The chat will start when you send the first message.
1Ikawa katika mwaka wa 25 wa kuhamishwa kwetu, mwaka ulipoanza, siku ya kumi ya mwezi, nao ulikuwa mwaka wa 14 wa kutekwa kwa huo mji, siku ileile ndipo, mkono wa Bwana uliponishika, ukanipeleka huko.
2Katika maono ya Kimungu akanipeleka katika nchi ya Waisiraeli, akaniweka katika mlima mrefu sana, nitulie huko; upande wake wa kusini kulikuwako yaliyofanana na majengo ya mji.
3Alipokwisha kunipeleka huko, mara nikaona mtu, akaonekana kuwa kama wa shaba, mkononi mwake alishika kamba ya katani na mwanzi wa kupimia, naye alikuwa amesimama langoni.[#Ez. 47:3; Zak. 2:1; Ufu. 21:15.]
4Akaniambia yule mtu: Mwana wa mtu, tazama kwa macho yako, tena sikiliza kwa masikio yako! Nao moyo wako uuelekeze kuyaangalia yote, nitakayokuonyesha! Kwani umeletwa huku, kusudi uonyeshwe mambo; yote, utakayoyaona huku, uwatangazie walio ukoo wa Isiraeli![#Ez. 44:5.]
5Nikaona ukuta wa nje ulioizunguka Nyumba pande zote pia. Nao mwanzi wa kupimia ulikuwa mkononi mwake yule mtu, ulikuwa wa mikono sita kama mkono wa mtu na upana wa shubiri moja; akaupima upana wa ukuta, ulikuwa mwanzi mmoja, nao urefu wake wa kwenda juu ulikuwa mwanzi mmoja.
6Kisha akaenda kwenye jengo la lango lililoelekea maawioni kwa jua, akavipanda vipago vyake, akakipima kizingiti cha jengo la lango, upana wake ulikuwa mwanzi mmoja; kizingiti hiki kimoja kilikuwa kwa upana mwanzi mmoja.
7Nacho chumba kimoja urefu wake ulikuwa mwanzi mmoja nao upana wake vilevile mwanzi mmoja, tena katikati ya vyumba kulikuwa mikono mitano. Kizingiti cha jengo la lango lililokuwa penye ukumbi, lililoelekea nyumbani, kilikuwa nacho mwanzi mmoja.
8Akaupima ukumbi wa lile jengo la lango wa upande wa nyumbani, nao ulikuwa mwanzi mmoja.
9Akaupima nao ukumbi wa lile jengo la lango wa upande wa mbele, nao ulikuwa mikono minane, nayo miimo yake ilikuwa mikono miwili, nao lukumbi huo ulikuwa upande wa nyumbani.
10Navyo vyumba vya jengo la lango hili lililoelekea maawioni kwa jua vilikuwa vitatu upande wa huku, tena vitatu upande wa huko, kipimo cha hivi vitatu kilikuwa hicho kimoja, hata kipimo cha miimo ya huku na ya huko kilikuwa hicho kimoja.
11Akaupima upana wa hapo pa kuingia, langoni nao ulikuwa mikono kumi, urefu wa lile lango ulikuwa mikono kumi na mitatu.
12Mbele ya vile vyumba palikuwa pamekatwa mipaka, urefu wao wa juu upande wa huku mkono mmoja, nao upande wa huko vilevile mkono mmoja; kila chumba kilikuwa mikono sita upande wa huku na mikono sita upande wa huko.
13Kisha akalipima jengo la lango toka dari la chumba hata dari la lchumba cha ng'ambo mikono ishirini na mitano, mlango ukiuelekea mlango wenziwe.
14Akafanya nguzo za mikono sitini; penye hizo nguzo ua ulilizunguka jengo la lango pande zote.
15Toka hapo pa kuingia langoni mpaka upande wa mbele wa ukumbi wa lango la ndani ilikuwa mikono hamsini.
16Madirisha yenye vyuma yalikuwa kwenye vyumba na kwenye miimo upande wa ndani wa hilo jengo la lango po pote; nao ukumbi ulikuwa na madirisha po pote yaliyoelekea ndani. Penye nguzo palikuwa pamechorwa mitende.
17Kisha akanipeleka katika ua wa nje, nikaona huko vyumba, tena chini palikuwa pametengenezwa sakafu kuzunguka pande zote uani; hapo penye sakafu palikuwa na vile vyumba, navyo vilikuwa thelathini.
18Hiyo sakafu ilikuwa kando penye malango, ikalingana na urefu wa majengo ya malango, ndiyo sakafu ya ua wa chini.
19Akaupima upana toka upande wa ndani wa jengo la lango la ua wa chini mpaka upande wa mbele wa jengo la lango la ua wa ndani mikono mia; vilikuwa hivyo upande wa maawioni kwa jua na upande wa kaskazini.
20Nalo jengo la lango la ua wa nje lililoelekea kaskazini akalipima urefu wake na upana wake.
21Vyumba vyake vilikuwa vitatu upande wa huku, tena vitatu upande wa huko; nazo nguzo zake na ukumbi wake kipimo chao kilikuwa kilekile cha jengo la mlango la kwanza. Urefu wake ulikuwa mikono hamsini, nao upana wake ulikuwa mikono ishirini na mitano.
22Madirisha yake na ukumbi wake na machoro ya mitende kipimo chao kilikuwa kilekile cha jengo la lango lililoelekea maawioni kwa jua; kwa vipago saba watu wakalipandia, kisha ukumbi wake ulikuwa mbele yao.
23Tena kulikuwako jengo la lango la ua wa ndani lililoelekea sawasawa jengo la lango la upande wa kaskazini na jengo la lango la upande wa maawioni kwa jua, akapima toka lango hata lango mikono mia.
24Akaniongoza njia ya kwenda kusini, nikaona, hata katika hiyo njia ya kwenda kusini kulikuwako jengo la lango, akazipima nguzo zake na ukumbi wake, kipimo chao kilikuwa kilekile.
25Hata madirisha yalilizunguka hilo jengo la lango na ukumbi wake pande zote, kama yale madirisha mengine yalivyokuwa, nao urefu ulikuwa mikono hamsini, nao upana ulikuwa mikono ishirini na mitano.
26Napo hapo palikuwa na vipago saba vya kupapandia, nao ukumbi wake ulikuwa mbele yao, nao ulikuwa na machoro ya mitende kwenye nguzo zake upande wa huku na upande wa huko.
27Tena kulikuwako hata jengo la lango la ua wa ndani katika hiyo njia ya kwenda kusini, akapima toka lango hata lango katika hiyo njia ya kwenda kusini mikono mia.
28Akanipeleka katika ua wa ndani kwenye njia ya kwenda kusini, akalipima hilo jengo la lango la kusini, vipimo vyake vilikuwa vile vile,
29Navyo vyumba vyake na nguzo zake na ukumbi wake vipimo vyao vilikuwa vilevile. Hata madirisha yalilizunguka hilo jengo la lango na ukumbi wake pande zote; nao urefu ulikuwa mikono hamsini, nao upana ulikuwa mikono ishirini na mitano.
30Pande zote palikuwa na vyumba, urefu ulikuwa mikono ishirini na mitano, nao upana ulikuwa mikono mitano.
31Ukumbi wake uliuelekea ua wa nje, nayo machoro ya mitende yalikuwa penye nguzo zake, tena hapo palikuwa na vipago vinane vya kupapandia.
32Kisha akanipeleka katika ua wa ndani penye njia ya maawioni kwa jua, akalipima jengo la lango vipimo vyake vilikuwa vilevile.
33Navyo vyumba vyake na nguzo zake na ukumbi wake vilikuwa vilevile. Hata madirisha yalilizunguka hilo jengo la lango na ukumbi wake pande zote. Urefu ulikuwa mikono hamsini, nao upana ukikuwa mikono ishirini na mitano.
34Ukumbi wake uliuelekea ua wa nje, nayo machoro ya mitende yalikuwa penye nguzo zake upande wa huku na upande wa huko, napo hapo palikuwa na vipago vinane vya kupapandia.
35Kisha akanipeleka penye jengo la lango la kaskazini, akalipima, vipimo vyake vilikuwa vilevile.
36Vyumba vyake na nguzo zake na ukumbi wake ni vivyo hivyo, nayo madirisha yalilizunguka pande zote; urefu ulikuwa mikono hamsini, nao upana ulikuwa mikono ishirini na mitano.
37Ukumbi wake uliuelekea ua wa nje, nayo machoro ya mitende yalikuwa penye nguzo zake upande wa huku na wa huko, napo hapo palikuwa na vipago vinane vya kupapandia.
38Hapo palikuwa na chumba, pake pa kuingilia palikuwa ukumbini mwa hayo malango, ndimo walimozisafishia nyama za kuteketezwa nzima za tambiko.
39Mle ukumbini mwa jengo la lango mlikuwa na meza mbili upande wa huku, tena meza mbili upande wa huko; ndipo, walipoziandalia ng'ombe za tambiko zilizochinjwa za kuteketezwa nzima nazo za weuo nazo za upozi.
40Tena upande wa nje pa kupandia napo pa kuliingilia jengo la lango la kaskazini palikuwa na meza mbili, nao upande mwingine wa ukumbi wa hilo jengo la lango palikuwa na meza mbili tena.
41Pamoja zilikuwa meza nne upande wa huku na meza nne upande wa huko kando ya hilo jengo la lango, zote pamoja zilikuwa meza nane; ndipo, walipoziandalia nyama zilizochinjwa.
42Tena palikuwa na meza nne za nyama za tambiko zilizoteketezwa nzima, zilijengwa kwa mawe yaliyochongwa, urefu wao ulikuwa mkono mmoja na nusu nao upana ulikuwa mkono mmoja na nusu, nao urefu wa kwenda juu ulikuwa mkono mmoja; ndipo, walipoviweka vyombo vya kuchinjia nyama wa kuteketezwa nzima na nyama wengine wa tambiko.
43Upande wao wa ndani palikuwa pametiwa mambo, urefu wao shibiri moja pande zote; hizo meza zilikuwa za kuwekea nyama, walizomtolea Mungu.
44Upande wa nje wa kila jengo la lango la ndani palikuwa na vyumba vya waimbaji katika ua wa ndani, kimoja kando ya jengo la lango la kaskazini kilielekea kusini, kimoja kilikuwa kando yake jengo la lango la maawioni kwa jua, nacho kilielekea kaskazini.
45Akaniambia: Hiki chumba kinachoelekea kusini ni cha watambikaji wanaongoja zamu humu Nyumbani.
46Nacho chumba kinachoelekea kaskazini ni cha watambikaji wanaongoja zamu mezani pa kutambikia, ndio wana wa Sadoki, ndio wanaomkaribia Bwana peke yao katika wana wa Lawi, wamtumikie.[#Ez. 43:19; 44:15; 1 Fal. 1:8,39; 1 Mambo 6:8.]
47Akaupima huo ua ulikuwa wenye pembe nne, urefu wake ulikuwa mikono mia, nao upana wake ulikuwa mikono mia. Nayo meza ya kutambikia ilikuwa mbele ya Nyumba.[#Ez. 43:13.]
48Akanipeleka penye ukumbi wa Nyumba, akaupima unene wa miimo ya huo ukumbi, ulikuwa mikono mitano upande wa huku, tena mikono mitano upande wa huko, nao upana wa lango ulikuwa mikono kumi na minne, nazo kuta za kando ya jengo la lango upande wa ndani zilikuwa mikono mitatu upande wa huku na mikono mitatu upande wa huko.[#1 Fal. 6:3.]
49Urefu wa ukumbi ulikuwa mikono ishirini, nao upana wake mikono kumi na miwili, tena hapo palikuwa na vipago vya kupapandia, tena penye miimo palikuwa na nguzo, moja upande wa huku na moja upande wa huko.[#1 Fal. 7:21.]