The chat will start when you send the first message.
1Kisha akanipeleka katika ua wa nje penye njia ya kwenda kaskazini, akanipeleka penye vyumba vilivyopaelekea hapo palipokatazwa watu, tena vililielekea jengo lililoko upande wa kaskazini.
2Upande wa mbele urefu wake ulikuwa mikono mia hapo pa kuingia upande wa kaskazini, nao upana wake ulikuwa mikono hamsini.[#Ez. 41:13.]
3Kuielekea ile mikono ishirini ya ua wa ndani, tena kuielekea sakafu ya mawe ya ua wa nje palikuwa na baraza juu ya baraza penye madari matatu.[#Ez. 40:17; 41:10.]
4Mbele ya hivyo vyumba palikuwa pa kupitia palipouelekea ua wa ndani; upana wake ulikuwa mikono kumi, nao urefu wake hiyo njia ulikuwa mikono mia moja, nayo milango ya zile baraza ilielekea kaskazini.[#Ez. 42:11.]
5Navyo vyumba vya juu vilikuwa vimekatwa kidogo kwa upana wao, kwani zilipunguzwa na zile baraza zilizopita mbele yao, vilikuwa vifupi kuliko vile vya chini na vya kati vya hilo jengo.
6Kwani vilikuwa vya madari matatu, nayo yalikuwa hayana nguzo kama nguzo za uani; kwa hiyo lvya juu vilipunguzwa upana toka chini kuliko vya chini na vya katikati.
7Tena palikuwa na kitalu nje kilichokwenda sawasawa na vile vyumba upande wa ua wa nje mbele ya vyumba, urefu wake ulikuwa mikono hamsini.
8Kwani urefu wa vyumba vilivyokuwa upande wa ua wa nje ulikuwa mikono hamsini, lakini vile vilivyokuwa upande wa Patakatifu urefu wao ulikuwa mikono mia.
9Chini yao hivyo vyumba palikuwa pa kuingia upande wa maawioni kwa jua, mtu akitoka katika ua wa nje.
10Sawasawa na hicho kitalu kilichokuwa hapo uani, lakini upande wa kusini, palikuwa na vyumba vilivyopaelekea hapo palipokatazwa watu na hapo penye jengo lile.
11Mbele yao palikuwa pa kupitia; ukipatazama, palikuwa na vyumba kama vile vya upande wa kaskazini, urefu wao na upana wao ni uleule, nazo njia zao zote za kutoka na mambo mengine yalikuwa yaleyale. Nayo milango yao[#Ez. 42:4.]
12ilikuwa kama milango ya vyumba vilivyoelekea kusini; pa kuingia palikuwa pembeni pa njia iliyokwenda mbele ya kitalu kilichokuwa sawa kama kile cha upande wa kaskazini, mtu akiishika ile njia ya upande wa maawioni kwa jua, afike hapo.
13Kisha akaniambia: Vyumba vya upande wa kaskazini, hata vyumba vya upande wa kusini vilivyopaelekea palipokatazwa watu, ndivyo vyumba vitakatifu; ndimo, watambikaji watakamokula vyakula vitakatifu vyenyewe, tena ndimo, watakamoviweka vipaji vitakatifu vyenyewe, vilaji vya tambiko na nyama za ng'ombe za tambiko za weuo nazo zao za upozi, kwani ndivyo vyumba vitakatifu.
14Watambikaji wakitaka kuingia humo, wasitoke Patakatifu na kupitia penye ua wa nje! Humo ndimo, wayaweke mavazi yao waliyoyavaa wakimtumikia Mungu, kwani nayo ni matakatifu. Sharti wavae mavazi mengine, kisha wapakaribie, watu walipo!
15Alipokwisha kuipima Nyumba upande wa ndani, akanitoa humo na kunipeleka nje penye jengo la lango lililoelekea maawioni kwa jua, akaipima pande zote kuizunguka.
16Akaupima upande wa maawioni kwa jua kwa ule mwanzi wa kupimia, nao ulikuwa wote pia mianzi mia tano kwa kupima na ule mwanzi.
17Akaupima upande wa kaskazini, nao ulikuwa wote pia mianzi mia tano kwa kupima na ule mwanzi.
18Akaupima upande wa kusini, nao ulikuwa mianzi mia tano kwa kupima na ule mwanzi.
19Akazunguka penye upande wa baharini, akaupima, nao ulikuwa mianzi mia tano kwa kupima na ule mwanzi.
20Alipopapima pande zote nne penye ukuta uliopazunguka, urefu wake ulikuwa po pote mia tano, nao upana wake ulikuwa mia tano kupatenga Patakatifu napo penye watu.