The chat will start when you send the first message.
1Akaniongoza tena kwenda penye lile lango lililoielekea njia ya maawioni kwa jua.
2Nilipotazama mara nikaona, utukufu wa Mungu wa Isiraeli ukija katika njia itokayo maawioni kwa jua, nao uvumi wake ulikuwa kama uvumi wa maji mengi, nayo nchi iliangaza kwa utukufu wake.
3Ulionekana kuwa kama lile ono, nililoliona, ulikuwa kweli kama lile ono, nililoliona nilipokuja kuuangamiza huo mji; tena ulionekana kuwa kama lile ono, nililoliona huko kwenye mto wa Kebari, nikaanguka kifudifudi.[#Ez. 1:8-11.]
4Nao utukufu wa Bwana ukaja kuingia humo Nyumbani katika njia ya lango lililoielekea hiyo njia ya maawioni kwa jua.[#Ez. 10:19; 11:22-23.]
5Ndipo, roho iliponichukua, ikanipeleka katika ua wa ndani, mara nikaona, utukufu wa Bwana ulivyoijaza Nyumba.[#2 Mose 40:34; 1 Fal. 8:10-11.]
6Nikasikia aliyesema na mimi toka mle Nyumbani, tena kulikuwako mtu aliyesimama hapo, nilipokuwa.
7Akaniambia: Mwana wa mtu, hapa ndipo penye kiti changu cha kifalme napo penye nyayo za miguu yangu; ndipo, nitakapokaa kale na kale katikati ya wana wa Isiraeli. Walio wa mlango wa Isiraeli hawatalipatia tena Jina langu takatifu uchafu, wala wenyewe, wala wafalme wao, wala kwa ugoni wao, wala kwa mizoga ya wafalme wao watakapokufa,[#Sh. 132:13-14.]
8wakiviweka vizingiti vyao penye kizingiti changu nayo miimo yao kandokando penye miimo yangu, pakawa ukuta tu uliopatenga pangu na pao, wakalipatia Jina langu takatifu uchafu kwa machukizo yao, waliyoyafanya; ndipo, nilipowamaliza kwa makali yangu.[#Ez. 8:7-18.]
9Sasa ugoni wao watauondoa pangu pamoja na mizoga ya wafalme wao, nipate kukaa katikati yao kale na kale.
10Wewe mwana wa mtu, walio mlango wa Isiraeli uwapashe habari za Nyumba hii, wapatwe na soni, wayaache maovu yao, waliyoyafanya, kisha waupime vema ulinganifu wake.[#Ez. 16:61,63; 36:32.]
11Nao watakapopatwa na soni, wayaache yale yote, waliyoyafanya, ndipo, utakapowajulisha umbo lake Nyumba hii, ilivyolinganywa, napo pa kuitokea napo pa kuiingilia, jinsi umbo lake lote pia lilivyo! Tena uwajulishe maongozi yalipasayo umbo lake lote na maonyo yake yote ukiyaandika machoni pao, waliangalie umbo lake lote na maongozi yote yalipasayo, wayafanye!
12Haya ndiyo maonyo yaipasayo hii Nyumba: Po pote penye mipaka yake izungukayo huku milimani juu ndipo Patakatifu penyewe. Yaangalieni haya maonyo yaipasayo Nyumba hii!
13Hivi ndivyo vipimo vyake pa kumtambikia Bwana vya kupapima kwa mikono, mkono ukiwa mkono wa mtu na upana wa shibiri: msingi ni mkono mmoja, nao upana wake ni mkono mmoja, tena pembeni pake panazunguka kitalu, urefu wake ni shibiri moja. Nao huu ndio urefu wa juu wa hapo pa kutambikia:[#Ez. 40:47; 2 Mose 27:1-8.]
14toka msingi ulioko mchangani mpaka daraja ya chini ni mikono miwili, nao upana wake mkono mmoja; tena toka daraja hili dogo mpaka daraja kubwa ni mikono minne, nao upana wake mkono mmoja.
15Kisha kilima cha Mungu ni mikono minne, tena hapo jikoni pa Mungu palikuwa na pembe nne zilizoelekea juu.
16Nalo jiko la Mungu ni mikono kumi na miwili urefu wake, nao upana wake ni mikono kumi na miwili, pande zake nne ni sawa, zenye pembe nne.
17Lile daraja kubwa urefu wake ni mikono kumi na minne, nao upana wake ni mikono kumi na minne, pande zake nne ni sawa; nacho kitalu kinacholizunguka ni nusu ya mkono, nao msingi wake po pote ni mkono mmoja; navyo vipago vya kupapandia viko upande wa maawioni kwa jua.
18Kisha akaniambia: Mwana wa mtu, hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu: Haya ndiyo, ninayokuagiza kuyafanya siku ile, hapo pa kunitambikia patakapokwisha kutengenezwa, watoe juu yake ng'ombe za tambiko pamoja na kupanyunyizia damu.
19Ndipo, utakapotoa ndama ya ng'ombe ya kiume kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, uwape watambikaji wa Kilawi walio wa uzao wa Sadoki, maana ndio wanaonikaribia na kunitumikia; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#2 Mose 2:9; Ez. 40:46.]
20Kisha sharti uchote damu katika damu yake, uinyunyizie pembe zake nne napo penye zile pembe nne za daraja napo penye kitalu kipazungukacho! Ndivyo, utakavyopaeua pamoja na kupapatia upozi.
21Kisha umchukue huyo ndama atakayekuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, umteketeze penye Nyumba hii hapo panapoitumikia kazi hii upande wa nje wa hapo Patakatifu.
22Siku ya pili sharti upeleke dume la mbuzi asiye na kilema, wapaeue hapo pa kutambikia kama walivyopaeua na kumtoa yule ndama.
23Utakapokwisha kupaeua, sharti upeleke ndama ya ng'ombe ya kiume asiye na kilema na dume la kondoo asiye na kilema.
24Hao uwapeleke wa kuwatoa usoni pa Bwana, kisha watambikaji wawamwagie chumvi na kumtolea Bwana kuwa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima.
25Sharti ufanye hivyo siku saba, wakitoa kila siku dume la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo pamoja na ndama ya ng'ombe ya kiume na dume la kondoo; hao wote, watakaowatoa, sharti wawe nyama pasipo kilema.
26Sharti siku saba wapapoze hapo pa kutambikia na kupaeua hivyo. Ndivyo, watakavyopatakasa, pawe patakatifu.[#2 Mose 28:41.]
27Watakapozimaliza hizo siku, basi, siku ya nane nazo siku zitakazokuwa zote watambikaji watolee hapo pa kutambikia ng'ombe zenu za tambiko za kuteketezwa nzima nazo za kushukuru; ndipo, nitakapopendezwa nanyi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.