Ezekieli 25

Ezekieli 25

Ufunuo wa mambo, Waamoni watakayoyaona.

1Neno la Bwana likanijia la kwamba:

2Mwana wa mtu, waelekezee wana wa Amoni uso wako, uwafumbulie yatakayokuwa![#Ez. 21:28-32; Yer. 49:1-6.]

3Waambie wana wa Amoni: Lisikieni neno la Bwana Mungu! Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa ulipazomea Patakatifu pangu, palipotiwa uchafu, kwa kuwa uliizomea nayo nchi ya Isiraeli, ilipoangamizwa, ukawagutia nao walio mlango wa Yuda, walipotekwa na kuhamishwa,[#Ez. 36:2; Omb. 2:16.]

4kwa hiyo utaniona, nikikutia mikononi mwao watakao maawioni kwa jua, waichukue nchi yako, iwe yao, wayapige mahema yao kwako, waitumie nchi yako kuwa makao yao; hao ndio watakaoyala matunda yako, tena ndio watakaoyanywa maziwa yako.

5Nao mji wa Raba nitautoa kuwa malisho ya ngamia, navyo vijiji vya wana wa Amoni vitakuwa matulio ya makundi ya mbuzi na kondoo. Ndipo mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.

6Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa ulipiga makofi pamoja na kupiga shindo kwa miguu yako, ukafurahi kwa moyo wako wote ulio wenye mabezo kwa ajili ya nchi ya Isiraeli,

7kwa hiyo utaniona, nikikukunjulia mkono wangu, nikutolee mataifa mengine, wakunyang'anye, kisha nitakuangamiza kwenye makabila ya watu, nikupoteze na kukutowesha katika nchi hizi. Ndipo, utakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.

Ufunuo wa mambo, Wamoabu na Waedomu watakayoyaona.

8Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa Wamoabu na Waseiri husema: Tazameni, mlango wa Yuda unafanyiziwa kama mataifa yote,[#Yes. 15; Yer. 48.]

9kwa hiyo mtaniona, nikiufunua ubavu wake Moabu kuanzia kwenye miji, kwenye ile miji yake iliyoko mipakani, iliyokuwa urembo wa nchi, kama Beti-Yesimoti na Baali-Meoni na Kiriataimu.

10Nchi yao nitaitoa nayo yao wana wa Amoni, niwape watokao maawioni kwa jua, iwe yao, kusudi wana wa Amoni wasikumbukwe tena kwenye mataifa.

11Wamoabu nao nitawahukumu; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana

12Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa Waedomu walijilipiza kwao wa mlango wa Yuda na kuwatoza malipizi, wamekora manza papo hapo, walipojilipiza kwao.[#Sh. 137:7; Yer. 49:7-22; Oba. 1-21.]

13Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Nitaikunjulia nchi ya Waedomu mkono wangu niangamize kwake watu na nyama, niigeuze kuwa mabomoko tu, kuanzia Temani mpaka Dedani watu watauawa kwa panga.

14Nami nitawatia mikononi mwao walio ukoo wangu wa Isiraeli, wawatoze malipizi, niyatakayo, wakiwafanyizia Waedomu mambo, machafuko yangu makali yenye moto yanayoyataka, wapate kujua, ya kuwa lipizi ni langu mimi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu[#5 Mose 32:35.]

Ufunuo wa mambo, Wafilisti watakayoyaona.

15Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kwa kuwa Wafilisti waliendelea kujilipiza, wakijilipiza na kutoza malipizi kwa mioyo yenye mabezo, wakayazidisha mabaya yao kwa kushika machukio ya kale na kale,[#Yes. 14:29; Yer. 47; Sef. 2:5.]

16kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Mtaniona, nikiwakunjulia Wafilisti mkono wangu, niwaangamize hao Wakreta na kuyapoteza masao yao yaliyoko pwani kwenye bahari.[#1 Sam. 30:14.]

17Nami nitawatoza malipizi makubwa na kuwapiga kwa makali yenye moto. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapowatoza malipizi yangu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania