbo yenye nguvu iliyofaa kuwa bakora ya mtawala nchi.
Hili ndilo ombolezo litakalokuwa ombolezo kweli.